• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
KIPWANI: Kipaji chake gumzo mtaani

KIPWANI: Kipaji chake gumzo mtaani

NA KALUME KAZUNGU

“MARA nyingi mimi hutumia kipawa changu cha kuimba kuwafundisha wanafunzi wangu darasani. Ajabu ni kwamba mbinu hiyo imenisaidia pakubwa kwani baadhi ya wanafunzi ambao hulala darasani au kuwa na ugumu wa kushika somo langu la Historia, hujipata wakifurahia na usingizi kuisha. Karibu wanafunzi wangu wote wanafanya vyema katika somo hilo!” asema Joseph Menza, al-maarufu Menzanoic Acid.

Menzanoic Acid anayefunza katika shule ya upili ya Siyu, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki, amekuwa gumzo mtaani kutokana na uimbaji wake sufufu wa nyimbo za injili na mbinu yake ya kufunza.

Aghalabu ukimkosa darasani, mtafute studioni akitunga, kuimba au kurekodi nyimbo zake.

Anasema kipaji chake kilichochewa na familia yake. Babake ni kiongozi mkuu wa kanisa vilevile mkufunzi mahiri wa kwaya. Nduguze wakubwa kwa wadogo, wote ni waimbaji na pia masogora katika upigaji wa ala za muziki kanisani.

Alipokuwa anasoma kidato, Menzanoic Acid anasema alitumia muda mwingi katika kukinoa kipaji chake. “Nilijiunga na kwaya ambayo kila mwaka iliwakilisha Pwani katika madaraja mbalimbali ya muziki nyakati hizo,” anasema.

Lakini swali ni je, mbona akajiita Menzanoic Acid?

“Nikiwa msanii wa nyimbo za injili, nilionelea kwamba ikiwa tindikali au ‘Sulphuric Acid’ inaogopewa na wanadamu, basi kukibuniwa Menzanoic Acid inayomtangaza Yesu, shetani ataogopa zaidi,” aeleza.

Kwa sasa anatamba kwa vibao sita Utabaki Mungu, Rosey, Niskize, Mtazame Yesu, Stress na Msaada Wangu.

Licha ya kwamba muziki wake wa injili anaufanyia Lamu,eneo lililo na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu, anaeleza kuwa hilo halijamvunja moyo.

Menzanoic Acid akitumbuiza mashabiki wake Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema baadhi ya vibao vyake amevifanya kwa mtindo wa kizazi kipya, japo ujumbe bado ni wa kumtukuza Mwenyezi Mungu, hali ambayo imepelekea muziki wake kuvuma miongoni mwa mashabiki ambao si Wakristo.

Anatoa mfano wa kibao chake Rosey anachosema kimemzolea sifa kochokocho ndani na nje ya Lamu. Wimbo huo unamuhusu Rosey ambaye mamake aliaga dunia na kumuacha bado kinda. Alibaki na babake ambaye baadaye alibadilika na kutaka kumbaka. Japo babake hakufaulu, alimuachia kidonda ambacho mpaka sasa kinamchoma. Ni hali wanayopitia wengi japo kimyakimya.

Anashikilia kuwa licha ya nyimbo za injili kutokuwa rahisi kupenya katika eneo linalotambua kwa wingi dini ya Kiislamu, Rosey kimeibuka kupendwa na kushabikiwa na wote, ikiwemo Mbunge wa Lamu Mashariki, Ali Athman Sharif.

Anasisitiza kuwa kilichomfanya kuimba nyimbo za injili hasa ni kutokana na imani yake ya Ukristo, kwamba sababu kuu ambayo mwanadamu aliumbwa ni kumuabudu na kumsifu Mungu.

Aidha anafichua kuwa katika nyimbo zake zote, wimbo wa Utabaki Mungu ndio anaoupigia upatu kwa sana kwani ulimvumisha.

Msanii huyu anasema licha ya kuwa si rahisi kwa mja kuzichoma mbili bila kuiunguza moja, kwa upande wake amefaulu katika taaluma yake ya Ualimu na pia Uimbaji.

Changamoto

Miongoni mwa changamoto anazopitia ni ukosefu wa studio nzuri au za hadhi inayostahili kurekodi muziki wake huko Lamu.

Anasema wakati mwingine pia hulazimika kukatiza mialiko anayopokea kama msanii kuhudhuria hafla mbalimbali kwani nyakati hizo humpasa kuwa darasani.

Aidha tatizo la baadhi ya vyombo vya habari hutaka kulipwa ili wacheze ngoma zake, humkwaza sababu bado mchanga ulingoni.

Isitoshe, anasema kuwa baadhi ya maprodusa ambao ni wasanii huishia kuharibu kazi za wasanii wanaochipuka,

Amewataka wasanii wanochipuka kujituma na kufanya utafiti wa kina iwapo wanataka kuendelea kuogelea katika bahari hii pana ya muziki.

Menzanoic Acid ameoa na ana watoto wawili.

You can share this post!

DOMO: Malipo hapa hapa duniani!

KASHESHE: ‘Mnikome!’

T L