• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KIGODA CHA PWANI: MCAs wawe huru kuwahoji mawaziri wateule wa Nassir

KIGODA CHA PWANI: MCAs wawe huru kuwahoji mawaziri wateule wa Nassir

NA PHILIP MUYANGA

BAADA ya Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir kuteua baraza lake la mawaziri mwezi uliopita kumekuwa na mjadala kuhusiana na uteuzi huo hususan iwapo kila sehemu ya kaunti imewakilishwa katika baraza hilo.

Suala hilo limechukuwa mkondo wa kisiasa kwani baadhi ya wanasiasa wanataka wawakilishi wadi kutupilia mbali orodha ya majina ya walioteuliwa iwapo maeneo bunge yao hayajapata wawakilishi katika baraza hilo la mawaziri wa kaunti.

Kwa sasa wananchi wanijiuliza iwapo bunge la kaunti kupitia wawakilishi wadi (MCA’s) litawahoji mawaziri hao wateule kwa njia ya haki na kutekeleza jukumu lao kulingana na katiba au watafuata maslahi ya wanasiasa na wahusika wengine wanaotaka baadhi ya watu wao wateuliwe.

Hili ni swali nzito ambalo wawakilishi wadi wa kaunti ya Mombasa wanafaa kujiuliza kwani hawafai kufuata tu upepo wa kisiasa na kuwapitisha au kuwaondoa mawaziri wateule bila sababu mwafaka.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa iwapo waziri yeyote mteule hatapita mahojiano hayo ya bunge la kaunti,basi ni sharti sababu zitolewe na kuwekwa hadharani ili wananchi wajue.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, MCA’s wanafaa kujua kuwa jukumu lao ni kuangalia uwezo wa kila waziri mteule na kumhoji ipasavyo iwapo wanaweza kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa katika wizara mbalimbali.

Wachanganuzi hao wanasema kuwa kuwahoji mawaziri ni jukumu MCA’s wamepewa na katiba na kwamba wanafaa kuwa huru kabisa wakati wanapolitekeleza bila kuegemea upande wowote.

KOSOA

Hivi majuzi,aliyekuwa mbunge wa Kisauni Bw Ali Mbogo alionekana kukosoa uteuzi wa baraza la mawaziri akisema kuwa haukuonyesha sura ya Mombasa.

Bw Mbogo alisema kuwa licha ya eneo bunge la Kisauni kumpigia kura Bw Nassir kwa wingi,eneo hilo halina waziri hata mmoja aliyeteuliwa katika baraza la mawaziri.

Aliongeza kusema kuwa viongozi wa eneo bunge hilo ni sharti wasimame kidete na kutetea wananchi wa eneo hilo.

“Lazima tupiganie haki yetu, hatuwezi kuwa tumeweka nguvu zetu mahali lakini leo hatutambuliki, viongozi wetu lazima wapiganie na kuhakikisha hiyo orodha (ya mawaziri wateule) imebadilishwa na tupate viongozi kutoka Kisauni,” alisema Bw Mbogo.

Aliongeza kusema kuwa eneo bunge la Kisauni liko na wasomi na haoni kwanini wasipate kiongozi katika baraza la mawaziri wa kaunti.

“Anasema (Bw Nassir) kuwa anataka kuona sura ya Kenya katika serikali yake,kabla afikirie sura ya Kenya, kwanza angeanza na sura ya maeneo sita ya Mombasa kuhakikisha kuwa kila eneo bunge Mombasa liko na uwakilishi katika baraza lake la mawaziri,” alisema Bw Mbogo.

Wakili Shukran Mwabonje ambaye ni mchanganuzi wa siasa alisema kuwa kipengele 197 cha katiba kinaipa mamlaka bunge la kaunti kuhakikisha kuwa utamaduni wa kila jamii umeonekana katika baraza la mawaziri.

Bw Mwaboje aliongeza kusema kuwa iwapo baadhi ya watu wanawasukuma MCA’s kufuata mkondo fulani wakati wa mahojiano ya mawaziri hao wateule,jambo hilo ni kinyume na matakwa ya wananchi na katiba na hatua mwafaka zinafaa kuchukuliwa.

KUKATAA ORODHA

“Iwapo orodha ya baraza la mawaziri haionyeshi tamaduni mbalimbali za kaunti ya Mombasa,basi MCA’s wana jukumu la kukataa orodha hiyo ndiposa gavana aweze kuteuwa baraza lingine ambalo linaonyesha uso wa Mombasa,” alisema Bw Mwabonje.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Bw Philip Mbaji, uhuru wa MCA’s katika kuwahoji walioteuliwa katika baraza la mawaziri unafaa kuwepo ili mahitaji ya wananchi yaweze kutimizwa. Alisema kuwa iwapo uteuzi wa mwaziri hao wa kaunti haufai au haukuwa unalingana na sheria,basi wawakilishi wadi wanafaa kurekebisha suala hilo.

“Wakijifurahisha kwa mawakala wa watu wanaotafuta mamlaka itakuwa sio tu kukiuka jukumu lao lakini pia kutia doa mahitaji ya wananchi na kwamba wanafaa kusimama wima katika suala hili,” alisema Bw Mbaji.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa pia wanasema kuwa MCA’s wanafaa kutekeleza jukumu lao bila msukumo wa mwanasiasa yeyote au chama cha kisiasa na kuwapatia wananchi wa kaunti ya Mombasa mawaziri bora ambao watatekeleza kazi yao bila kushurutishwa na mtu yeyote.

Wanaongeza kusema kuwa uhuru wa MCA’s kufanya mahojiano mwafaka na mawaziri walioteuliwa utaimarisha utenda kazi wa maafisa wa kaunti kwani watafahamu kuwa hakuna mwanasiasa yeyote atakayewatetea iwapo watafanya makosa.

Shughuli ya ukaguzi wa mawaziri wateule wa Bw Nassir ilipigwa jeki wiki iliyopita baada ya mahakama ya uajiri na masuala ya kazi kutupilia mbali ombi lililotaka zoezi hilo kuzuiwa kwa muda hadi kesi iliyowasilishwa kusikizwa na kuamuliwa.

Jaji wa mahakama hiyo Bi Agnes Nzei alisema kuwa kusimamisha zoezi hilo la mahojiano ya mawaziri wateule itakuwa mapema kwa mahakama kuingilia suala hilo kwa wakati huu.

Mawaziri wateule ni pamoja na Naibu Gavana Bw Francis Thoya ambaye atasimamia idara ya Mazingira na usimamizi wa taka, nafasi ambayo amekuwa akiishikilia kwa muda tangu wachaguliwe kuongoza Mombasa.

Bw Thoya amekuwa akiongoza maafisa wa kaunti katika shughuli za kusafisha mji wa Mombasa na kufunga sehemu za kutupa taka zilizoanzishwa kinyume cha sheria.

Jamaa na marafiki wafurahia uteuzi wa Emily Achieng Okello (kati),31, kama waziri mteule wa Maji na Mali Asili katika Kaunti ya Mombasa. Madiwani wa kaunti hiyo wamehimizwa kuwahoji mawaziri wateule bila kuogopa. PICHA | MAKTABA

Wengine walioteuliwa ni Emily Achieng (Maji, Mali Asili na Hali ya Hewa), Kenneth Muigai (Huduma ya Umma,Vijana,Jinsia na Michezo),Kibibi Abdallah (Uchumi Samawati,Kilimo na Ufugaji).

Bw Mohamed Osman (Utalii,Utamaduni na Biashara) Dkt Mbwarali Kame (Elimu na Masuala ya Kidijitali),Evans Oanda (Fedha na Uchumi) Dkt Swabah Ahmed (Afya) na Daniel Otieno Uchukuzi na Miundo Misingi).

  • Tags

You can share this post!

Wamiliki baa Murang’a walia kutapeliwa

WALIOBOBEA: Uhuru alipewa jina hilo na Mwai Kibaki

T L