• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Mbunge wa Gatanga atoa onyo sharti Del Monte igawe ekari 2, 000 za shamba kwa raia

Mbunge wa Gatanga atoa onyo sharti Del Monte igawe ekari 2, 000 za shamba kwa raia

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Gatanga Bw Edward Muriu ameonya kampuni ya Amerika ya Del Monte inayomiliki zaidi ya ekari 30, 000 za shamba kuwa ni lazima itenge ekari 2, 000 kwa wakazi ili wazigawane.

Kampuni hiyo hukuza mananasi na kuandaa juisi maarufu ya Del Monte, lakini katika siku za hivi karibuni imezindua kilimo cha macadamia.

Aidha, Bw Muriu alionya Gavana wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata akome mbio za kutwaa ekari 1, 400 kutoka kwa kampuni hiyo akidai anataka kujenga hospitali na soko.

“Ni uamuzi wa mahakama kwamba kampuni ya Del Monte itenge ekari 3, 400 kwa wenyeji wa Murang’a na zingine 600 kwa wenyeji wa Kaunti ya Kiambu. Hapa Murang’a, serikali ya Kaunti inakimbia kutwaa ekari 1, 400 na kusahau kwamba hata haijawahi kushiriki vita vya kupata ugavi huo,” mbunge huyo akasema.

Alisema kwamba wakazi wa Kandara na Gatanga ndio wamekuwa wakipigania shamba hilo ligawie wenyeji, huku serikali ya kaunti ikiwa shabiki tu.

“Katika mbio zake za kuanza kunufaika na matokeo ya vita vya raia, serikali ya kaunti ichunge asituingize kwa shida nyingine hapa.

“Tushirikishe harakati hizi kwa mpangilio. Ikipata ekari zake za kustawisha kwa miradi ya umma, isisahau kuwa hilo halitawezekana kabla raia wapate ekari zao 2, 000,” akasema.

Bw Muriu alisema kwamba “tunataka shamba la umma litenganishwe na lile la Kaunti. Ekari 2, 000 ziwekwe kando ili wapiga kura wa Gatanga na Kandara wakae chini waamue jinsi watakavyoligawana”.

Bw Muriu alisema kwamba ni jukumu la watu wa maeneo bunge hayo mawili kuamua jinsi watakavyogawana ikizingatiwa kuwa kuna zaidi ya wapiga kura 200, 000.

“Cha kutujalisha kwa sasa ni jinsi shamba hilo kwanza litapatikana. Tukipewa, sisi kama viongozi tutashirikisha harakati za ugavi. Ikiwa watapiga kura ya kugawana, ikiwa wataamua kulilima au kuliuza wagawane pesa…Hiyo haitakuwa shida,” akasema.

 

[email protected]

 

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Saba Saba: Raila Odinga amtaka Rais Ruto kukoma...

Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee...

T L