• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Afisa wa polisi alazimika kutumia mitandao kuomba mke arejee

Afisa wa polisi alazimika kutumia mitandao kuomba mke arejee

NA SAMMY WAWERU

AFISA wa polisi anauguza majeraha ya moyo kutokana na kile kinaonekana kana kwamba ametemwa na mkewe. 

Akiashiria kulemewa na machungu ya kuachwa, askari huyo amelazimika kumrai mkewe kupitia mitandao ya kijamii.

Afisa huyo anayejitambua kama Kelvin Muguku, amechapisha katika akaunti yake ya Facebook msamaha akililia kipenzi chake cha moyo kurejea nyumbani.

Chapisho hilo linasema, “Rejesha fahamu zako tujenge boma letu, kesho yetu lazima iwe bora. Mwanadamu hukosea, na ninajua nilikukosea tafadhali nisamehe, wewe ni furaha yangu.”

Kwa mujibu wa maelezo hayo yaliyoandamana na picha ya mkewe mrembo, yanaashiria Muguku huenda alifanya kosa lililomghadhabisha.

Afisa huyo hata hivyo hakufichua kosa alilofanyia mkewe.

“Tafadhali tumetoka mbali,” akatamatisha msamaha wake, ulioandamana na alama ya upendo.

Machapisho yake ya hapo awali, Muguku amepakia picha akiwa na mke wake, na watoto wawili.

Aidha, picha zingine anaonekana akiwa amevalia sare rasmi za polisi.

Kelvin Muguku. PICHA|HISANI

Machapisho hayo yanaashiria afisa anayependa na kuthamini mke na wanawe.

Baadhi ya watumizi wa Facebook wamevamia chapisho la Muguku kuomba msamaha, wakitoa hisia mseto na mawaidha.

Daniel Gachara ameandika: “Kuchapisha katika ukurasa huu inaonyesha unyenyekevu wako. Ninamhimiza (akimaanisha mkewe) awe na ujasiri moyoni kusamehe na kurejea, muwaze pamoja. Kuwa na familia ni jambo maridadi.”

“Mpe muda…Muda ndio kila kitu na ujishughulishe na mambo unayopenda na usikome kuomba Mungu, afanye kulingana na mapenzi yake na ukubali matokeo,” Mercy Wangui Wanjira akashauri.

Naye Samwel Kiprotich amechangia akisema “Ni jambo la muda tu na atakosa uwepo wako arudi. Nina uhakika pia atanyenyekea. Kuwa na subira”.

Baadhi hata hivyo wamemsuta, wakidai huenda alidanganya – Kuenda nje ya ndoa.

“Ndugu…Haya ni masuala ya kibinafsi. Haifai kuyaanika sana kwa watu kupitia mitandao ya kijamii, usidhani kila mtu ni rafiki ndugu, wengine wanacheka tu wakiona unavyoporomoka,” Joseph Mwaniki amemkosoa.

Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa polisi wameonekana kukumbwa na changamoto za kikazi, kifamilia na hata kimaisha, baadhi wakiishia kumiminia wapenzi wao au hata wafanyakazi wenza risasi.

Kitengo cha Idara ya Polisi (NPS) kinachoangazia masuala ya askari, hasa kutoa ushauri nasaha kinaonekana kuzembea wengi wakilemewa na msongo wa mawazo kufuatia hali ngumu ya maisha.

  • Tags

You can share this post!

Huddah Monroe: Ndoa si ndoto yangu, kwa nini nijipe...

Jitihada za kundi la walemavu kushusha gharama ya malisho...

T L