• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:40 PM
JUNGU KUU: Magavana walioshindwa sumu kwa wale wa sasa

JUNGU KUU: Magavana walioshindwa sumu kwa wale wa sasa

Na BENSON MATHEKA

MAGAVANA waliohudumu kwa muhula mmoja kuanzia 2013 hadi 2017 wanakabiliwa na wakati mgumu wakitaka kugombea kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2022.

Tayari baadhi ya magavana hao walioweka msingi wa ugatuzi katika kaunti zao wameelezea nia ya kuomba wapigakura wawape nafasi nyingine baada ya kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Ingawa kuna walio na nafasi ya kushinda wapinzani wao, wadadisi wanasema haitakuwa rahisi kwa baadhi yao hasa baada ya kiti hicho kuvutia viongozi wapya wakiwemo wabunge, maseneta, madiwani, maafisa wakuu serikalini kama makatibu wa wizara na wakurugenzi wa mashirika makubwa ambao wamejenga umaarufu mashinani.

“ Vile vile, magavana wanaohudumu kwa muhula wa kwanza wamekita mizizi ikizingatiwa kuwa walijifunza mengi kutoka kwa watangulizi hao wao, wakirekebisha makosa yanayoweza kuwafanya wakose kuhifadhi viti vyao ikiwemo kuhakikisha wamejiunga na vyama vya kisiasa na mirengo maarufu katika maeneo yao,” asema mchanganuzi wa siasa, James Warukira.

Baadhi ya waliokuwa magavana wa kwanza wa kaunti wanaomezea mate viti hivyo tena kwenye uchaguzi wa mwaka huu wameunda vyama vyao ili kuepuka ushindani kwenye mchujo ambao walidai ulitumiwa kuwanyima nafasi ya kushinda muhula wa pili.

Miongoni mwa walio na vyama vyao vya kisiasa ni William Kabogo (Kiambu, Tujibebe Wakenya Party), Ukur Yatani ( Marsabit, Upya Party), Isaac Ruto (Bomet, Chama cha Mashinani) na Peter Munya wa Meru, (Party of National Unity).

Kulingana na Bw Warukira, hatua ya magavana hao wa zamani kubuni vyama vya kisiasa ni kuepuka mchujo wa vyama vikubwa vya kisiasa ambao kwa kawaida huwa na ushindani mkali. Magavana wengine wa zamani walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 ni Evan Kidero ambaye amehamisha kambi yake kutoka kaunti ya Nairobi hadi Homa Bay kuliko na ushindani mkali kutoka kwa Mwakilishi wa Wanawake wa eneo hilo Glady’s Wanga, mwenyekiti wa chama cha ODM John Mbadi na mfanyabiashara Oyugi Magwanga ambaye aliibuka wa pili kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

John Mrutu aliyeshindwa na mtangazaji Granton Samboja kwenye uchaguzi wa kiti hicho kaunti ya Taita Taveta, Cleophas Langat aliyeshindwa na gavana wa sasa wa Nandi, Stephen Sang na Benjamin Cheboi aliyeshindwa na gavana wa Baringo Stanley Kitis.

Wengine ni Julius Malombe aliyebwagwa na Bi Charity Ngilu kaunti ya Kitui, Simon Kachapin aliyeshindwa na Profesa John Lonyangapuo kaunti ya Pokot Magharibi na David Nkedienye wa Kajiado aliyeangushwa na Joseph Ole Lenku.

Kulingana na Katiba, magavana wanafaa kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka mitano ikifuatana kumaanisha kuwa wakishinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, wanaweza kuhudumu kwa miaka kumi wakichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

“Hii ndiyo inafanya walionuia kugombea urais kama Bw Kabogo kubadilisha nia na kuamua kuwania ugavana. Pia wanatumia udhaifu wa magavana wa sasa,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Okoma.

Okoma anasema kwamba tofauti na mwanzo wa ugatuzi magavana hao walipohudumu, hali imebadilika huku kiti hicho kikivutia watu walio na ushawishi, uwezo na manifesto bora.

“Kinachoweza kuwaokoa ni umaarufu wa mirengo ya vyama watakayojiunga nayo. Wale ambao wana vyama vyao watalazimika kuweka mikakati thabiti kuweza kupenya katika siasa za Kenya zinazotawaliwa na mirengo,” asema Okoma.

Kwa sasa, mirengo miwili mikubwa imeibuka nchini, Azimio la Umoja wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na Hasla wa Naibu Rais William Ruto kupitia chama cha UDA.

You can share this post!

Njonjo alichangia mustakabali mwema wa taifa – Uhuru

MIKIMBIO YA SIASA: OKA ni mnara mpya wa Babeli uchaguzi...

T L