• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
KIKOLEZO: Riri, huyo Kanairo

KIKOLEZO: Riri, huyo Kanairo

NA SINDA MATIKO

UTAKUWA umeshaziskia taarifa kuwa Bad Gal Riri au ukipenda Rihanna ameamua kuingia kwenye soko la vipodozi nchini Kenya.

Kenya ni miongoni mwa mataifa nane Barani Afrika ambayo yatakuwa ya kwanza kupokea mzigo wa Fenty Beauty na Fenty Skin Care kuanzia Mei 27, 2022.

Kwa zaidi ya miaka minne sasa, Rihanna hajatoa muziki hata mmoja. Amekuwa akitumia muda huo kuikuza brandi yake ya vipodozi na mazagazaga ya urembo, Fenty Beauty.

Toka mwanzoni, alisema nia yake ya sio kutengeneza pesa lakini pia kuhakikisha kila mwanamke anaweza kurembeka.

“Lengo ni kumfaa kila aina ya mwanamke awe mweusi, hudhurungi, maji ya kunde au nini, la muhimu ni kupata kipodozi kinachoendana na ngozi yake,” alinukuliwa 2017.

Hayo yanaendelea kutimia ukizingatia kuwa Fenty kwa sasa ina zaidi ya aina 50 ya vipodozi hivyo kuiwezesha kumstiri kila mwanamke.

Ni brandi hii iliyomgeuza kuwa mwanamuziki bilionea kwa sarafu za dola za Kimarekani.

Na kwa kuwa sasa ameamua kupanua himaya yake ili aweze pia kuchuma mpunga kutoka Afrika, itakuwa poa kukuweka sawa namna ambavyo biashara hii ilivyomgeuza dola bilionea.

Agosti 2021, jarida la Forbes lilikadiria utajiri wake kuwa dola 1.7 bilioni. Utafiti wa Forbes ulibaini kuwa asilimia kubwa ilitokana na mauzo ya Fenty Beauty iliyopata makao mengine Kenya sasa.

Kampuni hii aliianzisha 2017 akimiliki asilimia 50 huku asilimia nyingine ikimilikiwa na kampuni ya Ufaransa inayojihusisha na bidhaa za kifahari, Moet Hennessy Louis Vuitton (LVMH).

Kati ya dola hizo 1.7 bilioni, unaambiwa dola 1.4 bilioni zilichangiwa na mauzo ya bidhaa za Fenty Beauty huku muziki wake ukichangia asilimia iliyosalia.

Aidha brandi yake ya fasheni Savage X Fenty pia inachangia asilimia iliyobaki. Hii ni takriban dola 270 milioni.

Takwimu hizi zitakuwa zimeongezeka kwa sasa.Alipoizindua, ndani ya mwaka huo tu, Fenty Beauty ilifanikiwa kuwa na jumla ya maduka 1,600 kwenye mataifa 17.

Ndani ya siku 40 za kwanza toka uzinduzi wake, kampuni hiyo ilitengeneza mauzo ya dola 100 milioni.

Kwa mujibu wa utafiti wa Forbes, brandi za mastaa kama Kylie Jenner, Kim Kardashian, Jessica Alba miongoni mwa wengine, hamna inayotengeneza mpunga kama inavyofanya Fenty.

Bei

Kinachoshangaza ni kuwa bidhaa za Fenty zina manunuzi makubwa mno licha ya kuwa ni za bei kubwa.

Uhusishwaji wake pamoja na ushirikiano na LVMH ndio chanzo cha kusukuma mauzo licha ya kuwa na bei ghali.Riri hajaachia wimbo toka 2016 lakini bado ana ushabiki mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye Instagram ana zaidi ya wafuasi milioni 103 huku Twitter akiwa na milioni 106.

Vita vya mashabiki kati ya Wakenya na Waganda kwenye Twitter kumhusu ni dhihirisho tosha jinsi mamilioni ya wafuasi wake hutaka kujihusisha naye. Hili limemrahisishia soko kwani si vigumu kumshawishi shabiki anayemhusudu.

Lakini kando na uhusishwaji wake, mchakato wa kuwa na aina 50 za vipodozi umevutia wateja wengi kila mmoja akiwa na uhakika wa kukipata kitu chake.

Aidha bidhaa zake hazifanyiwi majaribio kwenye wanyama kama zilivyo nyinginezo. Hili imezifanya kuenziwa na mashirika mengi yanayotetea haki ya wanyama na kuzifanya kuaminika hivyo kuvutia wateja zaidi pia.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Kwa sasa yuko freshi barida!

TAHARIRI: Ufafanuzi zaidi kuhusu Gredi ya 7 wahitajika

T L