• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KIKOLEZO: Hii ‘Real Housewives of Nairobi’ itaweza?

KIKOLEZO: Hii ‘Real Housewives of Nairobi’ itaweza?

NA SINDA MATIKO

NAFIKIRI taarifa tayari unazo na hata kama wewe ni mgeni mjini, lazima utakuwa umesikia kwamba mjini kama miji mingine yote mikubwa duniani, imepata shoo yake bab’kubwa The Real Housewives of Nairobi (RHON).

Tayari Wakenya wameshaanza kuponda wahusika mle kabla hata shoo haijaanza kupeperushwa rasmi na Showmax hadi baada ya wiki mbili kutoka leo.

Wakenya wengi walihisi shoo ilistahili kuwa na wahusika wanaonuka pesa kikweli, sio wanaofeki maisha na waliofeli kama ilivyo shoo zingine za Real Housewives.

Naelewa sana kwa nini mitazamo ipo vile ila nitakuambia kitu kheri nusu shari kuliko shari kamili.

Unajua ni kwa nini. Mchakato wa kuwa na RHON ulianza 2019 ila ukagonga ukuta. Real Housewives ni haki miliki ya Universal. 2019 ilimpa produza Claire Ash Meadow, kandarasi ya kuandaa shoo hiyo.

Ash kupitia kampuni yake Heels Production akaanza na manjonjo kibao akiahidi kitu kikubwa lakini ukosefu wa fedha na wahusika ukamtupa nje. Mwaka jana 2022 majukumu yakaiangukia Showmax ambayo ilimtumia produza mwingine na imefanikiwa kutupa shoo na wahusika hawa. Hebu tuwachambue:

VERA SIDIKA

Ingawaje produza Eugene Mbugua anamtaja kuwa mjasiriamali, na mtu mashuhuri, kila mtu anajua maelezo hayo yote sio kweli.

Sidika ni soshiolaiti aliyejipatia umaarufu kwa kuanika picha na video zake za nusu utupu.

Vera Sidika, mmoja wa washiriki wa Real Housewives of Nairobi. PICHA | HISANI

Biashara alijaribu mara mbili na zote zikafeli. Unaikumbuka ile Veetox aliyosema ni majani chai ya kupunguza tumbo na vitambi. Biashara ilifeli.

Akafungua saluni ya kifahari mitaa ya Westlands lakini bado ikafeli. Aliifunga na kuhamishia Mombasa. Haijulikani kama bado ipo.

Pamoja na dukuduku zote, nahisi kikubwa kutoka kwa Vera kwenye shoo ni kuipamba tu. Ila kama ana hela za kutisha, hilo ni la kujadili.

SUSAN KAITTANY

Ni mrembo ambaye produza amemtaja kuwa mjasiriamali shupavu anayemiliki saluni ya kisasa Posh Palace Hair Studio na pia duka la manukato.

Susan Kaittany, mmoja wa washiriki wa Real Housewives of Nairobi (RHON). PICHA | HISANI

Ila wapo wenye duku duku zao kama Mike Makori ambaye alimchamba kwa kusema ameshangaa vipi alipata shavu kwenye shoo ya kibabe kama hiyo wakati aliwahi kushindwa kumlipa kwa kazi aliyomfanyia.

“2018 alinipa kazi kama MC kwenye mojawepo ya shughuli zake halafu kwenye malipo akanizungusha weeh. Nilimwanika sana mitandaoni kiasi kuwa mamake alinifuata na kunilipa stahili yangu. Leo hii yupo kwenye RHON. Nairobi kweli mji wa ajabu sana.”

Kaitanny amewahi pia kutrendi baada ya kutibuana na aliyekuwa swahiba wake wa karibu sana Betty Kyalo. Inadaiwa ugomvi wao ulitokana na mwanamume mmoja mwenye pesa ambao wote walikuwa wakimgombania.

SONAL MAHERALI

Ukiamua kumjaji kupitia maisha yake ya Instagram, unaweza kuhisi ana maisha mazuri sana kumliko Beyonce.

Mama huyu wa watoto wanne anapenda kujishaua, produza kamtaja kuwa mjasiriamali kwenye dunia ya fasheni.

Sonal Maherali, mmoja wa washiriki wa Real Housewives of Nairobi. Picha|Hisani

Safari yake alianza kama vloga 2010 na kwa sasa ana kampuni yake ya mavazi Simba Maharani. Hapendi kuficha, huwa anajishasha wazi wazi alivyo na pesa. Ila unajua wanasema debe tupu ndio hufanya nini vile…?

Tusubiri kujionea shoo itakapopeperushwa.

MINNE KARIUKI

Ni mwigizaji ambaye anatamba kwa sasa na filamu ya Single Kiasi.

Aliwahi kuwa mtangazaji wa runinga ya KBC.

Minne Kariuki, mmoja wa washiriki wa Real Housewives of Nairobi. PICHA | HISANI

Ni mke wa ndoa wa mshikaji wake wa karibu na mfanyibiashara mwenza wa Jaguar, Charles Muigai. Muigai alikutana na Minne kipindi akiwa anasimamia kazi za Jaguar.

Maisha yake utayapenda kupitia lensi za mitandaoni zinazomwonyesha mtu anayeishi maisha ya kifahari.

LISA CHRISTOFFERSEN

Ukiniuliza mimi, pengine kwa wote hao, huyu ndiye mhusika anayetosheleza shoo.

Kwa nini? Nataka kuamini kuwa dereva wa zamani wa magari ya rally sio mtu maskini. Nchi hii, madereva wengi wa safari rally wanatokea familia za kitajiri sababu kumiliki gari la mashindano huwa ni gharama kubwa. Produza anamtaja kuwa dizaina na mmiliki wa kampuni ya safari za kifahari.

Lisa Christoffersen, mmoja wa washiriki wa Real Housewives of Nairobi. PICHA | HISANI

Pia ni mwasisi wa Lifestyle Nairobi, ambao ni ukumbi wa kisanaa eneo la kifahari Gigiri. Lifestyle Nairobi inamiliki onyesho la sanaa, migahawa, Spa, maduka ya fasheni na vyakula asilia.

KWA NINI HAWA?

Mkuu wa vipindi Showmax Denise Mwende amewataja wahusika hawa kuwa wanawake wenye upekee, wenye bidii, wanaojua kuishi maisha ya kifahari.

Je, RHON itaweza?

 

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: Xenia aingizwa mradi wa Spotify

LISHE: Faida na manufaa ya mafuta ya kanola

T L