• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Huenda mabwanyenye waliotekwa na Kang’ata ni njama kupangia Ruto mahesabu kuenda nyumbani?

Huenda mabwanyenye waliotekwa na Kang’ata ni njama kupangia Ruto mahesabu kuenda nyumbani?

NA MWANGI MUIRURI 

HATUA ya Gavana wa Murang’a, Irungu Kang’ata kuteua vigogo waliokuwa makuhani wakuu ndani ya mrengo wa Azimio katika uchaguzi mkuu wa 2022 imetafsiriwa kuwa ya kisiasa na inayolenga manufaa ya 2027.

Bw Kang’ata amewaingiza serikalini vigogo kadha waliokuwa nguzo muhimu kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa pamoja wakimpigia debe Raila Odinga ashinde urais.

Aliyekuwa mwenyekiti wa benki ya Equity Bw Peter Munga, mdosi wa kampuni ya Dyer and Blair Bw Jimnah Mbaru, pamoja na mwekezaji tajika katika sekta ya uanahabari Bw Samuel (SK) Macharia ni miongoni mwa mabwanyenye 15 ambao wameteuliwa na Gavana Kang’ata katika kamati ya ushauri wa kimaendeleo.

Bw Kang’ata amesema kwamba harakati zake zinalenga kuvuna maarifa na busara ya vigogo hao katika safu ya kuunda mikakati ya kibajeti na ubunifu wa kimaendeleo.

Ameongeza kuwa kundi hilo halitakuwa likilipwa mishahara au marupurupu, wadadisi wakisema kwamba huenda watumike katika ushirikiano wa sekta za umma na za kibinafsi katika mianya ya viwanda.

Huku uchaguzi mkuu wa 2017 ukianza kujiweka wazi kwamba utakuwa wa kupiga msasa utawala wa Rais William Ruto kwa ujumla, hali tete imeanza kujiangaza kwa baadhi ya wandani wake hasa Mlima Kenya.

“Huenda uchaguzi mkuu wa 2027 uwe wa kuadhibu au kuzawadi utawala wa Rais Ruto. Hali hadi sasa ni mbaya na asipotafuta mbinu ya haraka ya kufurahisha Mlima Kenya, basi tutapungiana mkono wa kwaheri 2027,” asema aliyekuwa Waziri msaidizi (CAS) Bw Zack Kinuthia.

Bw Kinuthia alisema kwamba “haikosi siasa za kujiokoa katika hatua ya Bw Kang’ata ya kuwateua wandani wa awali au hadi sasa katika serikali yake akilenga idadi sawa za kujipa afueni”.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto alipata asilimia 81 ya kura za Murang’a huku Bw Odinga akipata asilimia 17.

Mabwanyenye hao wa Murang’a waliimarisha kampeni za Bw Odinga eneo la Mlima Kenya na hata ingawa aliangukia pua, alipata kura ambazo katika uwaniaji wake wa awali hakuwa akizikaribia.

“Hesabu za siasa ni kwamba, katika ile hali ya kupoteza umaarufu ndani ya mrengo wa Rais Ruto huenda apate fidia kutoka kwa mrengo wa Azimio na pia kuhakikisha wapinzani wake watakuwa hafifu,” asema mwenyekiti wa vuguvugu la vijana wa UDA eneo hilo Bw Martin Warui.

Bw Warui anasema kwamba “watu hao, Bw Kang’ata amewavuta kwake wanajulikana pia na kuwa na ukwasi mkuu ambao huenda umfae katika kuweka bajeti ya kusaka awamu ya pili afisini”.

Bw Warui,  aidha, alisema Bw Macharia anawakilisha miundombinu sambamba ya kupigia mradi debe kupitia ueledi wa utangazaji.

“Hata tunaposema kwamba teuzi hizo ni za kimaendeleo, huwezi ukatenganisha hali hiyo na siasa za kujinusuru katika kuendeleza ubabe wa sasa na wa baadaye ikizingatiwa kwamba Bw Kang’ata anahudumu muhula wa kwanza huku sheria ikimpa ruhusa ya kuhudumu hadi 2032 iwapo atawania 2027 na ashinde,” akasema Prof Ngugi Njoroge.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Karisa Nzai ateuliwa kama msemaji wa Mijikenda

Kenya Power yakashifiwa kwa utepetevu stima zikipotea kwa...

T L