• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
DOMO: Malipo hapa hapa duniani!

DOMO: Malipo hapa hapa duniani!

NA MWANAMIPASHO

KAMA kuna demu aliyeniacha hoi siku za hivi karibuni ni huyu Miss Mandi.

Alitrendi kwa siku tatu mfululizo baada ya Wakenya kumtunuku wadhifa adimu, mwenyekiti wa kamati ya roho chafu.

Aisee! Asikudanganye mtu, Wakenya wanaojiita KOT sio watu salama kabisa. Kheri kufinywa kidole na mlango kuliko kushambuliwa na KOT. Wanatafuna, hawabakishi mtu.

Kwa mfano, hebu wazia hili mtu kukuchamba hivi;”mwanamke roho mbaya na makalio ngumu kushinda kesi ya shamba…” Utajihisi vipi? Na hii ni kati ya chambo nilizoona afadhali, mengine yalikuwa ya aibu kwa kweli. Hata Miss Mandi alikiri kuumizwa na matusi yale.

Wale KOT walimshambulia kwa hali na muhali. Kwa kila namna waliyoijua. Ni kama vile walikuwa na kisasi. Wale ambao hawakuwahi kumsikia, kwa siku tatu hizo walijiongeza na kuja na matusi yao.

Wala mimi sikumwonea huruma hata kidogo. Huwezi ukawa binadamu mwenye roho ya kutu kwa wenzio. Huwezi ukakosa utu kama huyu bibiye. Huwezi ukawadhalilisha watu kwa sababu unajiona upo kwenye levo nyingine ya kimaisha. Hivi kama ni ishu ya levo, oksijeni unayopumua wewe ina tofauti gani na yule unayemdharau na kumwona shonde?

Picha ilianza baada ya Miss Mandi kujigeuza mshauri nasaha Twitter. Akaachia posti nzito ya kuwakebehi watu wenye tabia za ubinafsi. Kumbe naye yumo! Ikawa kuna dume moja, Koome Gitobu lililowahi kufanya kazi na binti wa watu. Acha jamaa aachie ‘thread’ ya mateso aliyopitia mikononi mwa Miss Mandi.

Miss Mandi alimdhalilisha kwa kila alichokifanya, alichovaa na kilichokuwa kimebakia ni yeye kwenda kuchungulia rangi ya haja ya Koome. Maskini mtoto wa Mungu, alikipatapata. Lakini ana kila sababu ya kuwashukuru KOT kwa kumlipizia. Malipo ya duniani, huwa hapa hapa duniani.

Baada ya kutakatishwa, Miss Mandi aliamua kutoa taarifa ndefu akiomba msamaha. Kilichonikwaza zaidi ni jinsi msamaha wa binti huyo ulivyokuwa na kona nyingi kuliko zile unazokutana nazo maeneo ya barabara ya kuelekea Mai Mahiu-Naivasha.

Mwanzo alikiri kuumizwa na yale matusi lakini pia kwa wakati huo, radhi yake ikawa ni ya kukwepa ukweli. Alidai eti matukio ya kumdhalilisha Koome yalifanyika miaka 9 iliyopita walipofanya kazi kwenye stesheni ya 1 FM. Alikwenda zaidi na kudai eti mwanzo hakumbuki vizuri kama alimdhalilisha. Tena akaongeza kwa kusema eti ni miaka mingi imepita na kuwa kabadilika.

Haya ni mazungumzo ya mwehu unajua! Haijalishi ulimdhalilisha mtu lini, iwe ni miaka 30, 50 au 100. La mno ni kuomba msamaha kwa matukio hayo bila ya kauli za chenga chenga. Baada ya hapo sasa sema miaka imeenda na umebadilika. Sio eti hukumbuki matukio hayo.

Hivi hata zile meseji za kipumbavu alizowatumia Butita walipokuwa wakiomba kazi kwenye stesheni aliyokuwa akifanya kazi 2013 nazo hazikumbuki? Huyu ni binti mbinafsi ajabu. Twitter anakesha kuhubiri anavyochukizwa na tabia chwara wakati yeye ndiye mwenyekiti. Anahitaji maombi na tambiko.

You can share this post!

Raila, mashabiki walaani mauaji ya kipenzi Juma

KIPWANI: Kipaji chake gumzo mtaani

T L