• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
JUNGU KUU: Raila katika hatari ya kupoteza usemi Nyanza

JUNGU KUU: Raila katika hatari ya kupoteza usemi Nyanza

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na hatari ya kupoteza viti vya ugavana katika ngome yake ya Nyanza kutokana na kero iliyoibuliwa na hatua ya chama hicho kutoa tiketi za moja kwa moja kwa baadhi ya wagombeaji.

Hii ni baada ya wandani wa mwanasiasa huyo, ambao hawakuridhika na mtindo huo wa uteuzi wa wagombea nyadhifa hizo katika kaunti za Homa Bay, Migori, Siaya, Kisumu, Kisii na Nyamira, kukataa kuwaunga mkono wagombeaji wa ODM.

Chama cha ODM kilisema kiliamua kutoa tiketi za moja kwa moja kwa wagombeaji ugavana katika kaunti hizi, badala ya kutoa nafasi kwa wanachama kushiriki kura za mchujo baada ya kushawishika na matokeo ya kura za maoni yaliyoonyesha wagombea fulani kuwa maarufu zaidi kuliko wenzao.

Katika kaunti ya Homa Bay, tiketi ilimwendea Mwakilishi wa Kike wa kaunti hiyo Gladys Wanga, Seneta Ochilo Ayacko akatunukiwa tiketi ya Migori huku mwenzake wa Siaya, James Orengo akituzwa tiketi, bila jasho, kuwania ugavana.

Katika kaunti ya Kisumu, gavana wa sasa Peter Anyang’ Nyong’o ndiye atapeperusha bendera ya ODM kutetea kiti, Mbunge wa Dagorett Kaskazini Simba Arati akapewa tiketi ya Kisii huku ile ya Nyamira ikimwendea aliyekuwa mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya ODM Catherine Mumma alisema chama hicho kilitoa tiketi za moja kwa moja kwa wagombeaji hao baada ya matokeo ya kura ya maoni kuonyesha kuwa wao ndio waliokuwa maarufu.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi ambaye alisema kuwa hakukuwa na mantiki yoyote kwa ODM kutumia rasilimali nyingi kuendesha kura za mchujo kuwania tiketi za ugavana katika kaunti hizo baada ya matokeo ya kura za maoni kubaini washindi.

“Isitoshe, mbinu ya utoaji tiketi za moja kwa moja ni mojawapo ya zile zinazokubalika kulingana na kanuni za uteuzi wa ODM,” mbunge huyo wa Suba Kusini akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge mnamo Aprili 19.

Isitoshe, akiongea katika mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Qatar, Paddy Ahenda, mnamo Aprili 20, Bw Odinga alitoa wito kwa wafuasi wake katika ngome yake ya Nyanza kuwapigia kura wawaniaji wa ODM kutoka viti vya udiwani hadi urais, mtindo unaojulikana katika kimombo kama “six piece”.

“Huku nikiwa nimejitolea kupambana katika ngazi ya kitaifa, nawaomba kupigia kura wawaniaji wa ODM pekee kutoka viti vya udiwani hadi urais katika uchaguzi mkuu ujao. Hii ndiyo itatuwezesha kuwa na nguvu hitajika,” akawaambia waombolezaji nyumbani kwake marehemu Ahenda katika kijiji cha Kosewe, eneobunge la Kabondo Kasipul, Homa Bay.

Bw Odinga pia aliwashauri wale waliokosa tiketi za ODM kuwaunga mkono wenzao waliozipata akiahidi kuhakikisha kuwa wameteuliwa katika nyadhifa nyingine serikalini endapo muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya utashinda urais.

Lakini duru ziliambia ‘Taifa Jumapili‘ kwamba wawaniaji wa ugavana waliohisi kwamba ODM haiwatendei haki kwa kutoa tiketi za moja kwa moja kwa wapinzani wameamua kukaidi wito huo wa Bw Odinga.

Umaarufu wa wagombeaji hao umeimarika kwa kiwango kikubwa zaidi katika siku chache zilizopita, hali ambayo imesababisha wasiwasi miongoni mwa wakuu wa ODM.

Kwa mfano, katika kaunti ya Homa Bay duru zasema kuwa mambo yameanza kumwendea mrama Bi Wanga, huku aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero akivuna uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa wawaniaji waliolazimishwa kujiondoa.

Inasemekana kuwa wafuasi wa aliyekuwa Mbunge wa Kasipul Oyugi Magwanga na Bw Mbadi waliojiondoa kinyang’anyironi wameamua kumuunga mkono Dkt Kidero ambaye ameamua kuwania kiti hicho kama mgombeaji wa kujitegemea.

Bw Magwanga, ambaye aliwania ugavana wa Homa Bay katika uchaguzi mkuu wa 2017, alikubali kuwa mgombea mwenza wa Bi Wanga, baada ya wawili hao kupatanishwa na Bw Odinga mwenyewe katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

“Hali hii imefanya kambi ya Bi Wanga kuingiwa na wasiwasi mkubwa zaidi kiasi kwamba siku hizi ni nadra kwake kuandaa mikutano mikubwa ya hadhara kujipigia debe. Ukweli ni kwamba wagombeaji viti vingine ambao wamegura ODM na kuamua kuwa wagombeaji wa kujitegemea wanamuunga mkono Dkt Kidero,” anasema mbunge mmoja kutoka Homa Bay ambaye aliomba tusimtaje jina.

Mchanganuzi wa siasa za Nyanza David Owidi anasema sababu kuu wimbi la siasa unavuma kinyume na matarajio ya ODM katika kaunti za Nyanza ni hatua ya chama hicho kutoa tiketi ya moja kwa moja kwa wagombeaji ugavana.

“Sababu nyingine wito kwamba raia wakumbatie mtindo wa upigaji kura wa “six piece” kwani wakazi wengi wanafasiri mfumo huo kuwa sawa na wao kulazimishiwa viongozi,” anaongeza Dkt Owidi’ ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Katika kaunti ya Migori, Gavana wa sasa Okoth Obado, ambaye ni hasidi wa kisiasa wa Bw Odinga, amemuunga mkono waziri wa zamani Dalmas Otieno ili amwangushe Bw Ayacko.

Bw Otieno ambaye hadi Februari 2022 alikuwa kamishna wa Tume ya Mishahara Nchini (SRC), anawania ugavana wa Migori kwa tiketi ya chama cha Peoples Democratic Party (PDP) kinachoongozwa na Bw Obado.

Bw Ayacko pia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Migori (sasa Suna Mashariki) John Dache Pesa ambaye anawania kiti hicho kama mgombeaji wa kujitegemea.

Bw Pesa ni mmoja wa waliokerwa na hatua ya ODM ya kutoa tiketi ya moja kwa moja kwa Seneta Ayacko.

Katika kaunti ya Siaya, anakotoka Bw Odinga, Bw Orengo anakoseshwa usingizi na aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo.

Bw Gumbo ambaye anashirikiana na aliyekuwa Msemaji wa Polisi Charles Owino kama mgombea mwenza wake, anawania kwa tiketi ya chama cha United Democratic Movement (UDM).

Kwa upande wake, Profesa Nyong’o anakabiliwa na kibarua kikubwa kuhifadhi kiti hicho kutoka na upinzani mkali mtangulizi wake Jack Ranguma anayewania kwa tiketi ya chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG).

Chama hiki kinaongozwa na Mbunge wa Ugenya David Ochieng’ na ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio.

Kulingana na Dkt Owidi Bw Odinga anafaa kuwaweka huru wafuasi wake wawachague viongozi wanaowataka mradi wanaunga mkono azma yake ya urais.

“Hii ndio njia ya kipekee itakayoondoa taswira kwamba wapigaji kutoka ngome yake wameamkaidi, endapo wataamua kuwachagua wawaniaji wa vyama vingine kando na ODM,” anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Ulikosea stepu, Ruto amwambia Uhuru

Mchuuzi kutoka Sudan Kusini ashtakiwa wizi wa simu ya...

T L