• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
PAUKWA: Fantasia inavyokuza ubunifu wa watoto

PAUKWA: Fantasia inavyokuza ubunifu wa watoto

Na ENOCK NYARIKI

UDHAIFU mmoja unaotokana na mifumo ya elimu ni kusisitiza mno uhalisia katika uandishi hasa ule unaolenga watoto.

Dhana inayoshikiliwa na baadhi ya wadau wa elimu ni kuwa ndani ya uhalisia hujitokeza ubunifu.

Ingawa mawazo hayo yana ukweli kiasi fulani, ni muhimu kufahamu kuwa ubunifu hupaliliwa kwa muda mrefu na hauji kwa kulazimishiwa.

Lugha ni malighafi muhimu katika kuchochea ubunifu. Analojia inayozunguka sanaa nyingine itasaidia katika kuelewa umuhimu wa lugha.

Mchongaji vinyago, kwa mfano, huhitaji malighafi ya kutosha ili kuibuka na michongo inayovutia na inayokidhi mahitaji ya soko.

Malighafi yasipotosha au yakiwa ya kutumiwa kwa akali ndogo na kwa kubania, michongo itakosa thamani inayohitajika.

Kwa hivyo, ili kufikia ubunifu, sharti pawepo njia ya kuchochea stadi za kusoma na kusikiliza.

Ni muhimu kuwaandikia na kuwasimulia watoto kile wanachopenda bali si kile ambacho watu wanapenda.

Fantasia huwavutia watoto. Vyombo vya habari kwa mfano idhaa ya Kiswahili ya KBC na gazeti la Taifa Leo vimekuwa vikitumia fantasia kwa ufaafu kuwafikia watoto.

‘Hadithi za kale’ na ‘Hadithi za Kiwetu’ zilizoandaliwa na KBC ni mfano mzuri wa masimulizi ya kifantasia yaliyosaidia katika kupokea malighafi ya lugha.

Gazeti la Taifa Leo nalo limekuwa na mchango muhimu sana katika kuitumia fantasia kuwafikia watoto kupitia matumizi ya vibonzo na michoro ya rangi.

Mbinu hii imekuwa ikitumiwa tangu enzi ya vibonzo vya ‘Juha Kalulu’ hadi kizazi cha sasa cha akina IGAH na Wycotie.

Alhasili, katika kuwasaidia watoto kuipenda lugha ya Kiswahili, dhima ya kuburudisha sharti ije kwanza ikifuatwa na dhima nyingine.

You can share this post!

TALANTA YANGU: Yvonne ni Lupita anayeinukia

PAA yajipanga kudhibiti kaunti kura za Agosti

T L