• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Jay-Z akasirisha kwa jezi ya msikiti Lamu

Jay-Z akasirisha kwa jezi ya msikiti Lamu

Na KALUME KAZUNGU

PICHA ya mwanamuziki mashuhuri wa Amerika Shawn Carter, almaarufu Jay-Z, iliyosambazwa mitandaoni akiwa amevaa tishati iliyo na nembo ya msikiti wa Riyadha ulio Lamu, imeibua ghadhabu kutoka kwa Waislamu katika kisiwa hicho.

Viongozi wa kidini, wazee wa Kiislamu, waumini na wasimamizi wa msikiti huo mkongwe wanamtaka mwanamitindo wa mavazi, Zeddie Lukoye – anayedaiwa ndiye alibuni tishati zilizo na picha ya msikiti huo – kujitokeza na kuwaomba radhi kwani matumizi yake yanakiuka maadili ya kidini.

Kulingana nao, fulana hiyo yenye nembo ya msikiti wa Riyadha imeanza kuvaliwa kwenye mazingira yasiyostahili kidini, na hivyo kukosea heshima Waislamu.

Kupitia taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Kituo cha Kidini cha Riyadha, Bw Abubakar Badawy, usimamizi wa msikiti ulisema licha ya kwamba wazo la kubuni tishati hizo lingesaidia kutangaza Lamu – kwa vile msikiti huo ni makavazi ya kihistoria – itakuwa vigumu kuzuia watu wasivae katika maeneo yanayokosea dini heshima.

“Hatujaridhishwa na uchapishaji wa fulana yenye nembo ya msikiti wetu. Ikizingatiwa kuwa Riyadha ni msikiti na kituo cha kidini, si vyema kwamba nembo yake itatumiwa kuendeleza mambo ambayo maadili yake si ya kidini. Isitoshe, tunahisi hatua hiyo inashusha hadhi ya kihistoria ya kituo cha Riyadha,” alihoji Bw Badawy.

Juhudi zetu kumtafuta Bw Lukoye kujibu madai hayo ziligonga mwamba.

“Wasiwasi wetu ni kwamba huenda fulana kama hiyo ikaishia kutumika kwenye vituo vya burudani na pombe. Kwa heshima, tungeomba picha ya Jay-Z iliyoko mitandaoni iondolewe.

“Mwanamitindo pia atupilie mbali matumizi ya nembo ya msikiti wa Riyadha katika kazi zake, iwapo kweli anaheshimu dini na hata mwanzilishi wa kituo hicho cha kidini cha msikiti wa Riyadha, Habib Swaleh,” akasisitiza Bw Badawy kwenye waraka wake.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Dini ya Kiislamu, Ustadh Mohamed Abdulkadir, aliunga mkono wito huo.

“Hili si kosa kwa msikiti wa Riyadha pekee bali dini nzima ya Kiislamu. Utawezaje kutumia nembo ya kidini kuendeleza mambo yasiyozingatia misingi ya dini hiyo? Akubali makosa yake, aombe msamaha na pia atoe nembo hiyo kwenye fulana na biashara zingine alizopanga. La sivyo, sisi tutaelekea kortini,” alisema Bw Abdulkadir.

Naye mzee wa Lamu, Alawy Abzein alieleza haja ya wanamitindo kutafuta ushauri kwanza kwa wananchi na wazee wa Lamu wanapokuwa na wazo la kutaka kuitangaza taswira ya Lamu ulimwenguni.

Alisema badala ya kutumia nembo ya msikiti wa Riyadha, ambayo ni ya kidini, kuna nafasi ya kutumia nembo mbadala inayowakilisha Lamu; ikiwemo nyota na mwezi, jicho la Lamu, boti, mashua na ufuo wa bahari Hindi kisiwani Lamu.

You can share this post!

Liverpool kucheza dhidi ya Real Madrid leo usiku

Jinsi tulivyopigana na simba hayawani, nusra atumalize