• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kibarua cha Raila Sabasaba ikiwadia

Kibarua cha Raila Sabasaba ikiwadia

NA BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya unaoongozwa na Raila Odinga unakabiliwa na kibarua kigumu kufanikisha maandamano yaliyopangwa kufanyika leo Ijumaa kote nchini baada ya serikali kuyaharamisha.

Muungano huo wa Upinzani unasisitiza kuwa utaandaa maandamano katika barabara za jiji la Nairobi na miji mingine kote nchini kulalamikia hatua ya serikali ya kuongeza ushuru kupitia Sheria ya Fedha 2023 ikiwemo ya Hazina ya Nyumba.

Bw Odinga ametangaza kuwa muungano huo utaandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi kabla ya kuandamana kuadhimisha siku ya Sabasaba.

Siku hiyo ilitumiwa na waliopigania demokrasia ya vyama vingi kushinikiza serikali ya Kanu kufuta kifungu 2A cha katiba ya zamani kilichofanya Kenya kuwa ya chama kimoja cha kisiasa.

Hata hivyo, polisi wanasema wameruhusu mkutano wa Kamukunji pekee kufanyika wala hawataruhusu maandamano yoyote jijini. Msimamo wa polisi unaweka Azimio katika hali sawa Februari ambapo wafuasi wake walizuiwa kukusanyika katikati ya jiji.

Polisi walivunja misafara ya wafuasi wa Upinzani katika mitaa ya Kibera, Mathare, Eastleigh, Kawangware, na Mukuru kwa Njenja kwa kutumia vitoa machozi.

Viongozi wa serikali ya Kenya Kwanza pia wamekuwa wakionya kwamba hawatakubali maandamano jijini wakilaumu upinzani kwa kuwa na nia ya kutaka kuharibu mali na kuvuruga uchumi.

Mnamo Juni 19, Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki alionya wanasiasa wasioridhishwa na Sheria ya Fedha 2023 kutumia mchakato wa kisheria kupitia Mahakama akisema serikali haitaruhusu maandamano.

“Hatutakubali maandamano barabarani, uharibifu wa mali ya watu na biashara au kufunga barabara. Tofauti zikizuka kuhusu suala lolote, liwe la kisiasa, kiuchumi au kijamii, ni lazima kama nchi tujifunze kutumia njia za kidemokrasia na taasisi kuzitatua,” waziri Kindiki alionya.

Muungano wa Azimio ambao unatarajia kutumia kupanda kwa gharama ya maisha baada ya kuongezwa kwa ushuru kupitia Sheria ya Fedha ya 2023, umetangaza kuwa kutakuwa na mikutano na maandamano kote nchini.

Azimio inasisitiza mikutano na maandamamo ya leo ni mwanzo wa awamu mpya ya uasi dhidi ya serikali na wafuasi wao watakusanya saini kuondoa mamlaka waliyokabidhi viongozi wakiwemo wabunge waliopitisha sheria hiyo.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei jana Alhamisi alionya kuwa serikali haitaruhusu mikutano haramu isipokuwa katika uwanja wa Kamukunji.

“Ninaweza kusema kuwa Azimio ilifuata mchakato wa sheria kuandaa mkutano katika uwanja wa Kamukunji na tunataka kufahamisha umma kwamba waliomba kibali cha mkutano na sio maandamano ambayo watu wanazungumzia,” Bw Bungei alisema.

Hata hivyo, imeibuka kuwa viongozi wa Azimio wana mkakati mkali watakaotumia kufanikisha mikutano ya maeneo bunge.

Duru za ndani zilisema vinara wakuu wa muungano huo wakiongozwa na Bw Odinga, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Narc Kenya Martha Karua, Eugene Wamalwa wa DAP- Kenya, katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, George Wajackoya na aliyekuwa gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria walikutana Alhamisi na kukubaliana miji ambayo itatumiwa kwa awamu “kali ya maandamano” dhidi ya serikali.

Baadhi ya miji ni Nakuru, Thika, Kirinyaga, Laikipia, Kakamega, Vihiga, Busia, Narok, Kisumu, Kisii, Siaya, Migori na Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Sherehe kufana miji ya ndani na...

Mzozo wa madiwani na SRC kutatiza shughuli muhimu

T L