• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 1:42 PM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kenyatta (Mahiga), Nyeri

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kenyatta (Mahiga), Nyeri

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kenyatta (Mahiga) katika eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri kiliasisiwa Oktoba 2019 kwa lengo la kupiga jeki juhudi za Idara ya Kiswahili na kuboresha matokeo ya KCSE.

Madhumuni mengine makuu ya chama hiki almaarufu CHAKIKEMA, ni kustawisha matumizi ya lugha miongoni mwa wanafunzi na kupanua mawanda ya elimu katika nyanja zinazofungamana na Kiswahili.

Kwa kushirikiana na vyama vingine shuleni, CHAKIKEMA kipo mstari wa mbele kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kuwaamshia wanafunzi hamu ya kuchapukia sanaa za uigizaji, ulumbi na uandishi wa kazi bunilizi.

Chama kwa sasa kipo chini ya ulezi wa Bw Philip Kinyanjui anayeshirikiana kwa karibu na Bw Eliud Ngotho, Bw Karanja, Bi Wanjii na Bi Mote ambao ni walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Upili ya Kenyatta (Mahiga), eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri. PICHA | CHRIS ADUNGO

Mwalimu Mkuu, Bw Charles Wachira, naye amejitolea kwa hali na mali kufaulisha mikakati ya chama kwa kuhakikisha kwamba kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili katika maktaba.

Usomaji wa mara kwa mara wa magazeti ya ‘Taifa Leo’ kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaosimamiwa sasa na CHAKIKEMA, pia umeimarisha matokeo ya Kiswahili na kuinua viwango vya kuthaminiwa kwa somo hilo miongoni mwa wanafunzi.

Wanachama huandaa vikao vya mara kwa mara ili kuendesha mijadala inayochangia makuzi ya Kiswahili, kuandika insha na kuzamia mada zinazowatatiza madarasani chini ya uelekezi wa viongozi wao – Timothy Weru (Mwenyekiti), David Hare (Naibu Mwenyekiti), Kelvin Otieno (Katibu) na Jackson Njoku (Mhazini).

Kikiongozwa na kaulimbiu ‘Penye nia pana njia’, CHAKIKEMA sasa ni jukwaa mwafaka la kuwaondolewa wanafunzi dhana potovu kwamba Kiswahili ni somo gumu. Chama hiki kimebadilisha mtazamo hasi miongoni mwa wanafunzi kuhusu Kiswahili na wameanza kuionea fahari lugha hii badala ya kuibeza.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Sasha Kenya

NGUVU ZA HOJA: Sababu ya Mswahili kuhusishwa na ulaghai

T L