• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee Lamu

Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee Lamu

NA KALUME KAZUNGU

SIKU ya Kiswahili Duniani imeadhimishwa kwa njia ya kipekee kisiwani Lamu ambapo wataalamu wa lugha hiyo, malenga, wacheza ngoma, wanamuziki, walimu na wadau wengine wamejumuika kwenye warsha ya kujadili na kuitukuza lugha hiyo inayoendelea kupanuka kwenye nchi nyingi za Bara Afrika na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Maafisa wa Muungano wa Vijana wa Lamu Youth Alliance (LYA) kwa ushirikiano na Halmashauri ya Makavazi na Turathi nchini (NMK) wameshirikiana kuandaa warsha na tumbuizo hizo zilizofanyika kwenye uga wa Mkunguni na pia ndani ya jumba la Lamu Fort.

Wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na za upili pia wamejumuika na kuipamba siku hiyo kwa mashairi, nyimbo na ulumbi miongoni mwa mawasilisho mengine.

Ilikuwa ni siku iliyomeremeta kwelikweli.

Siku ya Kimataifa ya Kiswahili huadhimishwa Julai 7 kila mwaka.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Afisa Msimamizi wa Turathi na Makavazi (NMK) tawi la Lamu, Mohammed Ali Mwenje amesifu jinsi lugha ya Kiswahili inavyozidi kupanua mawanda yake na kutumiwa na watu wengi zaidi duniani.

Takwimu zinaonyesha kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ambapo ni karibu wazungumzaji 200 milioni kwa sasa.

Bw Mwenje aidha amesema huku Kiswahili kikitukuzwa, pia ipo haja ya lahaja za asili za lugha kuhifadhiwa, kupitia maandishi kwenye madaftari ili kuzikinga zisiangamie.

Ametaja lahaja kuu nne za Lamu kama vile KiAmu, KiPate, Kitikuu na Kisiu kuwa kwenye hatari ya kumezwa na hata kupotea kabisa ikiwa hakutakuwa na mpango wa kuhifadhi lahaja hizo kwenye madaftari.

“Nashukuru kwamba leo twajivunia kuzungumza Kiswahili. Ni lugha inayoenziwa kwani imesaidia kuunganisha watu duniani kijamii, kiuchumi na biashara na mengineyo. Pia ni vyema kukumbuka kuwa tuko na lahaja zetu. Ikiwa kutakosekana mpangilio utakaohakikisha lahaja zetu zinahifadhiwa, basi huenda tukazipoteza,” akasema Bw Mwenje.

Afisa Mkuu Mtendaji wa muungano wa vijana wa Lamu Youth Alliance, Ahmed Walid ametaja lugha ya Kiswahili kama kitambulisho cha baadhi ya watu na maeneo yao.

Bw Walid amesema kukipoteza au kukiharibu Kiswahili ni sawa na kupoteza chimbuko la watu fulani.

“Sisi watu wa mwambao wa Pwani, hasa Lamu, twajiita Waswahili kutokana na jinsi tunavyoizungumza lugha hii. Kumaanisha endapo lugha itaborongwa, basi jamii nzima ya Uswahilini pia itachukuliwa kuwa imeyumba. Tutazidi kushikana kukikuza na kukiendeleza Kiswahili,” akasema Bw Walid.

Malenga tajika wa Kisiwa cha Lamu, Hashim Said Mohamed, maarufu DJ Fakhrudin amesema furaka yake ni kuona kila kabila, jamii, nchi, mabara na ulimwengu mzima ukikumbatia Kiswahili.

Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mnamo Ijumaa, DJ Fakhrudin amejitolea kughani mashairi mitaani, vichochoroni na vishorobani mwa mji wa Kale wa Lamu.

Mashairi hayo yamekuwa na maudhui yanayohusu kukikuza, kukienzi na kukitukuza Kiswahili.

“Mimi kama malenga tajika na mwanafalsafa wa lugha ya Kiswahili nchini na Afrika Mashariki, nitawasisitizia wakazi wa Lamu, Wakenya wote na ulimwengu kwa ujumla kwamba Kiswahili ndiyo mambo yote. Ni jukumu letu kukiendeleza,” akasema Dj Fakhrudin.

Maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani ni mafanikio yaliyopatikana baada ya uamuzi kuafikiwa kwenye kikao cha 41 cha mkutano wa nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (UNESCO) 2021.

Ni hapo ndipo tangazo lililotolewa kwamba Julai 7 kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa Gatanga atoa onyo sharti Del Monte igawe ekari 2,...

Maandamano ya Azimio yalivyosambaa Saba Saba

T L