• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Ngilu: Mwanasiasa wa kike mwenye ujasiri wa aina yake

Ngilu: Mwanasiasa wa kike mwenye ujasiri wa aina yake

KWA HISANI YA KYB

WAKATI Charity Kaluki Ngilu alipogombea urais 1997, yeye na mshindi wa nobeli Wangari Maathai waliandikisha historia kwa kuwa wanawake wa kwanza Kenya kufanya zaidi ya kuota tu kuhusu jambo hilo.

Wakati huo kulikuwa na mwanamke mmoja katika baraza la mawaziri, Nyiva Mwendwa, aliyekuwa ameteuliwa waziri wa utamaduni na huduma za jamii mwaka wa 1995, na kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa waziri Kenya.

Kisadfa, Mwendwa pia anatoka Kitui na mwanafunzi wa zamani wa shule ya wasichana ya Alliance. Mbali na Mwendwa, kulikuwa na wanawake wachache katika bunge.

Kulikuwa na wanawake wachache katika historia ya Kenya kushikilia nyadhifa za juu serikalini; wanawake kama mameya Grace Onyango na Margaret Kenyatta.

Na sasa uwezekano wa mwanamke rais ulikuwa kwa ‘Mama Rainbow’, jinsi Wakenya walivyomuita Ngilu, wakirejelea chama chake cha National Rainbow Coalition.

Kugombea urais kulihitaji ujasiri wa hali ya juu.

Siku chache baada yake kutangaza azma yake, Ngilu alishambuliwa na kujeruhiwa na wakora waliokuwa na mapanga alioamini walikuwa vijana wa chama cha Kenya African National Union (KANU).

Hii ilikuwa baada ya kuzungumza katika mkutano wa kisiasa.

Baadaye alipokea simu ikimtisha kutoka kwa mtu aliyesema, “Kwa hivyo unagombea baada ya kilichofanyika Jumamosi,” Ngilu alisema kwenye mahojiano na New York Times mwaka wa 1998.

Lakini alikuwa mwanamke aliyekuwa na ndoto. Alitaka kuona Kenya ikikombolewa kutoka sheria za usalama za utawala wa Moi, kupitishwa kwa katiba mpya kupunguza nguvu za rais, na kubuni mfumo wa kugawana mamlaka.

“Marais wanafaa kuhudumu na sio kuhudumiwa. Ninataka kubadilisha ofisi hiyo,” alisema.

Hakutimiza azima yake, alipoibuka katika nafasi ya tano katika orodha ya wagombeaji 15 akiwa na kura 469,807.

Hii haikuwa jambo dogo ikizingatiwa nyakati na wapinzani aliokabiliana nao, waliojumuisha rais aliyekuwa mamlakani Daniel Arap Moi, ambaye alikuwa ametawala kwa miaka 20 na vigogo wa siasa kama Mwai Kibaki, Raila Odinga na Michael Wamalwa.

Anaweza kuwa alipoteza katika kura, lakini jaribio la Ngilu lilikuwa ushindi kwa wanawake na wasichana wa Kenya.

Ngilu alichaguliwa mbunge 1992 kwa tiketi ya chama cha Democratic Party kilichoanzishwa na Mwai Kibaki.

Aliwakilisha eneobunge la Kitui ya Kati hadi 2013 alipogombea kiti cha ugavana kaunti ya Kitui.

Mwaka wa 2002, Mwai Kibaki alichaguliwa rais na kuteua baraza lake la mawaziri kwa umakini mkubwa, kwa kuwa alikuwa na malengo ya maendeleo na ahadi za kutimiza.

Ngilu aliteuliwa waziri wa Afya ikiwa mara yake ya kwanza kujiunga na baraza la mawaziri Gideon Konchella akiwa waziri msaidizi wake na Joseph Meme akiwa katibu wa wizara (PS).

Ngilu aliteuliwa tena kusimamia wizara hiyo 2005 waziri msaidizi wa huduma za matibabu akiwa Wilfred Machage na Samuel Moroto wa Afya ya Umma.

Katibu wa wizara alikuwa Hezron Nyagito — mwanauchumi stadi ambaye baadaye aliteuliwa naibu gavana wa Benki Kuu ya Kenya.

Baada ya kuhudumu mwa mihula miwili katika Wizara ya Afya, Ngilu aliteuliwa waziri wa maji na unyunyuziaji 2008 na akaanzisha miradi kadhaa ya maji katika kaunti kame nchini.

Mtetezi shupavu wa wanawake, alikuwa mmoja wa wanawake watatu walioshinda ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

You can share this post!

SOKOMOKO WIKI HII: Wetang’ula atajifua sana kukabili...

Kiini cha Raila kuogopa kuitwa ‘mradi’ wa Uhuru

T L