• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:50 AM
VYAMA VYA KISWAHILI: Chama dawa mjarabu kukabili mitazamo hasi kuhusu lugha shuleni Minhaj, jijini Nairobi

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama dawa mjarabu kukabili mitazamo hasi kuhusu lugha shuleni Minhaj, jijini Nairobi

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Minhaj Academy (CHAKIMA) kilianzishwa kwa lengo la kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu somo la Kiswahili na kukuza talanta zao katika sanaa mbalimbali.

Ikiongozwa na Bw David Chombo, kamati ya walimu wa Kiswahili shuleni humo iliteua jopo la wanafunzi ambao walitwikwa jukumu la kuwa vinara wa chama baada ya kubaini utashi wao katika Kiswahili.

Kupitia CHAKIMA, wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Minhaj Academy katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi walifunguliwa milango ya kuanza kukithamini Kiswahili, kumudu sarufi na kuandika insha za kusisimua.

Tangu kiasisiwe, chama hiki kimekuwa chombo maridhawa kinachotumiwa na wanafunzi wa Minhaj Academy kuzizamia baadhi ya mada ambazo huwatatiza madarasani.

Mbali na kutekeleza jukumu kubwa la kutambua na kukuza vipaji mbalimbali vya wanafunzi katika utunzi wa kazi bunilizi na kughani mashairi kwa mahadhi mbalimbali, chama pia hutoa jukwaa kwa wanafunzi kujifundisha jinsi ya kuwa mahatibu mahiri, wanahabari stadi na waigizaji shupavu.

Wakati wa kubuniwa, chama kilikuwa na wanafunzi wachache mno. Hata hivyo, hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka michache iliyopita zilivutia wanafunzi wengi kujiunga nacho.

Kwa usaidizi wa walimu wa Kiswahili ambao ni Bw Eric Muteti, Bw Alfred Otieno na Bw Dominic, chama kina mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa madhumuni ya kuwakutanisha wanafunzi na baadhi ya walimu, wanahabari na waandishi maarufu wa Kiswahili kutoka humu nchini.

Wanapokuwa shuleni kwa masomo ya kawaida, wanachama huandaa kongamano la Kiswahili kila muhula ili kujadili masuala mbalimbali katika Kiswahili.

Walezi wa chama wamehakikisha kuwa kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili na nakala za magazeti ya Taifa Leo maktabani.

Wanachama hukutana mara kwa mara kujadili masuala mbalimbali kuhusu uandishi wa insha na kazi nyinginezo za kibunifu.

Chini ya uongozi wa Bw Muteti, Idara ya Kiswahili imekuwa imara katika kuandaa maswali elekezi ambayo hujadiliwa na wanafunzi katika vikao vya CHAKIMA. Kufaulu kwa mikakati hiyo kunahitaji ushirikiano mkubwa kwa kuwa kidole kimoja hakivunji chawa.

Uwapo wa chama hiki shuleni umeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji wakubwa wa gazeti la Taifa Leo.

Baadhi ya changamoto zinazokabili CHAKIMA ni kijisehemu cha wanafunzi kutokionea fahari Kiswahili pamoja na ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli mbalimbali za chama ambacho kwa sasa kinalenga kuchapisha jarida la Kiswahili mara moja kwa mwaka.

Minhaj Academy. Picha/ Chris Adungo

Changamoto nyingine ni donda sugu la msimbo wa Sheng ambao unatishia kulemaza umilisi wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Ingawa hivyo, chama kinajitahidi kuwa jukwaa mwafaka la kuchochea wanafunzi wa Minhaj Academy kufaulu vyema katika mitihani ya KCPE.

Zaidi ya kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, madhumuni mengine ya CHAKIMA ni kustawisha matumizi ya lugha shuleni na kupanua mawanda ya elimu katika nyanja nyinginezo zinazofungamana na Kiswahili.

Chama pia kimejitolea kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine kuboresha matokeo ya mitihani katika masomo yote yanayotahiniwa katika KCSE.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Georginah Nyatichi

Omanyala ni miongoni mwa walioalikwa kuhudhuria maadhimisho...

T L