• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 9:39 PM
KIGODA CHA PWANI: Teuzi za Jumwa, Mvurya zaleta mkondo mpya kwa siasa za Pwani

KIGODA CHA PWANI: Teuzi za Jumwa, Mvurya zaleta mkondo mpya kwa siasa za Pwani

NA PHILIP MUYANGA

KUTEULIWA kwa Bw Salim Mvurya na Bi Aisha Jumwa katika baraza la mawaziri katika serikali ya Dkt William Ruto kunamaanisha ya kuwa wawili hao watakapoidhinishwa na bunge ndio watakaopeperusha bendera ya serikali katika ukanda wa Pwani.

Kwa muda mrefu ukanda wa Pwani umekuwa na waziri mmoja pekee katika baraza la mawaziri, Bw Najib Balala, na kuteuliwa kwa wawili hao ambao pia ni wanasiasa kumezua msisimko wa jinsi siasa za ukanda wa Pwani zitakavyochukua mkondo mpya.

Licha ya kuwa Bw Balala, ambaye pia alikuwa mwanasiasa, alikuwa katika baraza la mawaziri linaloondoka, hakuonekana kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa na siasa za ukanda wa pwani.

Swali wananchi wengi wa ukanda wa Pwani wanajiuliza ni iwapo kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa ni kwa sababu ya kuwa walimuunga mkono Dkt Ruto katika azma yake ya kuwa rais licha ya kuwa maeneo mengi ya ukanda wa Pwani ni ngome ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Na je kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa, waliokuwa gavana wa Kwale na mbuge wa Malindi matawalia,kwa baraza hilo la mawaziri kutawaweka katika nafasi ya juu ya ushawishi wa kisiasa katika siasa za ukanda wa Pwani?

Maswali

Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo yamo vinywani mwa wakaazi wengi wa kaunti sita za Pwani ikitiliwa maanani ya kuwa hakuna kinara au kiongozi anayesemekana kuwa na ushawishi wa kisiasa wakati huu kama ilivyokuwa nyakati za marehemu Shariff Nassir na marehemu Karisa Maitha ambao walikuwa vigogo wa siasa za Pwani.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa katika baraza la mawaziri kunatokana na kumuunga mkono kwa dhati Dkt Ruto katika azma yake ya kuwa rais wa tano nchni.

Wanaongeza kusema kuwa ingawa viongozi hao hawatajihusisha na siasa moja kwa moja kutokana na majukumu yao ya uwaziri, kuteuliwa kwao kumewapa ushawishi mkubwa katika siasa za ukanda wa Pwani kwa kuwa wanatarajiwa kuwa ‘macho na masikio ya serikali’ pwani nzima kwa jumla.

Hata hivyo baadhi ya wakaazi wa Pwani wanasema kuwa chama cha ODM bado kina umaarufu mkubwa ukanda wa Pwani na itabidi Bw Muvrya na Bi Jumwa kujizatiti vilivyo iwapo watakuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa eneo la Pwani.

Mchanganuzi wa siasa Dkt Daniel Mwaringa anasema kuwa Bw Mvurya na Bi Jumwa wanastahili uteuzi huo katika baraza la mawaziri kwa sababu ya mchango wao mkubwa katika kampeni za United Democratic Alliance (UDA) na muungano wa Kenya Kwanza.

Dkt Mwaringa ambaye ni mhadhiri wa masuala ya mawasialiano katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM) alisema kuwa uongozi wa Bi Jumwa katika siasa za Pwani zinahusishwa na chama cha UDA ndiposa anastahili kutunukiwa kiti hicho cha uwaziri.

Kulingana na Dkt Mwaringa, katika ukanda wa Pwani chama cha UDA kinahusishwa sana na Bi Jumwa kama kiongozi aliyeweza kukipigia debe.

“Hata Bw Mvurya kama mshirikishi wa kampeni za Kenya Kwanza alifanya kazi kubwa katika kampeni za kuhakikisha UDA imepata kura nyingi katika ukanda wa Pwani,” alisema Dkt Mwaringa.

Kulingana na Dkt Mwaringa, uteuzi wa Bi Jumwa pia una umuhimu mkubwa sana kwa kina mama wa jamii ya Wamijikenda na ukanda wa Pwani kwa jumla kwani safari yake ya kisiasa ilianza akiwa diwani.

Mshauri wa masula ya siasa Bw Bozo Jenje anasema kuwa jitihada za Bw Mvurya na Bi Jumwa kumpigia debe Dkt Ruto na uaminifu wao umechangia pakuwa kuteuliwa kwao katika baraza la mawaziri.

“Bw Mvurya na Bi Jumwa walikuwa kati ya viongozi waliojitolea mhanga kwa kumpigia debe Dkt Ruto,” alisema Bw Jenje na kuongeza kwamba kwa kazi hiyo wawili hao wanastahili uteuzi huo katika baraza la mawaziri.

Mchanganuzi mwingine wa masuala ya kisiasa Bi Maimuna Mwidau alikubaliana na kauli ya kuwa Bw Mvurya na Bi Jumwa waliteuliwa kutokana na mchango wao mkubwa kwa muungano wa Kenya Kwanza.

“Bw Mvurya aliweza kuleta gavana (Bi Fatuma Achani) kwa kura nyingi huko kaunti ya Kwale na pia amekuwa mfuasi wa rais Ruto kwa muda mrefu sana,” alisema Bi Mwidau.

Kupigia debe UDA

Bi Mwidau aliongeza kusema kuwa pia Bi Jumwa amekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe chama cha UDA kote nchini na katika kaunti yake ya Kilifi.

Hata hivyo, Bi Mwidau alisema kuwa uteuzi wa wawili hao hautaleta ushawishi wowote wa kisiasa zaidi na kaunti zao za Kwale na Kilifi.Alisema kuwa katika kaunti ya Kilifi UDA ilipata mbuge mmoja japo Bi Jumwa alijitahidi kuhamasisha wapiga kura wengi ingawa hakufua dafu.

“Ikizidi chama cha Pamoja African Alliance (PAA) ni kichanga sana na kiliweza kupata wabunge wawili na wawakilishi wadi kadhaa, katika kaunti ya Kwale Bw Mvurya alijaribu kwani walimchagua gavana ambaye ni mwandani wake wa kisiasa,” alisema Bi Mwidau.

Bi Mwidau alisema kuwa Bw Mvurya na Bi Mwidau hawataleta mabadiliko makubwa kisiasa Pwani.

“Ukanda wa Pwani hadi sasa umeshindwa kutoa kinara ambaye anashawishi (wa kisiasa) wa huu mwambao mzima,” alisema Bi Mwidau.

  • Tags

You can share this post!

SOKOMOKO WIKI HII: Sabina akaangwa na Wakenya kwa kuhoji...

MIKIMBIO YA SIASA: Raila amempisha Kalonzo kuongoza Azimio...

T L