• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
GWIJI WA WIKI: Abel Nyamari

GWIJI WA WIKI: Abel Nyamari

NA CHRIS ADUNGO

KUANDIKA kazi yoyote ya fasihi kunahitaji wakati, utulivu na wito wa ndani ya nafsi.

Huwezi kujilazimisha kutunga.

Huu ndio mtazamo wa Bw Abel Nyamari ambaye kiu ya kuchangia makuzi ya Kiswahili kupitia sanaa ya uandishi ilianza kumtambalia katika umri mdogo.

Kwa mtazamo wake, mwandishi asiye na ujuzi wa kutumia lugha kwa ufundi hukosa uhuru wa kusema anachokitaka kwa jinsi anavyotamani kifikie hadhira yake.

“Ingawa uhuru wa mwandishi umo katika utashi na falsafa yake, lugha ndicho kitovu cha kazi ya fasihi na kamba inayovuta hadhira kwa dhamira ya sanaa,” anasema.

Abel alilelewa katika eneo la Mosocho, Kaunti ya Kisii. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa Bw Fredrick Nyamari na Bi Dorcas Bitutu. Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi R.M Gudka Memorial, Kisii (1999-2008) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Koelel Forces Academy, Gilgil (2009-2012).

Ingawa matamanio yake yalikuwa kuwa, alihiari kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (2013-2017). Akiwa huko, alijiunga na Chama cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Kenyatta (CHAKIKE) na akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu (2014-2016).

Alikuwa pia mstari wa mbele kuhakikisha kuwa CHAKIKE kinawakilishwa vyema humu nchini na katika makongamano mbalimbali ya kimataifa yaliyofanyika chini ya mwavuli wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Makongamano hayo yalimpa fursa maridhawa za kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti na ufundishaji wa Kiswahili.

Guru Ustadh Wallah Bin Wallah aliwahi kumtuza kwenye sherehe za Kumi Kumi kituoni WASTA Matasia, Ngong mnamo 2014, 2015 na 2016.

Baada ya kushiriki mafunzo ya nyanjani katika Shule ya Upili ya Randani, Kisii (2016), Abel alihamia Nyali, Kaunti ya Mombasa ili kuzamia utafiti wa Fasihi za Kiafrika (2018-2019). Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Hema–Chitago iliyoko Kisii kati ya 2019 na 2021 na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Utunzi wa mashairi na uandishi wa vitabu ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Abel tangu utotoni. Insha nyingi alizoandika shuleni zilimvunia tuzo za haiba na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Akiwa chuoni, alishirikiana na washairi wengine, akiwemo Bi Halima Zainabu kutunga mashairi ya majibizano.

Mengi ya mashairi hayo yalishabikiwa pakubwa kila yalipopeperushwa na idhaa ya KU 99.9 FM katika kipindi ‘Mizani ya Lugha’.

Shairi ‘Handisheki’ alilotunga kwa ushirikiano na mwalimu Felix Onsongo lilikaririwa na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Hema–Chitago katika mashindano ya tamasha za kitaifa za drama mnamo 2020 na likatia fora hadi kiwango cha kaunti.

Kampuni ya Elong’o Publishers ilimfyatulia riwaya ‘Kivuli cha Usaliti’ mnamo Machi 2023 na ikapokelewa vyema na wapenzi wa fasihi ndani na nje ya Kenya. Amechangia pia hadithi fupi ‘Mganga Kofia Nyekundu’ katika antholojia ‘Uchungu wa Mwana’ (Elong’o Publishers, Novemba 2023).

Abel anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi chipukizi wanaotangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Amepania pia kutumia ujuzi wake wa ualimu kuelekeza vijana katika masuala ya maadili, jinsi ya kujitegemea na kukabili changamoto mbalimbali maishani.

Kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kujiendeleza kitaaluma na kuwa miongoni mwa wahamasishaji wakuu wa Kiswahili kupitia uandishi wa Fasihi ya Kiafrika.

Kwa pamoja na mkewe Bi Claire Adhiambo wamejaliwa mtoto wa kike, Noelle Kimberley.

  • Tags

You can share this post!

Hofu genge la uhalifu likilenga sasa kupora wamiliki wa...

Mwanamke ashtakiwa kuvunja kioo cha gari la Mercedes la...

T L