• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Korti yatupa baadhi ya ushahidi wa mume anayetaka kutaliki mke

Korti yatupa baadhi ya ushahidi wa mume anayetaka kutaliki mke

Na SAM KIPLAGAT

MISINGI ya mtu kupatiwa talaka ni wazi kabisa – ukatili, usherati, kuthibitisha kwamba ndoa hiyo imevunjika kabisa au wakati mwanandoa amemtelekeza mwenzake kwa angalau miaka miwili.

Aghalabu, huwa ni rahisi kuthibitisha misingi hii na kupata kibali cha korti cha kufungua pingu za ndoa na kuvunja ahadi. Lakini ni upeo upi mwanamume au mwanamke anaweza kufika akitafuta ushahidi wa kuthibitisha usherati kwa mfano?

Naam, juhudi za mwanamume za kukusanya ushahidi thabiti iwezekanavyo ili kuthibitisha madai ya usherati dhidi ya mke wake ziligonga mwamba wakati Mahakama Kuu ilipomzuia kutumia faili kadhaa – ikiwemo mawasiliano ya simu yaliyorekodiwa, picha, matukio yaliyorekodiwa kwenye CCTV na jumbe kutoka akaunti ya mke kwenye WhatsApp, kwa sababu ulipatikana kinyume cha sheria.

Mwanamume huyo aliyetambulishwa kama KKR kwa sababu za kisheria, alikuwa amekusanya jumla ya faili 68 za ushahidi alizokusudia kutumia katika kesi ya talaka iliyowasilishwa mbele ya hakimu wa Korti ya Milimani.

Hata hivyo, mkewe aliyetambulishwa kama RC, alikanusha jumla ya vipengele 45 kwa sababu vilikusanywa kwa njia iliyokiuka haki na hadhi yake yake kuhusu habari za siri na kuwasilisha kesi katika Mahakama Kuu.

Jaji Anthony Mrima alikubaliana naye katika baadhi ya malalamishi na kufutilia mbali ushahidi huo, akisema hauwezi ukawasilishwa kama ushahidi katika kesi ya talaka. “Kauli imetolewa kuwa hatua ya Mlalamishi ya kuweka kisiri kamera za CCTV chumbani mwa mtoto wao ambamo mshtakiwa anaishi kwa sasa, hatua ya mlalamishi ya kuweka kisiri vinasa sauti kwa lengo la kurekodi mazungumzo ya siri ya mshtakiwa, hatua ya mlalamishi ya kutumia kisiri mpelelezi wa kibinafsi pamoja na hatua ya mlalamishi ya kufungua baruameme na akaunti za mshtakiwa katika mitandao ya kijamii bila idhini kutoka kwa mlalamishi, yote hayo yanakiuka Vifungu vya Sheria 28, 31 na 50(4) vya Katiba,” ilisema korti.

Ushahidi uliowasilishwa kortini ulionyesha kuwa KKR alikuwa pia amempa kazi mpelelezi wa kibinafsi aliyempiga picha mke wake, akaweka kamera za CCTV chumbani na eneo linalozingira nyumba yao, akaweka vinasa sauti katika gari lake, hayo yote katika juhudi za kukusanya ushahidi.

Aidha mpelelezi huyo aliopoa jumbe kutoka simu ya mshtakiwa. Ndoa ya wawili hao ilisambaratika mnamo 2019 ambapo KKR aliwasilisha kesi akiomba kumtaliki mkewe kwa misingi ya ukatili na usherati. Aliitisha vilevile kuachiwa usimamizi wa watoto wao wawili.

RC, hata hivyo, alipinga ushahidi huo kutumiwa akihoji kwamba ulikusanywa kupitia njia ya siri, mbinu inayoingilia faragha ya mtu binafsi na kinyume na sheria kupitia vinasa sauti vilivyowekwa kisiri, kuingia bila idhini katika baruameme na akaunti zake kwenye mitandao ya kijamii na kamera za siri.

Alihoji kuwa uchunguzi uliofanywa bila kibali, kinyume na sheria na kisiri, kurekodi na kuingilia simu yake binafsi, baruameme na mitandao ya kijamii, unakiuka haki zake katika Kifungu cha Sheria 50(4) kinachokataza ushahidi kukusanywa kwa njia inayokiuka haki na uhuru wake kimsingi.

Mwanamume huyo alitetea hatua ya kumwajiri mpelelezi wa kibinafsi akisema hatua hiyo iliambatana na sheria na kwamba ushahidi wote aliokusanya ulikuwa halali na unaoweza kutumika.

Jaji Mrima, hata hivyo, alitoa uamuzi kuwa kuna hatari kuu katika utekelezaji haki endapo mbinu ya kukusanya ushahidi haitajikita katika Katiba na sheria.

“Haiwezi kuwa ndio mtindo kwamba kila mtu anaweza kufanya jinsi apendavyo katika ukusanyaji wa ushahidi hasi dhidi ya mwenzake. Ni sharti kuwe na utaratibu unaoelekeza mambo katika masuala ya umma pamoja na masuala ya kibinafsi vile vile. Ni utaratibu huo unaohitajika na Katiba ya sheria,” alisema Jaji.

Alieleza kuwa hatua ya kuweka kisiri kamera za CCTV na vinasa sauti ili kurekodi mawasiliano na nyendo za siri za mtu, isipokuwa ikiwa imeidhinishwa kisheria, kando na kuwa ya kuchukiza, haitarajiwi vilevile katika enzi hii ya katiba mpya.

“Hatua hiyo ni sawa na kuingilia hadharani faragha na hadhi ya mtu,” alisema.

Alieleza kuwa kuna njia kadhaa za kisheria ambazo KKR angeamua kutumia kupata habari alizohitaji.

Kwa mfano, jaji huyo alisema kuwa, mshtakiwa angeripoti suala hilo kwa polisi, uchunguzi uanzishwe kuhusiana na uavyaji mimba unaodaiwa kufanywa na mke wake, ambao ni hatia kisheria.

“Ikiwa tabia kama hiyo kutoka kwa raia wa kibinafsi haitadhibitiwa na kuelekezwa ipasavyo, matokeo yake yatakuwa kuchochea vurugu katika jamii. Itakuwa wazi kwa kila mtu kwenda huku na huko akikusanya ushahidi dhidi ya mwenzake katika njia yoyote. Tabia kama hizo ni sharti zidhibitiwe,” alisema.

Mume huyo alikuwa amedai kwamba kampuni hiyo inayoendeshwa na familia yake ilikuwa imeidhinisha uwekaji wa vifaa vya kufuatilia mienendo ya mtu na vinasa sauti katika magari.

Jaji Mrima alipuuzilia mbali madai hayo akisema hatua ya kuweka kinasa sauti kwenye gari inayotumiwa kwa kawaida na mwanamke huyo ilikiuka haki zake kuhusu faragha na hadhi.

Korti, hata hivyo, ilisema kuwa kamera zote za CCTV zilizowekwa kwenye lango, sebuleni, chumba cha kujiliwaza, chumba cha maakuli na chumba cha kulala ambacho kwa sasa hutumiwa na mume, ziliwekwa kwa ufahamu na idhini ya wanandoa hao. Mahakama ilifutilia mbali ushahidi uliorekodiwa katika chumba cha mtoto wao ambacho kinatumiwa na mwanamke huyo, ikisema hakuna ushahidi kwamba hatua hiyo iliidhinishwa na wote wawili.

“Hatimaye, Mahakama hii imepata na kushikilia kwamba katika kesi hii, ushahidi wowote uliokusanywa kutoka kamera za CCTV zilizowekwa kisiri katika chumba cha mtoto wa wanandoa hao, ushahidi kutoka kwa kinasa sauti chochote, ushahidi uliokusanywa na mpelelezi wa kibinafsi na ushahidi wowote kutoka kwa baruameme na mitandao ulikusanywa kinyume na sheria na unavuruga utekelezaji wa haki,” alisema.

Korti hata hivyo iliruhusu matumizi ya Kitabu cha Matuko kilichotolewa kama ushahidi ikisema kuwa matini ya OB ni nakala ya umma. Aliruhusu pia vipimo vya ujauzito ambavyo mwanamume huyo anadai kuwa mkewe alikuwa amebeba mimba nje ya ndoa lakini akaavya baadaye. Ushahidi ulipatikana katika chumba cha mtoto wao.

“Mlalamishi hakanushi mahali ambapo mshtakiwa alipata hayo. Ushahidi unakubaliwa,” korti ilisema.

Ushahidi mwingine uliotupwa nje ni pamoja na mazungumzo ya mwanamke huyo na mwanawe na mengine na anayedaiwa kuwa mpenziwe, picha za mawasiliano yake kibinafsi matukio kwenye shajara yake, tiketi za ndege na risiti, kwa sababu ulipatikana kwa njia haramu. Jaji huyo alisema katika ndoa, wakati vifaa kama hivyo vinakusudiwa kuwekwa ama ndani ya boma au katika eneo linalozingira boma, wanandoa ni sharti wakubaliane.

“Sababu ni kwamba kamera hurekodi picha kadhaa ambazo zinahusu faragha ya mtu. Ikiwa vifaa hivyo vitawekwa bila ya wanandoa kufahamu, kuna uwezekano wa masuala muhimu yanayohusu faragha na hadhi ya mtu kuibuka,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Itambue siri kubwa ya ibada ya kufunga...

MUTUA: Kinoti arekebishe kosa si kushtumu wanahabari