• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kitakachofuata kuhusu mauaji ya Jeff Mwathi?

Kitakachofuata kuhusu mauaji ya Jeff Mwathi?

Na SAMMY WAWERU

IDARA ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI), kitengo maalum kinachoshughulikia masuala ya mauaji kilitangaza jana kukamilisha uchunguzi wa kifo cha Jeff Mwathi aliyefariki Februari 22, mwaka huu katika hali isiyoeleweka.

Kupitia taarifa, DCI ilisema Ijumaa adhuhuri uchunguzi ulikamilika baada ya kupokea ripoti ya upasuaji kutoka kwa Mtaalamu Mpasuaji Mkuu wa Serikali.

Kufuatia ghadhabu za Wakenya mitandaoni, Mkurugenzi Mkuu wa DCI, Bw Mohamed Amin aliagiza uchunguzi unaozingira kifo cha mwanamitindo huyo kufanywa upya.

Msukumo huo ulitokana na amri ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki aliyeahidi kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waliohusika na mauaji ya Jeff, 23.

“Faili imekabidhiwa Mkurugenzi Mkuu Mashtaka ya Umma (DPP), kuikagua na kutoa ushauri,” sehemu ya taarifa ya DCI ilielezea.

Miezi miwili baada ya kijana huyo kuuawa kinyama, hakuna aliyetiwa nguvuni kujikokota kwa kesi hiyo kukiibua maswali chungu nzima.

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi, Lawrence Njuguna maarufu kama DJ Fatxo anahusishwa na mauaji hayo ikizingatiwa kuwa Jeff alikumbana na mauti katika nyumba ya msanii huyo eneo la Roysambu, Nairobi.

Lawrence Njuguna almaarufu Dj Fatxo mwimbaji wa Mugithi anahusishwa na mauaji ya Jeff Mwathi. Picha / HISANI

Awali, uchunguzi uliofanywa na maafisa wa DCI Kituo cha Polisi cha Kasarani ulidai kijana Jeff alijitia kitanzi.

Kauli hiyo hata hivyo ilifutiliwa mbali na kitengo maalum cha DCI kinachoshughulikia masuala ya mauaji.

Mahakama aidha iliamuru kufukuliwa kwa mwili wa Jeff, na uchunguzi zaidi kufanyika.

Marudio ya upasuaji yaliyofanyika Machi 31 na Dkt Johansen Oduor (Mpasuaji Mkuu wa Serikali), yaliashiria kijana huyo alifariki kutokana na majeraha mabaya kichwani na mapajani.

Dkt Oduor aliambia wanahabari kuwa Mwathi pia alikuwa na majeraha mabaya shingoni.

Kwa upande mwingine, tetesi zinahoji alinajisiwa kabla ya kutendewa unyama uliomkumba.

DCI imekamilisha uchunguzi wake, faili tayari imekabidhiwa DPP Noordin Haji kwa ukaguzi na kutoa mwelekeo, ni kipi kitakachofuata Jeff Mwathi kupata haki?

Kisa cha kijana huyo kikiendelea kuzua mdahalo mkali mitandaoni, ni kina nani hao waliochukua nafsi yake na kwa nini imechukua muda mrefu kukamatwa na kuchukuliwa hatua kisheria?

Ni nani huyo analinda mhalifu/wahalifu wanaopaswa kuwa jela?

Korti na DCI wasisahau Wakenya wangali na makovu ya mauaji ya kikatili ya ndugu wawili Kianjokoma, Embu 2021 waliofariki mikononi mwa askari.

Familia ya vijana hao ikisubiri haki kutendeka, kisa cha Jeff kitachukua mkondo upi?

DCI, DPP na Idara ya mahakama ina mlima wa kibarua kuhakikisha haki inapatikana, Kenya isiwe sawa na shamba la wanyama ambapo kuna wanyama muhimu kuliko wengine.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa dini ya Kiislamu wataka waumini kusubiri...

Kipindupindu: Wafungwa wa gereza la Thika waendelea kupata...

T L