• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Handisheki ya kisiri ilishafanyika kitambo, ni picha hazikupigwa, Kanini Kega adai

Handisheki ya kisiri ilishafanyika kitambo, ni picha hazikupigwa, Kanini Kega adai

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega ameiponda serikali ya Rais William Ruto anayoishutumu kwa kuzidi kukandamiza eneo la Mlima Kenya huku akidai kiongozi wa nchi tayari ameshafanya handisheki ya kisiri na kinara wa Azimio Raila Odinga.

Mbunge huyo wa EALA vilevile ametangaza kuwa chama cha Jubilee kitawasilisha mgombea wa urais 2027, huku akimlaumu Rais Ruto kwa kuwatenga watu kutoka Eneo la Kati na kuwapokonya nyadhifa serikalini.

“Rais William Ruto na Raila Odinga walifanya handisheki kitambo. Ni vile tu mara hii, handisheki haikupigwa picha nje ya Jumba la Harambee,” alisema Bw Kega akizungumza Jumatatu Oktoba 23, 2023 asubuhi katika runinga ya Inooro.

“Ruto anakaribishwa na kukumbatiwa na viongozi kutoka eneo la Nyanza kwenye mikutano ya hadhara. Je, vipi kuhusu Gachagua wetu? Hatupaswi kuonekana kana kwamba ni sisi tu tunaopinga umoja wa kitaifa!”

Bw Kega vilevile alionekana kumwondolea lawama kinara wa Azimio kuhusu matatizo yanayokumba eneo la Kati.

Aidha, amewataka wanasiasa walioendeleza dhana ya kumpiga vita Rais Uhuru Kenyatta kuhusu gharama ya juu ya maisha kuomba radhi akisema Wakenya wangali wanateseka huku serikali ya UDA ikifanya mambo yale yale yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake.

“Wanasiasa wa Mlima Kenya wamekuwa wakiendesha kasumba kuwa matatizo ya eneo hili yamesababishwa na Raila Odinga. Sasa wamekumbana na uhalisia kuwa changamoto za Mlima Kenya zinatokana na mapato duni ya kilimo, ukosefu wa ajira, unywaji pombe, mihadarati, sera duni za kibiashara masuala ambayo hayamhusu Bw Odinga.”

“Rais Ruto anawafuta kazi serikalini watu kutoka Mlima Kenya bila kujaza nafasi zao na watu kutoka eneo hilo. Stima zilipopotea nchini kote, aliwafuta kazi wafanyakazi kwenye uwanja wa ndege kutoka eneo letu ilhali stima hazizalishwi wala kuunganishiwa katika uwanja wa ndege!”

Kuhusu aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria, Bw Kega alisema kuwa Bw Kuria aliyehamishiwa Wizara ya Utumishi wa Umma, alifeli kuipigia debe Kenya kama kivutio kikuu cha kibiashara katika eneo la Afrika Mashariki.

“Katika muda wote alioongoza Wizara hiyo, hakuwahi kuhudhuria mkutano hata mmoja wa kupanga mikakati ya jinsi Kenya ingenufaika kutokana na nafasi zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Huku akionya kuhusu utengano katika eneo la Kati, alitoa wito kwa baraza la wazee wa jamii hiyo kukubali kupitisha usukani kwa Naibu Rais Gachagua kuwa msemaji wa Mlima Kenya kutoka kwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Akizungumzia kuhusu misukosuko inayokumba chama cha Jubilee, Bw Kega ametoa wito kwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula kutangaza rasmi chama hicho kuwa kinachojisimamia.

Alisema hatua hiyo itamwezesha mbunge Maalum wa Kaunti ya Murang’a Sabina anayepigwa vita na Azimio kama Naibu Kiranja wa Walio Wachache kuchukua usukani kama Kiranja wa Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua azuru Ulaya huku Rais akitua Saudia licha ya...

Mtoto aaga dunia kwa kukosa kuhudumiwa hospitalini kwa saa...

T L