• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KIPWANI: Msupa wa kwanza produza katika Coke Studio ‘19

KIPWANI: Msupa wa kwanza produza katika Coke Studio ‘19

NA SINDA MATIKO

PWANI ina sifa mbili kwenye kuchipua vipaji.

Anapotokea msanii mwenye swag ya Uswahili kwenye uimbaji wake, yeye huhusishwa na Pwani moja kwa moja.

Sasa maelezo hapa huwa mawili, msanii husika atakuwa ni mzaliwa wa Pwani na ndio maana uimbaji wake una swag ya Kiswahili na kama basi sio mzaliwa, itakuwa alilelewa Pwani.

Sanapei Tande, Otile Brown ni baadhi tu ya mastaa waliotokea Bara ila unapowahesabu wasanii wa Pwani lazima nao uwataje sababu makuzi yao kule yaliwabadilisha na kuwafanya Wapwani.

Yupo pia Viola Karuri produsa wa kike mkali ambaye alihiti 2017 baada ya kufanya kava ya hit ya Despacito kwa Kiswahili.

Kazi zake kadhaa zilizofuata, Viola alizirekodi na kuimba kwa Kiswahili sanifu kiasi cha kuwachanganya wengi walioamini anatokea Bara.

Mwenyewe wajua ulinishtua kidogo?

Kwa nini sasa? Kisa nazungumza Kiswahili kwa ufasaha?

Eeh?

Haha, wajua wengi wananichukulia kuwa binti wa mjini ila hata uswahilini nipo. Natokea Meru ila maisha yangu ya awali nilikulia Mombasa na maeneo mengine ya Pwani. Lakini pia Tanzania sababu wazazi wangu walikuwa watu wa kutalii wakitafuta maisha, hayo ndio maisha yaliyonisanifishia Kiswahili changu.

Eti eeh?

Lakini hata zaidi zipo sababu zinginezo. Mwanzo mamangu ni Mchagga, mojawepo ya makabila ya kule Tanzania halafu ongeza na kukulia Mombasa toka nikiwa binti wa miaka 12.

Uliweka historia ya kuwa msupa wa kwanza kuwa produsa kwenye Coke Studio 2019.

Ilikuwa ni tukio kubwa sana kwangu, ukizingatia kwamba wanawake kwenye tasnia hii ya utayarishaji muziki hatuheshimishwi.

Isitoshe ilikuwa tukio la kuthibitisha uwezo wangu kama mtayarishaji muziki sababu ndio taaluma niliyosomea.

Kipaji kipo, kwa nini ukasomea tena muziki?

Ndio kipaji kipo tena cha kuzaliwa, lakini katika kuifanyia maboresho zaidi nilijiunga na Berklee College of Music kule Boston Marekani alikopitia pia Eric Wainaina.

Ndiko nilikosomea jinsi ya kuandaa muziki, kuandika mashairi , kutia zile vokali na mambo mengine ya kimuziki.

Kando na kuheshimishwa, Coke Studio ilikujenga vipi?

Ukiachia mbali koneksheni nilizotengeneza kwa kutangamana na wasanii wengine pamoja na maproduza aina aina, ni kwamba nilipiga mkwanja mzuri tu.

Hii ni kwa sababu unapokuwa pale, maisha yako na shughuli zinginezo yanasimama hivyo ili kukuweka pale inabidi ulipwe. Niliunda pochi nene.

Ukiwa Marekani, pia ulipata fursa ya kufanya kazi na manguli kama Naomi Campbell, na hata kutengeneza sauti za filamu za Harry Porter. Najiuliza mbona usingepambania nafasi yako Marekani?

Mwanzo kabisa nilipoondoka Kenya kwenda Marekani, lengo lilikuwa ni kusomea muziki kisha nirejee nyumbani kufanyia huku.

Pili kutoboa kwenye muziki wa Marekani sio rahisi ki hivyo, wale wana watu wao kama vile Beyonce isitoshe tamaduni na muziki wao ni tofauti kabisa na wa kwetu.

Ila umekuwa kimya sana kwa miaka kadhaa?

Ndio maisha ya muziki kuna nyakati unakuwa upo wakati mwingine unavuta pumzi kujipanga zaidi. Lakini pia nimekuwa nikishughulika zaidi na utayarishaji wa kazi kadhaa ambazo bado hazijaachiwa.

Kwa juhudi zako kwenye muziki nahisi kama bado jina lako sio kubwa inavyotakiwa, kwa nini?

Labda unieleze mdogo wangu. Sababu naamini katika Play Ke ambayo nyie wanahabari mumekuwa mkitukandamiza. Pili, muziki wangu naamini una uzito. Pengine sichezwi vya kutosha au sijui ni kwa sababu napata shoo nyingi za bendi, sielewi. Ila hainifishi moyo mimi, nashukuru kwa wale wachache wanaonitambua.

Maisha ya mwanamuziki wa kike Kenya yakoje?

Magumu kwa kiasi fulani. Watoto wa kike tunapitia mitihani mingi tu. Wapo wengi wameacha kwa sababu wapenzi wao hawakuwasapoti kwa kuhisi ni kazi ya kihuni.

Pili hatujawezeshwa, wengi wetu hatuna fedha za kutosha kusukuma miradi ya usanii ambayo ni ghali, hilo pia linatukwamisha.

Tatu ni kwamba wapo wadau katika tasnia ambao ukitaka msaada wao watakutaka kimapenzi mwanzo.

Wewe unayamudu vipi?

Mwanzo nina mume mwelewa sana kwa sababu tulikutana naye nikiwa Chuoni Berkelee kwa hiyo sapoti yake ninayo kwa asilimia 100.

Pili nina mipaka yangu, ambayo siwezi kuivuka au kujivunjia heshima.

Na bado wanaume wanakutongoza?

Watakosaje wakati mtoto mzuri huyu. Ndio hulka ya wanaume, hawajali kama umeolewa au la. Ila huwa ninajua namna ya kusonga nao na kuhakikisha sivuki mipaka yangu.

Miaka ya nyuma kuliwahi kuzuka tetesi kwamba ulikuwa na mahusiano na staa wa RnB Treyz Songz?

Hahaha! Mnachekesha sasa, nyie wanahabari kweli wambea. Ipo hivi, nilikuwa nimesafiri Botswana kwenda kuandaa shoo ya Treyz na nikapata fursa ya kupiga picha naye. Sasa kuposti mkaamua kujijazia.

Mume wangu alicheka sana sababu hata nikiondoka alijua nipo wapi na nafanya nini.

Kwenye ndoa tuhesabu miaka mingapi?

Zaidi ya mwongo na nusu sasa.

Watoto nao?

Wapo wakose kwa nini.

Wangapi?

Haha! Umeanza umbea sasa kaka.

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: Miaka 10 akiwa singo na hajuti

Raila kupiga lami baada ya AU kumwonyesha lango

T L