• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:52 PM
SOKOMOKO WIKI HII: Wetang’ula atajifua sana kukabili mikwaruzo ya ‘chui’

SOKOMOKO WIKI HII: Wetang’ula atajifua sana kukabili mikwaruzo ya ‘chui’

Na LEONARD ONYANGO

BAADA ya kuhangaishwa na kundi la ‘waasi’ kwa zaidi ya mwaka mmoja, kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula sasa amepumua.

‘Waasi’ hao wakiongozwa na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi na mwenzake wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu wamehamia nyumba mpya ya Democratic Action Party – Kenya (DAP-K) – chama kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Wawili hao, walikuwa mwiba kwa Bw Wetang’ula ambaye pia ni kinara wa One Kenya Alliance (OKA).

Bw Wetang’ula amekuwa akidai kuwa misukosuko iliyokumba chama chake cha Simba (Ford Kenya) ilifadhiliwa na kinara wa ODM Raila Odinga.

Viongozi wa chama cha DAP-K kilicho na nembo ya chui, wameapa ‘kumkwaruza’ Bw Wetang’ula katika Uchaguzi Mkuu ujao hadi wapigakura wamkatae.

Tayari wazee wa jamii ya Wabukusu wamemtaka Bw Wetang’ula kuachana na ‘vitisho’ vya kutaka kuwania urais 2022 na badala yake amuunge mkono Bw Odinga.

Bw Wetang’ula ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Sirisia mnamo 2002 kupitia chama cha Ford Kenya, kilichowahi kuongozwa na magwiji wa kisiasa katika eneo la Magharibi Masinde Muliro na aliyekuwa makamu wa Rais Michael Kijana Wamalwa, sasa anadai DAP-K imefadhiliwa na Bw Odinga kwa lengo la kummaliza kisiasa.

Wakenya sasa wanangoja kuona ikiwa chama cha Ford Kenya kilicho na nembo ya Simba kitararuriwa na kucha za chui katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Vilevile, yawezekana chama cha DAP-K ni paka anayedai kuwa chui.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Kiti cha ugavana wa Mombasa chasakwa kwa...

Ngilu: Mwanasiasa wa kike mwenye ujasiri wa aina yake

T L