• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kamwe huwezi kufanikiwa maishani ukiwa mtu aliye mwepesi wa kukata tamaa

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kamwe huwezi kufanikiwa maishani ukiwa mtu aliye mwepesi wa kukata tamaa

NA WALLAH BIN WALLAH

TUNAJUA kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani.

Lakini usikubali kushindwa haraka haraka tu ati kwa sababu kushindwa kupo! Hapana! Kataa! Usiwe mwepesi wa kukata tamaa unapofanya shughuli yoyote ya kutafuta mafanikio katika maisha yako!

Lazima uwe na msimamo thabiti wa kuwania ushindi ndipo ufaulu na ufanikiwe maishani. Kila wakati unapohisi kwamba moyo wako unakabiliwa na chembechembe za kulemewa ama kushindwa, jihimu uweke akili zako, ubongo wako na mawazo yako yote katika mizani ya kujitahidi mpaka ufanikiwe!

Kushindwa upesi upesi ni ishara kwamba umekubali au umeamua mwenyewe kushindwa.

Usiridhike wala usikubali asilani kuyatelekeza malengo yako badala ya kuyatekeleza!

Usighairi kutimiza ndoto yako. Azma yako ndiyo maisha yako na mustakabali wako!

Watu wote waliofanikiwa maishani hawakukata tamaa kamwe!

Wamisri walijikusuru kujenga haram au piramidi za kutisha ulimwenguni bila kutumia saruji wala zege! Na bado zipo zinavutia hadi leo!

Thomas Edison alijitahidi mara mia tisa akijaribu kuvumbua kutengeneza balbu ya umeme mpaka akafaulu ndipo leo tunabofya tu swichi kupata mwangaza wa umeme majumbani!

Huwaje wengine wetu tunashindwa kuvumilia kujifunza japo vitu vidogo tu kama vile ngeli za Kiswahili ili tuzungumze na kuandika Kiswahili fasaha kila siku?

Ndugu wapenzi siri ya mafanikio ni bidii na moyo wa kutokata tamaa! Ukishindwa leo, jaribu tena na tena! Ipo siku utafanikiwa vizuri sana.

  • Tags

You can share this post!

Kocha apongeza usimamizi wa Kenya Pipeline kwa kufanikisha...

NDIVYO SIVYO: Neno ‘mgombea-mwenza’ na mitego yake...

T L