• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Jitihada za kundi la walemavu kushusha gharama ya malisho ya kuku  

Jitihada za kundi la walemavu kushusha gharama ya malisho ya kuku  

NA MWANGI MUIRURI
KUNDI la Walemavu 20 katika Kaunti ya Murang’a limeahidi kuzindua chakula cha kuku kitakachouzwa kwa bei nafuu kabla ya Desemba 2023.

Kundi hilo linalofahamika kama Vision Farmers Challenged People (VFCP) kutoka wadi ya Ichagaki eneobunge la Maragua, limepata ufadhili wa Sh1.8 milioni kutoka kwa Benki ya Ustawishaji Afrika (AfDB).

“Ufadhili huo unajumuisha malighafi kutengeneza chakula cha kuku, mashine za kutekeleza jukumu hilo na utaalamu wa kuchanganya malighafi hayo,” akasema mwenyekiti wao Bi Damaris Muthoni.

Muthoni alisema kwamba kilichobakia sasa ni kupata uwanja wa kuweka mitambo hiyo na kazi kung’oa nanga.

“Tunashirikiana na viongozi wetu wakiwemo, mbunge wa Maragua Mary wa Maua na diwani (MCA) wa Ichagaki Bw Hilary Muigai ili watutengee nafasi katika shamba la serikali,” akasema.

Mwenyekiti wa Vision Farmers Challenged People (VFCP) Bi Damaris Muthoni wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali. Picha|MWANGI MUIRURI

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini, Bw Gitonga Murungi alisema kwamba ameagiza Mkuu wa Tarafa ya Maragua, Bw Joshua Okello kuhakikishia usalama wa malighafi hayo na pia mtambo.

“Tunaelewa changamoto za kundi hili na katika juhudi zake za kujiimarisha, nitahakikisha kwamba tumelihami na uwezo wote wa kiserikali ili liafikie malengo yake. Kama serikali, tumeona uwezekano wa kuimarika kwa uchumi mashinani kupitia harakati za kundi hili na mchango wao katika ufugaji utasaidia kushuka kwa bei ya uzalishaji na pia nafasi za kazi,” akasema.

Bw Okello alithibitisha kupata mwelekeo wa Bw Murungi, akisema, “Kwa sasa tuko katika harakati za kupata uwanja wa serikali ili mradi huu ung’oe nanga. Serikali iko tayari kushirikiana na yeyote mwenye nia njema kuimarisha ustawi wa taifa”.

Bi Muthoni alisema kwamba “tukijaliwa fanaka katika maono yetu, tutashukisha bei ya chakula cha kuku kwa asilimia 25 na tukiendelea kupata ufadhili zaidi, tutaipunguza hata kwa asilimia 50”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Afisa wa polisi alazimika kutumia mitandao kuomba mke arejee

Gaucho aonywa kuhusu ‘ulimi wake hatari’

T L