• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Maandamano ya Azimio yalivyosambaa Saba Saba

Maandamano ya Azimio yalivyosambaa Saba Saba

NA WAANDISHI WETU

UASI dhidi ya serikali jana Ijumaa ulionekana kuenea huku maandamano yaliyoendelezwa na Upinzani yakishamiri na kukwamisha shughuli katika maeneo mengi nchini.

Kinyume na hapo awali ambapo maandamano hayo yamekuwa yakifanyika majijini Nairobi na Kisumu ambayo ni ngome za kisiasa za Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga, jana Ijumaa shughuli hiyo ilishika kasi hata katika miji ambayo hujiepusha na maandamano.

Bw Odinga aliongoza maandamano hayo Nairobi na kuwahutubia wafuasi wake katika uwanja wa kihistoria wa Kamkunji ambako alitangaza kuwa yatafanyika tena Jumatano ijayo.

Wafuasi wa upinzani walifurika barabarani kwa wingi katika miji mbalimbali wakilalamikia gharama ya juu ya maisha, baadhi wakimshambulia kwa maneno makali Rais William Ruto kwa kutotimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Mbali na Nairobi na Kisumu, maandamano hayo pia yalifanyika Mombasa, Kisii, Nyandarua, Kakamega, Machakos, Kirinyaga, Turkana na Nyandarua.

Wakati wa maandamano hayo, baadhi ya wafuasi wa upinzani walikamatwa na kusukumwa kwenye karandinga.

Jijini Nairobi biashara zilifungwa huku Bw Raila na wanasiasa wengine wa Upinzani wakiandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji.

Mkutano wa Bw Raila ulihudhuriwa na halaiki ya raia ila makabiliano makali yalizuka kati ya wafuasi wake na maafisa wa polisi, msafara wa Bw Odinga ulipojaribu kuingia jijini kupitia Kariokor na Gikomba baada ya hafla hiyo.

Polisi walitumia vitoa machozi na kufyatua risasi hewani kuwazuia wafuasi hao kuingia katikati ya jiji huku maduka mengi yakifungwa Gikomba ambako kwa kawaida huwa imesheheni shughuli za kibiashara.

Katikati ya jiji la Nairobi pia na wingu la moshi wa vitoa machozi litanda huku baadhi ya wafuasi wa Upinzani wakikabiliana na polisi kijasiri.

Mjini Kisii, kuna wakati ambapo polisi waliishiwa na vitoa machozi.

Ilibidi wasaidiwe na wenzao kutoka Idara ya Magereza. Waandamanaji waliziba barabara nyingi za mji huo na kuwasha moto, huku polisi wakiwarushia vitoa machozi.

Baadhi ya waandamanaji waliburura jeneza lililokuwa na picha ya Rais William Ruto kama njia ya kumlaani, wakidai uongozi wake ndio chanzo cha uchumi mgumu .

Mjini Mombasa, wabunge Rashid Bedzimba (Kisauni), Mohamed Machele (Mvita) na Bady Twalib waliungana na waandamanaji kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na kupandishwa kwa ushuru.

Hali ilikuwa vivyo hivyo katika miji ya Kakamega, Mumias na Kisumu, waandamanaji wakifukuzana na polisi.

Vijana katika kituo cha biashara cha Shinyalu ambao walikuwa kwenye bodaboda walikabiliana vikali na polisi. Naibu kiongozi wa ODM, Bw Wycliffe Oparanya, aliye pia gavana wa zamani, aliongoza maandamano ya Mumias alikozindua mchakato wa kukusanya saini za kutaka kuondoa utawala wa sasa mamlakani. Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Narc Kenya Martha Karua pia waliongoza maandamano katika kaunti za Machakos na Kirinyaga mtawalia. Mbunge Robert Mbui wa Kathiani aliwashaajisha wananchi washiriki mchakato wa kukusanya saini za kumwondoa Rais Ruto mamlakani kwa kuwa hilo litarahisisha Bw Musyoka kuingia mamlakani.

Aliyekuwa Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi na aliyekuwa mwaniaji wa ubunge wa Laikipia Mashariki kupitia Jubilee Sarolyne Mwendia walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Nyahururu kwa kuandaa maandamano mjini humo.

Ripoti za Cecil Odongo, Wycliffe Nyaberi, Sammy Kimatu, Ruth Mbula, Pius Maundu, George Munene Winnie Atieno, Sammy Luta, Eric Matara na Isaac Wale

  • Tags

You can share this post!

Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee...

Koth Biro: Leads United watuma salamu kwa wapinzani wao

T L