• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
GWIJI WA WIKI: Georginah Nyatichi

GWIJI WA WIKI: Georginah Nyatichi

Na CHRIS ADUNGO

KAZI bora ya uandishi ni zao la bidii, stahamala na utafiti wa kina. Hakuna mafanikio ambayo mtu atayapata bila kujituma!

Tupo jinsi tulivyo kwa sababu ubora wetu umechangiwa na watu wengine. Teua marafiki watakaokupiga jeki na kukusogeza karibu na malengo yako. Nyati mwenda pweke ni windo rahisi la simba!

Mtangulize Mungu katika kila jambo, uwe na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika shughuli zako na uithamini sana familia yako. Usitamauke unapokosa kufaulu. Endelea kukazana na hatimaye milango ya heri itajifungua!

Huu ndio ushauri wa Bi Georginah Nyatichi Makini – mwandishi mzoefu na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Nyaikuro, Kaunti ya Nyamira.

MAISHA YA AWALI: Nyatichi alizaliwa katika kijiji cha Mwamisoko, eneo la Bomwanda, Kaunti ya Kisii. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa marehemu Mzee Michael Makini na Mama Teresia Kemunto.

Nduguze Nyatichi ni Thomas Mogere, Cosmas Mwasi, Irine Bosibori na Edinah Mariechana.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Mwamisoko (1987-1994) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Peter’s Suneka, Kaunti ya Kisii mnamo 1995.

Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mnamo 1998 na akapata nafasi ya kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza) katika Chuo Kikuu cha Nairobi (Bewa la Kikuyu) kati ya 2000-2005.

Miongoni mwa wahadhiri waliompokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kumchochea pakubwa kukichangamkia Kiswahili ni Dkt Rayya Timammy, Dkt James Zaja Omboga na Dkt Amiri Swaleh.

Ilikuwa hadi 2013 ambapo Nyatichi alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya uzamili. Alifuzu katika 2017 baada ya kuwasilisha tasnifu “Udhihirikaji wa kanuni ya Dahl katika lugha ya Ekegusii” chini ya usimamizi wa Prof Ireri Mbaabu na Dkt Leonard Chacha.

Nyatichi kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Moi. Miongoni mwa waelekezi wake ni Prof Samuel Obuchi, Prof Mark Mosol Kandagor, Prof Robert Oduori, Dkt Magdaline Wafula na Dkt Noordin Mwanakombo.

UALIMU: Nyatichi alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Matongo, Kisii pindi baada ya kuhitimu chuoni. Alihudumu huko hadi Oktoba 2006 ambapo alijiariwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) na kutumwa kufundisha katika Shule ya Upili ya Kiendege, Kaunti ya Nyamira.

Alipata uhamisho hadi Shule ya Upili ya Nyaikuro mnamo Mei 2017 na kwa sasa ndiye mkuu wa somo la Kiswahili na mwalimu msaidizi katika Idara ya Ushauri Nasaha katika shule hiyo inayoongozwa na Dkt Eric Wara (Mwalimu Mkuu).

Mbali na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili shuleni, Nyatichi amekuwa mstari wa mbele kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano mbalimbali ya uigizaji, utunzi wa mashairi, ulumbi na uandishi wa kazi bunilizi.

Anashikilia kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano wa kiko na digali miongoni mwa walimu katika Idara ya Lugha ni nguzo na mhimili wa mafanikio wanayojivunia kila mwaka katika KCSE Kiswahili.

Bi Georginah Nyatichi Makini – mwandishi mahiri na mwalimu mbobevu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Nyaikuro, Kaunti ya Nyamira. Picha/Chris Adungo

Walimu wanaoshirikiana naye kwa sasa kuendesha gurudumu la Kiswahili shuleni Nyaikuro ni Bw Manyanya, Bw Orito, Bw Manyange, Bi Kemunto, Bi Bwari, Bi Bochaberi, Bi Onyinkwa na Bw Haggai (Mkuu wa Idara).

Nyatichi amekuwa mtahini wa kitaifa wa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) tangu 2017. Uzoefu wake katika utahini wa Karatasi ya Pili ya Kiswahili (KAR 102/2) umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu wenzake na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

UANDISHI: Nyatichi alitambua kipaji chake cha uandishi akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha.

Umilisi wake wa Kiswahili ulimfanya kuwa maarufu mno miongoni mwa wanafunzi wenzake katika shule ya upili. Baadhi yao walimtaka awaandikie barua za kuwatumia marafiki zao katika shule nyinginezo – za mbali na karibu.

Walimu pia walitia azma ya kumpa Nyatichi majukwaa maridhawa ya kupalilia kipaji chake cha uandishi baada ya kutambua upekee na ukubwa wa uwezo wake katika Kiswahili.

Alitunga idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na akapata fursa adhimu za kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Bw Timothy Omusikoyo Sumba ni miongoni mwa mikota wa lugha wanaozidi kumhimiza Nyatichi kuogelea katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili. Ndiye alimshika Nyatichi mkono na kumwelekeza kwa wachapishaji kadhaa wa vitabu walioanza kufyatua kazi zake za uandishi.

Kufikia sasa, Nyatichi amechangia mashairi katika diwani ‘Malenga wa Afrika’ na ‘Malenga wa Kenya’ zilizochapishwa na African Ink Publishers (AIP) na Elong’o Publishers mtawalia. Tungo zake pia huchapishwa mara kwa mara katika gazeti hili la ‘Taifa Leo’.

Baadhi ya hadithi zake ni ‘Jina la Mume Wangu’ katika mkusanyiko wa ‘Jela ya Wendawazimu na Hadithi Nyingine’ na ‘Likizo ya Lazima’ katika antholojia ya ‘Maisha Karakana na Hadithi Nyingine’.

Nyatichi ndiye mwandishi wa hadithi ‘Awando na Ayando’ katika diwani ya watoto ya ‘Zawadi ya Babu na Hadithi Nyingine’ iliyotolewa na Kitovu cha Hadithi Publishers mnamo 2021. Anapania sasa kuandika vitabu vingi vya hadithi za watoto kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC).

JIVUNIO: Kubwa zaidi katika maazimio ya Nyatichi ni kuwa mwandishi maarufu na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu. Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Kwa pamoja na mumewe Bw Caleb Nyangaresi, wamejaliwa watoto watatu – Esther Kemunto, Elias Nyangari na Elsie Bochere.

You can share this post!

‘Deep State’ ilivyozima mashujaa

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama dawa mjarabu kukabili mitazamo...

T L