• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
#KUMEKUCHA: Shabiki wa Taifa Leo Mzee Paulo Mwanyalo akumbuka sehemu ya Kibogoyo ilivyomburudisha

#KUMEKUCHA: Shabiki wa Taifa Leo Mzee Paulo Mwanyalo akumbuka sehemu ya Kibogoyo ilivyomburudisha

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

AMEKUWA msomaji wa Taifa Leo tangu lianzishwe mwaka 1958 yeye mwenyewe akiwa na umri wa miaka 23.

“Tangu Taifa litoke mitaani, nimekuwa sikosi nakala yangu isipokuwa siku chache mno ambazo gazeti hilo halikuwa likifika nilipokuwa nikiishi Wundanyi na hata nilipohamia huku Taveta,” amesema Mzee Paulo Mwanayalo.

Mwanyalo anayeishi kijiji cha Kimorigo, wadi ya Mboghoni, Kaunti Ndogo ya Taveta anasema amekuwa shabiki mkubwa wa gazeti la Taifa Leo tangu libuniwe na hadi sasa anaendelea kulisoma na hapendi kukosa kulinunua hata siku moja.

Alipoulizwa ni sababu gani hasa iliyomfanya apendezwe kulisoma gazeti hili, Mwanyalo alisema alipokuwa kijana, elimu yake ya lugha ya Kiswahili ilikuwa duni, hivyo Taifa lilimsaidia pakubwa kuelewa lugha hiyo.

“Mbali na kujifunza lugha ya Kiswahili kwa kusoma Taifa, pia nilifahamu mengi juu ya siasa za nchi inavyoendelea na mambo gani yanayofanyika nchini Kenya pamoja na sehemu zote za dunia,” akasema msomi huyo maarufu wa jarida hili.

Akiongea juu ya ubora wa gazeti hili, Mwanyalo alisema anavutiwa mno na Taifa Leo kutokana na mvutio wa kurasa zake zote, Kiswahili cha mafunzo kinachotumika, ufahamu wa lugha wa waandishi wake na makala pamoja na habari kem kem za siasa, utamaduni na michezo.

“Hapo zamani, nilikuwa nikipendelea mno kusoma makala ya wanasiasa wa hapa nchini, wa sehemu nyingine za Afrika na ulimwengu,” akasema jagina huyo ambaye anajivunia hadi sasa anaweza kusoma gazeti hili alipendalo bila ya kutumia miwani.

Mwanyalo ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 86 amewaomba wakuu wa Taifa warudishe sehemu ya Kibogoyo ya kujibu maswali ya wasomaji. “Hakika, wasomaji walikuwa wakiuliza  maswali mazuri na Kibogoyo akijibu majibu mazuri na mengine ya kuchekesha!” akasema.

Alisema angelifurahikia pia kama sehemu ya Nyota Zenu itarudishwa katika gazeti hili kwani anaamini wasomaji wengi walikuwa wakipenda kusoma kujua nyota zao. “Mimi binafsi nilikuwa sikosi kusoma nyota yangu kila siku,” akasema.

Mzee Mwanyalo anataka makala ya Majimbo yarudishwe ili Wakenya wafahamu juu ya majimbo mbalimbali, watambue desturi na mila ya majimbo hayo na ni watu wa makabila gani wanaoishi huko. PICHA/ ABDULRAHMAN SHERIFF

Mzee Mwanyalo anataka makala ya Majimbo yarudishwe ili Wakenya wafahamu juu ya majimbo mbalimbali, watambue desturi na mila ya majimbo hayo na ni watu wa makabila gani wanaoishi huko.

Katika makala hayo, angelipendelea zaidi ikufahamu jinsi makabila yaliyokuwako kwenye majimbo hayo na kuekleza habari za jinsi watu wa sehemu hizo walivyokuja kuishi kwenye majimbo hayo.

“Ni vizuri tufahamu na kuelimishwa jinsi kabila ama makabila fulani yalivyofika kwenye jimbo hilo, jinsi wanavyoishi, mila na desturi zao nakadhalika,” akasema.

Mwanyalo alilalamika ukosefu wa Ukurasa wa WAKITA ambao anasema una umuhimu kwa wasomaji wote wa gazeti hilo ambao wanajifunza mengi juu ya lugha ya Kiswahili.

Jagina huyo ambaye anasema si shabiki wa michezo, anataka gazeti hili lifahmishe kizazi cha wakati huu juu ya historia za wanasiasa wakongwe wa jimbo hili la Pwani ambao walitoa huduma bora kwa watu wao.

Aliwataja baadhi ya wanasiasa hao kuwa kina marehemu Ronald Gideon Ngala, Robert Matano, Shariff Nassir, Maalim Bakuli, Emmanuel Karisa Maitha, Danson Mwanyumba, Darius Mbela, Eliud Mwamunga, Osnel Mnene na Mwacharo Kubo kati ya wengine kadhaa.

“Katika makala hayo, wanasiasa hao waelezwe walitoka sehemu gani, walikuwa na vyeo gani, wametekeleza miradi gani na wameitumikia nini jimbo la Pwani na nchi ya Kenya kwa ujumla,” akasema Mwanyalo.

Alipendekeza mambo kadhaa ya kulitaka gazeti hili litekeleze ili kurudisha umaarufu wake wa kale pamoja na kuvutia wasomaji wengi zaidi. Kati ya mapendekezo yake ni pamoja na kutaka kurasa zake zirudi kama zilivyokuwa hapo awali ama ziongezwe zaidi.

Pia anapendelea kila mara kuwe na mashindano ya Insha sio kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari bali pia kwa wasomaji na akataka kuweko na siku maalum ya kuzungumziwa shule za Pwani zenye historia ya kuwako miaka mingi iliyopita, zikiwemo zile tangu enzi ya ukoloni.

Mwanyalo amependekeza kuwa badala ya kuwepo kwa Vituko vya Pokoyoyo, nafasi hiyo itumike kwa kuwekwa Nyota ambazo zinavutia wasomaji wengi zaidi.

Mwanyalo anaishi kijijini hapo Kimorigo pamoja na mkewe Dorcas Pili Mwanyalo, mtoto wake wa pili, Mariam Mashindano na mwanawe wa tatu Michael Mkirema Mwanyalo hali wanawe wengine, Elina Mwanyalo na Mary Paul wanaishi Mombasa na Daniel Sholo Mwanyalo yuko Wundanyi.

Mzee Mwanyalo anasema kuwa yeye hupendelea kutumia chakula wanacholima shambani mwao hapo kijijini Kimorigo. “Napenda zaid kula chakula kinachotoka shamba letu na hasa ugali, malinge, mihogo na ndizi,” akasema.       

MwanayeMichael Mkirema anasema baba yake huwa na hamu ya kunywa chai mara baada ya kupokea nakala yake ya gazeti la Taifa Leo. “Wakati wote wa asubuhi, baba huwa anapiga simu kujulia kama magazeti yamefika mjini Taveta ili amtume mwenye bodaboda kumnunulia,” akasema Mkirema.

Anasema siku ambazo gazeti linachelewa kufika ama kutofika kabisa, huwa ni siku ya majonzi makubwa kwa baba yetu. “Asubuhi akiamka baba Mwanyalo hana lugha nyingine isipokuwa lugha ya kufahamu kama gazeti limefika na anapolipata, huwa furahani,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 26 wateketea madarasa yaliposhika moto

Wasichana matineja katika hatari – ripoti

T L