• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
MIKIMBIO YA SIASA: OKA ni mnara mpya wa Babeli uchaguzi ukinukia

MIKIMBIO YA SIASA: OKA ni mnara mpya wa Babeli uchaguzi ukinukia

Na CHARLES WASONGA

HATIMA ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) inaonekana kuyumba mwaka huu mpya na kudidimiza uwezekano wake wa kudhamini mgombeaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hii ni baada ya migawanyiko kuchipuza ndani ya muungano huo huku wabunge wa vyama tanzu wakiugura na kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja.

Kwanza mnamo Ijumaa, Naibu Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Ayub Savula na Mbunge wa Teso Kaskazini Oku Kaunya walitangaza kujiondoa OKA na kujiunga na vuguvugu hilo linaloongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kuanzia leo (Ijumaa) nimetoka katika huo upuzi unaoitwa OKA. Najiunga na Azimio la Umoja chini ya uongozi wa Baba,” akasema Bw Savula alipohutubu katika mkutano wa vuguvugu hilo uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Bukhungu, mjini Kakamega.

Hata hivyo, mbunge huyo wa Lugari alifafanua kuwa atasalia mwanachama wa ANC licha ya kuamua kumuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Kwa upande wake Bw Kaunya alisema alichukua hatua hiyo kutokana na ombi la Bw Odinga huku akimtaka Bw Mudavadi kuungana naye katika kufanikisha ndoto ya waziri huyo mkuu wa zamani kuingia Ikulu.

“Niko hapa kuandaa barabara kwa kiongozi wa chama changu cha ANC Musalia Mudavadi. Nina matumaini kuwa hivi karibuni ataungana nami katika safari hii ya kumpeleka Baba Ikulu,” akasema Bw Kaunya.

Mbunge huyo alimwalika Bw Odinga kuenda Teso huku akiahidi kuingia katika “bedroom yake” sawasawa; kuashiria kuwa huenda akajiunga rasmi na chama cha ODM.

Mbali na wabunge hao, zaidi ya madiwani 10 waliochaguliwa kwa tiketi za vyama vya ANC na Ford Kenya walitangaza kujiunga na ODM wakati wa mkutano huo. Walipokelewa rasmi na Naibu Kiongozi wa ODM Gavana Wycliffe Oparanya.

Dalili kwamba mambo hayakuwa shwari yalianza kudhihirika bungeni mnamo Desemba 29, 2021 pale wabunge wa vyama vya ANC, Wiper na Ford Kenya waliposhirikiana na wabunge wa ODM na Jubilee kuwashinda wabunge wa mrengo wa Tangatanga katika vuta nikuvute kuhusiana na mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa.

Ni mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga (Ford Kenya) pekee aliegemea mrengo wa Tangatanga wakati wa upigaji kura kuhusu hoja za marekebisho ya mswada huo.

Hatua ya wabunge wa OKA kushirikiana na wenzao wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, kwa mfano ilikinzana na msimamo wa Bw Mudavadi aliyepinga mswada huo.

Kiongozi huyo wa ANC alidai kuwa mswada huo uliodhaminiwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya “unaupimia hewa” muungano wa OKA kwa kupendekeza kuwa vyama vya kisiasa vinavyotaka kubuni miungano viwasilishe stakabadhi hitajika kwa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu.

“Pendekezo kama hili lina malengo fiche. Kwa mfano, linalenga kutukaba koo katika OKA ili tutaje mgombeaji wetu wa urais haraka si kwa manufaa yetu bali washindani wetu. Nawaomba wabunge wetu kukataa mswada huu,” akasema Bw Mudavadi.

Mchanganuzi wa siasa za Magharibi ya Kenya Martin Andati anasema hatua ya baadhi ya wabunge wa vyama tanzu katika OKA kuamua kujiunga na Azimio la Umoja ni dalili tosha kwamba hali si shwari katika muungano huo mchanga.

“Isitoshe, hatua ya wabunge kama Savula na Kaunya na wengine wengi kuamua kumpigia debe Raila inadhihirisha kuwa wameng’amua kuwa Bw Mudavadi hajaonyesha ukakamavu unaohitajika katika kinyang’anyiro cha urais,” akasema.

“Aidha, hatua ya seneta wa Kakamega Cleophas Malala kumwalika Naibu Rais William Ruto katika mchuano wa soka mjini Mumias ni ishara tosha kwamba amejiunga na mrengo wa Tangatanga. Hali hii bila shaka inahujumu nafasi ya Bw Mudavadi ya kuingia Ikulu,” Bw Andati anaongeza.

Kwa upande wake, mdadisi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema kuwa migawanyiko na ukosefu wa uthabiti ndani ya OKA ni ishara kuwa muungano huo hauwezi kutoa mgombeaji wa urais.

“Hali hii inathibitisha kuwa farasi ni wawili katika kinyang’anyiro cha urais mnamo Agosti 9, 2022. Kwa hivyo, itabidi vinara wa OKA waamue iwapo wataungana na mrengo wa Dkt Ruto au ule wa Raila,” anaeleza.

You can share this post!

JUNGU KUU: Magavana walioshindwa sumu kwa wale wa sasa

TAHARIRI: Ushirikiano unahitajika mno katika elimu 2022

T L