• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kioni: Kenya inaongozwa na viongozi waliokataa Katiba

Kioni: Kenya inaongozwa na viongozi waliokataa Katiba

NA SAMMY WAWERU

CHAMA cha Jubilee kimeendeleza mashambulizi yake kwa serikali ya Kenya Kwanza, kikidai taifa linaongozwa na viongozi waliokataa Katiba.

Akihutubu katika kikao na wanahabari Jumatatu, Julai 24, 2023 jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa chama, Bw Jemeremiah Kioni alidai wananchi wasitarajie sheria kufuatwa akisema Rais William Ruto alikuwa miongoni mwa waliokataa Katiba ya sasa, iliyozinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

“Kenya kwa sasa inaongozwa na watu wasioheshimu Katiba, ndio maana visa vya kamatakamata ya watu wanaotofautiana nao vinashuhudiwa,” alisema Bw Kioni.

Katibu Mkuu huyo wa Jubilee (JP), alitoa matamshi hayo akirejelea kukamatwa kwa baadhi ya wabunge kadha wa Azimio na wafuasi wake kufuatia maandamano yaliyoitishwa na kinara wa muungano huo, Bw Raila Odinga.

Upinzani unapinga kupanda kwa gharama ya maisha, yanayozidi kulemea Wakenya.

Akihutubia waandishi wa habari, Bw Kioni pamoja na viongozi na wanasiasa wenza katika chama, alikuwa na nakala ya Katiba.

“Hii Katiba sasa ni nakala tu. Haifuatwi kamwe,” alilalamika Mbunge huyo wa zamani Ndaragwa.

Azimio imeapa kuendeleza maandano yaliyoratibiwa kufanyika siku tatu kila wiki, licha ya serikali kuyaharamisha.

Waandamanaji kadha wamepoteza maisha, na wengine kusalia kuuguza majeraha mabaya.

Maafisa wa polisi wamelaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi, Rais William Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua wakiwapongeza kwa kile wanahoji kama “kufanya kazi bora kulinda maisha na kuzuia uharibifu wa mali na biashara”.

  • Tags

You can share this post!

Njama ya Wanakandarasi kupora Murang’a Sh2.53 bilioni...

Mtoto Sagini: Washtakiwa waliomng’oa macho wasukumwa jela...

T L