• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
GWIJI WA WIKI: Sasha Kenya

GWIJI WA WIKI: Sasha Kenya

Na CHRIS ADUNGO

KISWAHILI ni miongoni mwa lugha kuu za Kiafrika zinazozungumzwa na idadi kubwa zaidi ya watu nchini Amerika.

Kwa mujibu wa kampuni ya tafsiri ya Akorbi jijini Dallas, Jimbo la Texas, watumiaji wa Kiswahili nchini Amerika waliongezeka kwa asilimia 22 kati ya 2016 na 2018 baada ya lugha hii kuanza kufundishwa katika takriban vyuo vikuu 100.

Euphresia Likhanga Sasha Kenya ni miongoni mwa Wakenya ambao ni mabalozi wa Kiswahili nchini Amerika. Yeye ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, mshairi shupavu, mwigizaji stadi, mjasiriamali na muuguzi.

“Kiswahili kilinibishia milango nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nilikifungulia na kikapata makao salama na ya kudumu ndani ya moyo wangu.”

“Nilianza kukitumikisha kupitia mashairi, nyimbo na michezo ya kuigiza nyakati za tamasha za kitaifa za muziki na drama chini ya uelekezi wa Bw Toili Khisa aliyenifundisha katika shule ya upili,” anasema.

Sasha alilelewa katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi na akakulia baadaye katika mtaa wa Kawangware, Nairobi.

Sasha Kenya wakati wa mahojiano. Yeye ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, mshairi shupavu, mwigizaji stadi, mjasiriamali na muuguzi nchini Amerika. PICHA | CHRIS ADUNGO

Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa Bw Bernard Likhanga na Bi Colleta Musonye aliyekuwa mwimbaji katika Kwaya ya Ikulu na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Lang’ata Road, Nairobi, kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Chamakanga Girls, Kaunti ya Vihiga (2001-2004). Alisomea Stashahada ya Juu (Higher Diploma) katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika taasisi ya Kenya School of Professional Studies, Parklands, Nairobi (2006-2008).

Baada ya kufaulu vyema katika mitihani ya TOEFL na ASSET mnamo 2008, Sasha alipata fursa ya kusomea katika Chuo cha Principia, eneo la St Louis, Missouri, Amerika. Ni wakati uo huo ambapo ombi lake la kuwa muuguzi katika kituo kimoja kinachoendeshwa kwa kanuni za Sayansi ya Kikristo jijini Boston, Jimbo la Massachusetts, Amerika, lilikuwa limekubalika.

Japo alifunga safari ya kuelekea Amerika mnamo 2009 akiwa na azma ya kushika mambo mawili (kujiendeleza kielimu na kutafuta riziki), ugumu wa ratiba ya kazi ya uuguzi ulimzimia ghafla mshumaa wa masomo.

Alirejea Kenya mnamo 2012 kufunga pingu za maisha kabla ya kurudi Amerika baada ya miezi minne. Hata hivyo, alipitia misukosuko tele katika ndoa na akatalikiana na mumewe mnamo 2018.

Mnamo 2017, Sasha alihamia Jimbo la Ohio, Amerika na akapanda ngazi kuwa mshauri na mwelekezi mkuu wa wauguzi wachanga. Tangu 2018, amekuwa mkazi wa Jimbo la New Jersey anakofanyia shughuli za uuguzi na ujasiriamali.

Ilikuwa hadi 2021 ambapo alijitosa katika ulingo wa muziki wa Injili. Alishirikiana na msanii Justina Syokau kuimba ‘Mfalme wa Amani’ na kibao hicho kikawachochea kufyatua wimbo ‘One Miracle’ mwanzoni mwa 2022.

Sasha Kenya wakati wa mahojiano. Yeye ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, mshairi shupavu, mwigizaji stadi, mjasiriamali na muuguzi nchini Amerika. PICHA | CHRIS ADUNGO

Mbali na kutumia muziki kueneza Ukristo na kupigia Kiswahili chapuo, kubwa zaidi katika maazimio ya Sasha ni kusaidia wasiojiweza katika jamii, kuwa mlezi wa vipaji miongoni mwa vijana pamoja na kupiga vita ndoa za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake.

Mwimbaji huyu amejaliwa mtoto wa kike, Tracy Muchiti. Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika ulingo wa muziki ni kumtanguliza Mungu, kujiamini na kujituma.

“Hakuna kitu cha maana ambacho sisi binadamu tunaweza kufanya na tukafanikiwa bila kumtegemea Mola,” anasema.

You can share this post!

SGR: Jinsi Wachina walivyozima Uhuru

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya...

T L