• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:50 AM
Johana Chacha: Mwanahabari wa zamani akiri kuwa mateka wa pombe, akitumai mradi wa Pasta Dorcas Gachagua utamuokoa

Johana Chacha: Mwanahabari wa zamani akiri kuwa mateka wa pombe, akitumai mradi wa Pasta Dorcas Gachagua utamuokoa

NA FRIDAH OKACHI

MWANAHABARI wa zamani wa kituo cha KTN na K24, Johana Chacha ni miongoni mwa walionufaika kupitia mpango wa kurekebisha tabia ulioazishwa na mke wa Naibu wa Rais, Pasta Dorcas Gachagua.

Chacha alikiri kulemewa na kero ya unywaji pombe kupindukia, mpango wa mke wa Bw Rigathi Gachagua kuangazia pombe, dawa za kulevya na mihadarati ukimletea afueni.

Kupitia video iliyochapishwa na Pasta Dorcas, kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, Bw Chacha alisema alitumia pombe kwa muda mrefu na kumkatizia hamu ya uanahabari baada ya kuwa mraibu wa pombe kazini.

Chacha alipokea barua ya kuachishwa kazi baada ya kususia kufika kazini kwa siku tatu mfululizo bila kupeana sababu yoyote.

“Nilianza uanahabari 2013. Nilifanya kazi na kituo cha KTN kisha nikaelekea kituo cha K24 na kupandishwa cheo hadi kuwa ripota mkuu, halafu nikawa mhariri katika kitengo cha siasa. Hapa ndipo nilipoteza mwelekeo, nikajiingiza kwenye uraibu wa pombe na kususia kufika kazini. Siku ya nne nilirudi kazini, nikaulizwa maswali ambayo sikuwa na majibu na kuihsia kupoteza kazi,” alisimulia mwanahabari huyo.

“Katika siku hizo tatu, wahariri na wenzangu walijaribu kunitafuta kadri wawezavyo akini hawakunipata,” aliendelea kueleza.

Baada ya kazi kuisha 2016, mwanahabari huyo alizidi kunywa pombe kupita kiasi.

Miaka saba akiwa mateka wa pombe, aliamua kutuma ombi na kujiunga na mpango wa kupata mafunzo jinsi ya kuasi uraibu wa vileo.

“Niliposikia Pasta Dorcas Gachagua ameanzisha mradi wa kusaidia vijana kurekebisha tabia na kukabiliana na unywaji pombe na mihadarati, nilitamani sana kujiunga nao. Nilijiandikisha. Wataalamu walitupa mafunzo na ushauri jinsi ya kujiondoa kwenye minyororo ya pombe. Nilikamilisha mafunzo hayo Septemba 2023, na ninasubiri kuhitimu Novemba 2023.

“Changamoto imekuwa kuacha. Nimefahamu jambo la kwanza ni kufanya uamuzi kutoka rohoni. Tangu nitoke kule, nimejiunga na kanisa. Washirika wananifuatilia kila mara na kutoa msaada wa kifedha na chakula,” alisema Bw Chacha.

Agosti 2023, Bi Gachagua alizindua kambi ya wanaume ya ustawi na urekebishaji tabia katika Uwanja wa Maonyesho wa Jamhuri, Jijini Nairobi.

Hii ni baada ya waraibu wa dawa za kulevya na vileo kujitolea kurekebisha tabia baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Alitoa wito kwa jamii kuwakumbatia waraibu hao na kuwachukulia kama sehemu ya jamii kubwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Nyamira sasa yajisimamia kusambaza huduma za maji

Vuguvugu la Bunge la Mwananchi lataka leseni ya kampuni ya...

T L