• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
KIKOLEZO: Sema ku-beat!

KIKOLEZO: Sema ku-beat!

NA SINDA MATIKO

MACHI 2022, mwigizaji Bruce Willis alitangaza kustaafu uigizaji kutokana na maradhi ya aphasia yaliyomfanya kutoweza kuendelea.

Maradhi hayo yaliathiri ubongo wake hivyo kutatiza uwezo wake wa kuzungumza.Huwa sio jambo la kawaida au rahisi kustaafu kutoka kwenye tasnia ya burudani kama hii, ila wapo mastaa hapa nje na ndani ya Kenya waliochukua uamuzi sawa na Bruce Willis kutokana na sababu moja au nyingine. Hawa ni baadhi tu.

Kevin Samuel

Kakake mkubwa mtangazaji wa zamani wa runinga Janet Mbugua, wiki iliyopita aliiambia safu hii ameamua kustaafu uigizaji.

Nyota huyo wa Mali alikuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa filamu ya Igiza, ambapo ni mhusika mkuu, yeye pamoja na Serah Teshnah.

“Baada ya miaka yote hiyo, Igiza ndio kazi yangu ya mwisho ya uigizaji. Nimestaafu, nataka nijishughulishe na mambo mengine yanayonivutia kama vile masuala ya afya ya umma. Isitoshe, familia yangu ipo Paris, nataka niwe karibu nayo,” akasema.

Hadi anarejea kwenye Igiza, Kevin alikuwa tayari ameshapotea kwenye tasnia ya uigizaji kwa takriban miaka minne.

“Mimi kurejea sio kwamba nilikuwa narudi kuigiza. Hapana. Kazi hii niliitiwa kipindi nikiwa Kenya wakati wa lockdown. Lakini kubwa zaidi ni stori ya uhusika wangu ndio ilinivutia zaidi kujiunga nayo. Ni uhusika wa jamaa anayehangaika na uraibu wa ulevi, uraibu ambao nilipambana nao sana kuuacha. Kwa misingi hiyo, nilihisi kukubali ofa hii, ndio njia mwafaka ya mimi kustaafu. Nimemalizana na shughuli hii,” kafanua zaidi.

Eve D’Souza

Alikuwa ni mtangazaji wa redio lakini pia mwigizaji mashuhuri hasa wa vipindi vya vichekesho.

Baada ya zaidi ya miaka 10 kwenye uigizaji, akitokea kwenye kipindi kama vile Vashita, Eve aliamua kuachana na mishemishe hiyo.

Badala yake alianzisha kampuni yake ya uzalishaji filamu Moonbean Productions na kuamua kufanya kazi nyuma ya kamera.

Aidha baada ya kufunga ndoa na Simon Anderson, alihamia Dubai na mume wake wanakoishi wakiendelea na pilkapilka zao za maisha.

Kwa sasa kando na usimamizi wa kampuni yake, kafungua chaneli yake ya YouTube ambayo amekuwa akiposti sana masuala yanayohusiana na maisha yake binafsi.

Cameroon Diaz

Aliamua kustaafu uigizaji 2014 kipindi ambacho jina lake lilikuwa limeshika kasi na taaluma yake kung’aa.’Ninajua watu wengi hawataelewa uamuzi huu ila wasichokijua ni kuwa, kama mwigizaji unakuwa na majukumu mengi na magumu sana kiasi cha kukosa muda wako. Nilitathmini maisha yangu na kuona nahitaji kupumua ili pia niweze kufanya mambo ya kibinafsi,’ Cameron alifafanua chanzo chake cha kustaafu mapema.Alikiri kuwa uigizaji uliathiri mambo mengi kwenye maisha yake ikiwemo mahusiano kutokana na yeye kukosa muda.

Portia de Rossi

Staa huyu wa series ya Scandal, aliamua kustaafu akiwa na umri wa miaka 45.

Akipiga stori kwenye shoo ya Ellen DeGeneres, alifichua sababu zake.

“Nilijua katika miaka 10, 20 ijayo, taaluma yangu ya uigizaji ingeelekea wapi na kwa sababu hizo nikaamua kustaafu na kuanzisha biashara,” akasema.

Jack Gleeson

Alitokea kwenye series maarufu ya The Game of Thrones alikovalia uhusika wa King Joffrey Baratheon.

Baada ya uhusika wake kuuawa, Jack mwenye umri wa miaka 30 alitangaza kustaafu.

Alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka saba tu. Alipoulizwa sababu za kuondoka mapema, alikiri kupoteza hamu ya uigizaji.

“Nilipoanza kuigiza ilikuwa ni kwa sababu ya kutaka kuonyesha kipaji changu na kuwafurahisha watu. Ila ilipofikia suala la kipaji kuanza kunilipa, kidogo nilipoteza ile hamu ya kuigiza kwa sababu toka mwanzo hamu yangu haikuwa nipate pesa. Nilishindwa kudumisha dhamira yangu asilia hivyo nikaona bora niache kuliko kuathiri amani yangu,” akakiri.

You can share this post!

Kiungo Danny Drinkwater aomba msamaha kwa...

Kocha Gareth Southgate aita Jarrod Bowen na James Justin...

T L