• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
TALANTA YANGU: Yvonne ni Lupita anayeinukia

TALANTA YANGU: Yvonne ni Lupita anayeinukia

Na CHRIS ADUNGO

KUBWA zaidi katika matamanio ya Yvonne Adego Mwashe, 11, ni kutikisa ulingo wa sanaa ya uigizaji na kufikia kiwango cha staa wa filamu za Hollywood aliyeshinda tuzo ya hadhi ya Oscar mnamo 2014, Lupita Nyong’o.

Zaidi ya kuwa lulu katika fani ya uigizaji, mwanafunzi huyu wa darasa la sita katika Shule ya Light International Mombasa analenga pia kuwa mchezaji maarufu wa sataranji (chess) na kumfikia bingwa mara tano wa dunia katika mchezo huo, Magnus Carlsen kutoka Norway.

Miongoni mwa watu wanaozidi kuweka hai ndoto hizi za Yvonne ni mama yake mzazi, Bi Judith Karigu Kiragu.

“Kipaji cha uigizaji kilitambulika ndani ya Yvonne akiwa mtoto mdogo. Japo alipenda sana uimbaji na uchoraji, alivutiwa pia na sataranji. Alitia azma ya kutononoa talanta zake, nasi wazazi tukashirikiana na walimu kumpa majukwaa mwafaka azipalilie,” akatanguliza Bi Kiragu.

“Alianza masomo shuleni tayari akifahamu thamani ya michezo na sanaa ya uigizaji. Alipenda kupigwa picha na alihamu kuonekana kwenye runinga siku moja. Sasa anapendelea Hisabati, Kiingereza, Sayansi na Muziki. Anavutiwa pia na masomo yanayoegemea sanaa na mawasiliano. Huenda akawa mwanahabari!” akasema.

Weledi wa Yvonne katika sataranji uliwahi kumpa fursa ya kuwakilisha Kenya katika michezo ya African Youth Chess Championships nchini Ghana mnamo Septemba 2021.

Amewahi pia kushiriki mapambano ya World Youth Rapid Chess Championships mnamo Agosti 2021, miezi mitatu kabla ya kunogesha kipute cha African Schools Individual Chess Championships jijini Nairobi.

Ilikuwa Januari 2020 kwenye hafla ya kuhamasisha vijana katika eneo la Tharaka Nithi kutambua na kutumikisha vipaji vyao ambapo Yvonne alipata fursa iliyomwamshia hamu ya uigizaji. Alishiriki filamu ambapo yeye ndiye alikuwa msichana wa pekee katika darasa lililojaa wanafunzi wa kiume.

Yvonne, aliigiza mhusika mkuu, Mukami, katika filamu hiyo inayotiwa ladha na sataranji – mchezo unaohitaji akili pevu ili kumpiku mpinzani. Ingawa kwa kawaida ni mpole na mnyamavu, Yvonne ana ukakamavu wa kuajabiwa. Uwezo wake katika sanaa ya ulumbi hupigwa jeki na umilisi mkubwa wa Kiingereza na Kiswahili.

Uwezo

“Yvonne ana ujuzi wa kuzitendea haki nafasi za kuigiza anazopewa jukwaani. Alijiunga na Chama cha Drama shuleni muhula uliopita na amepata umaarufu miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake. Inatia moyo kwamba anazidi kutambulika kimataifa,” anasema Bi Vincencia Denge Nyaminde ambaye ni mwalimu wa Yvonne shuleni Light International, Mombasa.

You can share this post!

EPL: Chelsea yapiga Spurs kwa mara ya tatu chini ya wiki...

PAUKWA: Fantasia inavyokuza ubunifu wa watoto

T L