• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:26 PM
KIGODA CHA PWANI: Raila na Ruto kutumia ardhi kama chambo cha kampeni

KIGODA CHA PWANI: Raila na Ruto kutumia ardhi kama chambo cha kampeni

TAKRIBAN chini ya siku sabini kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 kivumbi cha kampeni za kisiasa katika ukanda wa Pwani kinatarajiwa kuonekana baada ya wagombea wakuu wawili wa urais Dkt William Ruto na Bw Raila Odinga kutaja vikosi vitakavyoendeleza kampeni zao ukanda huo.

Ukanda wa Pwani huwa ni mojawapo ya maeneo yanayoshuhudia kampeni zilizoko na joto jingi la kisiasa ikitiliwa maani wawaniaji wengi hususan wale wa urais hutumia swala la ardhi,ambalo huzua hisia kali miongoni mwa wananchi, kujipigia debe.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, waliotajwa katika vikosi vya kampeni za viongozi hao wa muungano wa Kenya Kwanza na ule wa Azimio ni ishara tosha ya kuwa kwa sasa ndio mkoko umealika maua.

Kikosi cha Bw Ruto kinaongozwa na magavana Salim Mvurya na Amason Kingi, aliyekuwa gavana wa Lamu Issa Timamy na mwakilishi wa wanawake katika bunge kutoka kaunti ya Taita Taveta Bi Lydia Haika.

Azimio

Watapambana na kikosi cha muungano wa Azimio la Umoja ambacho kinaongozwa na Gavana Hassan Ali Joho pamoja na mwenzake wa Taita Taveta Granton Samboja, mbuge wa Mvita Abdulswamd Shariff Nassir na mwenzake wa Taveta Bi Naomi Shabaan na mfanyibiashara Suleiman Shahbal.

Vikosi hivyo vya kampeni vinatarajiwa kupatia viongozi wao takriban kura 1.9 milioni kutoka kaunti zote sita za Pwani zikiwemo Taita Taveta, Kilifi, Mombasa, Tana River, Kwale na Lamu.

Maswala yanayotarajiwa kuangaziwa na viongozi hao ni lile la ardhi ambalo limechukua takriban asilimia 70 ya mikutano ya kampeni ya wanasiasa hao, swala la uchumi wa bahari na ugavi wa mamlaka ya kisiasa.

Vikosi hivyo vya miungano hiyo vilijitosa uwanjani kutafuta kura huku kile cha Kenya Kwanza kikijiunga na Dkt Ruto katika mikutano yake ya Mombasa, Kwale, Kilifi na Taita Taveta kuanza rasmi kampeni.

Katika kampeni yake ya juzi akiambatana na kikosi chake eneo la Pwani, naibu rais William Ruto alisema kuwa iwapo atachukua hatamu za uongozi wa nchi basi ataanzisha mfuko wa hazina maalum ya kutafuta pesa za kununua shamba ili kutoa kwa maskwota.Bw Ruto alimsuta mpizani wake Bw Odinga akisema kuwa hajasaidia kwa njia yeyote kutatua suala la ardhi eneo la Pwani.

“Ni nini yeye (Bw Odinga) amefanya kutatua shida hiyo? Ilikuwa wakati wake kama waziri mkuu ndiposa swala la unyakuzi wa ardhi lilikuwa kubwa,” alidai Dkt Ruto katika mojawapo ya mikutano hiyo.

Kauli hiyo ilionekana kuungwa mjono na Bw Mvurya aliyesema kuwa Bw Odinga hakuangazia swala la ardhi alipokuwa mamlakani.

Kwa upande wake, Bw Kingi alisema kuwa viongozi wengi wakubwa wa Pwani hapo awali wameshikilia wizara ya ardhi lakini hakujakuwa na manufaa yeyote.

Kikosi cha Azimio kikiongozwa na Bw Joho kilikita kambi eneo la Malindi huku kikianza kumpigia debe kinara wao Bw Odinga siku ya Alhamisi.

Bw Joho alionekana kumsuta Gavana Kingi akisema kuwa mawaziri wa ardhi kutoka eno la Pwani waliokuwa hapo awali sio kama yeye.

“Mimi siogopi mtu yeyote, namuogopa Mungu, mimi ni mtu wa ukweli nawahakikishia yale hayakufanyika miaka yote siku nikiingia kwa wizara ya ardhi yale hayakufanyika yatafanyika,” alisema Bw Joho.

Aliongeza kusema kuwa kama waziri atakuwa kwa meza ya maamuzi ya kiserikali na jambo muhimu kwake ni kuhakikisha muhula wa uongozi unaokuja swala la ardhi haliwezi kurejelewa tena.

“Ajenda ni moja kwa muhula unaokuja hatuwezi tena kurudia siasa za mashamba katika jimbo letu la Pwani,kama kuna mashamba serikali itanunua ,si wananunua kwa wengine,” alisema Bw Joho.

Katika mkutano wake wa hivi majuzi eno la Pwani, Bw Odinga aliahidi kurejesha uchumi wa Pwani kwa kuhakikisha shughuli zihusikanazo na bandari ya Mombasa remeregeshwa. ‘Tunajua Pwani inategemea Bandari ya Mombasa kuimarisha uchumi wake, ninajua vile Bandari ya Mombasa inamaanisha kwenu,hiyo itakuwa mojawapo ya ajenda yangu ya kwanza nitakapo apishwa,” alisema Bw Odinga.

Hata hivyo baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa wanasema kuwa licha ya vikosi hivyo kuwa na viongozi tajika,havitaweza kuwashawishi wapiga kura iwapo hawataeleza sera zao bila kurudia yaliyosemwa miaka iliyopita.

Suala la Ardhi

Waliongeza kusema kuwa swala la ardhi limekuwa hapo tangu miaka iliyopita na wananchi wamechoka kusikiza.

“Kwa sasa wapiga kura wanahitaji vitendo na suluhisho la mambo ya ardhi,sio tu kusema wataangazia swala hilo,” alisema mchanganuzi mmoja wa siasa aliyetaka jina lake libanwe.

Pia baadhi ya wapiga kura wanajiuliza iwapo viongozi hao wa kampeni za Dkt Ruto na Bw Odinga wataweza kufanya kampeni bila kuhusisha vinara hao siku ambazo zimesalia ama watachoka wafikapo katika mwa safari.

“Viongozi wengi walioko katika vikosi hivyo viwili hawawezi hata kuitisha mkutano na kuweza kuwashawisha wapiga kura kwani wnegine wao walipigiwa kura wakaenda na wamerudi sasa wakati wa kampeni,” alisema mama mmoja aliyejitambulisha kama Salma.

Mchanganuzi wa saisa Bw Mwakera Mndwamrombo alisema kuwa kuchaguliwa kwa viongozi hao wa kampeni za wawili hao hakutakuwa na mabadiliko makubwa isipokuwa kupigania vitu kwa watu wanaojuana kisiasa.

“Ukiviangalia vikosi vyote viwili, hakuna hata kimoja kina mwamko mpya,” alisema Bw Mndwamrobo

  • Tags

You can share this post!

Kingi ni msaliti, viongozi wadai

TAHARIRI: Tuwakatae wanasiasa wenye ndimi za chuki

T L