• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Sherehe kufana miji ya ndani na nje ya Kenya

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Sherehe kufana miji ya ndani na nje ya Kenya

Na CHRIS ADUNGO

KILELE cha maadhimisho ya pili ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU) kitashuhudiwa leo Ijumaa jijini Nairobi na Mombasa, wadau watakapodhihirisha lugha hii ilivyo sehemu muhimu ya tamaduni na taratibu za maisha ya kila siku ya Waswahili – asili, wazawa na waridhiwa wanaoelewana kilahaja.

“Maadhimisho haya yatatoa fursa kwa wapenzi wa lugha kujadiliana zaidi kuhusu mikakati ya kuimarisha matumizi ya Kiswahili na wito kutolewa kwa vyuo vikuu kuweka misingi ya kufundisha lugha hii kwa hadhi na viwango vitakavyokabiliana na kasi ya ukuaji wake,” anasema Mhariri Mkuu wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Prof Mark Mosol Kandagor.

Tofauti na mwaka jana ambapo asasi mbalimbali za kielimu – hasa vyuo vikuu – zilijiendeshea maadhimisho ya kwanza ya SIKIDU katika viwango vyao binafsi, Serikali Kuu mara mara hii ilijichukulia usukani wa maandalizi na imekuwa mstari wa mbele kufanikisha mipangilio yote.

Wizara ya Masuala ya Kigeni itakuwa leo Ijumaa na hafla yake katika mkahawa wa QMins ulio mkabala na Bomas jijini Nairobi huku Idara ya Utamaduni na Turathi katika Wizara ya Utalii, Wanyamapori na Turathi za Kitaifa ikishirikiana na Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuendesha sherehe nyingine eneo la Fort Jesus Park (Swahili Centre na Swahili Pothub), NMKHTI Grounds, Mombasa.

Hafla ya Mombasa itaanza kwa matembezi ya saa mbili kutoka Uhuru Gardens hadi Fort Jesus. Matembezi hayo yataanzishwa na Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Turathi za Kitaifa, Bi Penina Malonza, kwa ushirikiano na Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir.

Wakazi wa Mombasa watahamasishwa kuhusu jinsi ya kubidhaaisha Kiswahili na nafasi ya lugha hii katika soko la ajira duniani.

Wataburudishwa kwa nyimbo, mashairi, maonyesho ya vyombo vya kitamaduni, vyakula, tamasha za ngoma za kiasili, midahalo, tamasha za vijana na mashindano ya aina mbalimbali.

“Lengo letu ni kueleza taifa na ulimwengu kuhusu hatua kubwa ambazo Kiswahili kimepiga katika sekta nyingi. Zaidi ya kufundishwa kimataifa, ndiyo lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kutengewa siku maalumu ya kuadhimishwa,” akasema Prof Clara Momanyi.

“Katika siku hii, ni muhimu tuketi pamoja na kuchangamkia Kiswahili si tu kwa maandishi na mazungumzo, bali kupitia utajiri wa utamaduni wetu na kumbukumbu za matendo ya magwiji waliotutangulia ili sauti zao na zetu zitande kote ulimwenguni,” akaongezea.

Upekee wa sherehe hizo za Mombasa zitakazoendelea hadi Julai 9 ni kwamba zitafanyika katika mazingira yaliyo na wazungumzaji asilia wa Kiswahili.

Hivyo, washiriki watajifunza mengi kuhusu utamaduni wa Waswahili kuanzia kwa vyakula, miti-shamba, mavazi, mapambo, mashairi, maigizo, hotuba, densi na ngoma za kiasili pamoja na vifaa wanavyovitumia kufanyia shughuli mbalimbali.

Kwa mtazamo wa Prof Kandagor, huenda maadhimisho ya leo Ijumaa yakachochea serikali kufichua kipindi mahsusi inapokusudia kuunda Baraza la Kiswahili la Kenya litakalokuwa na jukumu la kuandaa maadhimisho yajayo ya SIKIDU kwa hadhi inayostahiki na utaratibu bora zaidi.

“Maadhimisho ya aina hii yanakusudia kutumbusha kuwa Kiswahili ni zaidi ya lugha ya mawasiliano na kwamba ni kielelezo cha utamaduni na utambulisho wetu,” anaelezea.

Kuanzia Jumanne, wapenzi wa Kiswahili kutoka dayaspora (mataifa ya kigeni) waliandaa warsha iliyowapa fursa ya kutafakari kuhusu haja ya kuhakikisha kuwa hawawi nyuma katika safari ya kuijengea lugha hii majukwaa zaidi ya kukuzwa kimataifa. Maadhimisho ya QMins yatanogeshwa na kuwepo kwa John Kinyua (Seneta wa Laikipia), Yusuf Hassan (Mbunge wa Kamukunji), Leonard Mambo Mbotela (mtangazaji) na Dkt Hubert Gijzen (Mkurugenzi wa Kikanda, UNESCO).

Kauli za ufunguzi zitatolewa na Balozi Ann Wanjohi (Mkurugenzi, Kitengo cha Diplomasia ya Utamaduni), Balozi Washington Oloo (Mkurugenzi, Masuala ya Diaspora) na Bi Rosaline Njogu (Katibu, Masuala ya Diaspora).

Prof Kithaka Wa Mberia, Prof Leonard Muaka na Makamu Rais wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), Prof Iribe Mwangi, watawakilisha wasomi na wataalamu wa Kiswahili huku Prof Kimani Njogu akiongoza hafla ya kuzinduliwa rasmi kwa programu ya Kiswahili na kitabu chenye makala ya kitaaluma kutoka kwa baadhi ya wasomi wa Kiswahili.

Mbali na mada kuu, ‘Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Utangamano’, mada nyinginezo zitakazojadiliwa ni ‘Kiswahili: Tulikotoka, tulipo na tunapofaa kwenda’ (Prof Kandagor), ‘Kiswahili: Uzalendo na Utaifa’ (Wallah Bin Wallah) na ‘Nafasi ya Kiswahili katika Elimu na Utafiti’ (Dkt Assumpta Matei).

  • Tags

You can share this post!

Mjane akimbilia mahakama kunusuru kipande cha ardhi

Kibarua cha Raila Sabasaba ikiwadia

T L