• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Kiini halisi cha wawaniaji kurukaruka

Kiini halisi cha wawaniaji kurukaruka

NA CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa hofu ya kushindwa katika kura za mchujo na mabadiliko kwenye ulingo wa siasa maeneo mbalimbali nchini ndizo sababu zinazochangia wanasiasa kuhama vyama vya kisiasa.

Sababu nyingine ni kukaribia kukamilika kwa muda ambao Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alitoa kwa vyama kuwasilisha orodha ya majina ya wanachama wao kwa afisi yake ili zik – aguliwe.

Ndani ya muda wa juma moja lililopita, chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto, kimepata pigo kubwa, hususan, katika eneo la Gusii baada ya viongozi wake kuhamia vyama vingine.

Mnamo Jumanne wiki hii, aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Kusini Omingo Magara alijiondoa kama Mwekahazina wa Kitaifa akidai “hamna demokrasia” katika chama hicho.

Bw Magara ambaye ametangaza azma ya kuwania kiti cha ugavana wa Kisii aliamua kujiunga na chama tawala cha Jubilee ambacho ni mshirika mkuu katika vuguvugu la Azimio la Umoja.

“Nilikuwa na ndoto na hamu ya kuwania Ugavana wa Kisii kwa tiketi ya UDA ambayo pia nimetumikia kama Mweka Hazina ya kitaifa. Lakini utovu wa demokrasia katika chama hicho umenisukumu kuamua kuondoka ili nijaribu kufanikisha ndoto yangu ndani ya chama kingine,” akawaambia wanahabari mjini Kisii.

Siku moja baadaye katibu mpanga ratiba wa chama hicho Wanjala Iyaya naye alijiondoa na kujiunga na chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kinachoongozwa na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba Bw Iyaya anakimezea mate kiti cha ubunge cha Webuye Mashariki kinachoshikiliwa wakati huu na Bw Dan Wanyama.

Mnamo Februari 19 mwaka huu aliyekuwa kiongozi wa vijana katika UDA tawi la Kisii Antony Kibagendi alihama na kujiunga na chama cha ODM baada ya kujibizana vikali na Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro.

“Tulitofautiana na Bw Osoro kuhusu maandalizi ya kura ya mchujo ya chama cha UDA itakayotumiwa kuwateua wagombeaji wake katika uchaguzi mkuu ujao. Nilibaini kuwa kuna njama ya kuwapendelea baadhi ya wawaniaji kutokana na sababu ambazo hazieleweki,” Bw Kibagendi akaambia safu hii.

Mwanasiasa huyo sasa ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Kitutu Chache Kusini kinachoshikiliwa sasa na Bw Richard Onyonka. Mbunge huyo , ambaye amehudumu kwa mihula mitatu, amejitosa kinyang’anyiro cha useneta wa Kisii kwa tiketi ya ODM.

Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi anasema Bw Magara na wenzake waliogura UDA walichukua hatua hiyo baada ya kukosa tiketi ya moja kwa moja.

“Dai la Bw Magara kwamba UDA haina demokrasia halina msingi wowote. Aliogopa kupambana na wawaniaji wengine katika mchujo na ndio maana ametoroka. Naibu Rais amekariri kila mara kwamba hakuna mwaniaji atapendelewa katika shughuli hiyo muhimu,” akasema.

Kauli ya Bw Sudi inaungwa na Mbunge wa Kitutu Masaba Ezekiel Machugo aliyesema, “watu walitaka kutumia UDA kuendeleza matakwa yao ya kibinafsi.”

  • Tags

You can share this post!

Amerika, NATO hawatamuweza Putin kwa sasa

Corona: Gavana ashauri wakazi wapokee chanjo

T L