• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
UCHAMBUZI WA FASIHI: Wahusika, maudhui na vitushi: Sura ya Sita ya Chozi la Heri

UCHAMBUZI WA FASIHI: Wahusika, maudhui na vitushi: Sura ya Sita ya Chozi la Heri

Na JOYCE NEKESA

JUMA lililopita tuliangazia sura ya tano ya riwaya ya Chozi la Heri.

Umuhimu wa mandhari ya msitu wa Mamba uliangaziwa ambapo tuliona jinsi mandhari yalivyochangia kujenga maudhui, wahusika na ploti.

Leo tunaangazia sura ya sita ambapo mandhari ni katika shule ya Tangamano.

Wahusika wanaorejelewa hapa ni Umulkheri, Mwalimu Dhahabu, Lunga, Naomi, Sally, Billy, Sauna, Dick, Mwaliko, Askari katika kituo cha polisi, Hazina na Julida.

Umulkheri anashauriwa na mwalimu Dhahabu arejee darasani kwani alikuwa amesalia mawazoni.

Umu anasinywa na mazingira mageni ya shule ya Tangamano – baridi kali, kusomeshwa kugeni, walimu wageni, mbinu mpya za kufundishwa; hali ambayo Umu hakuzoea.

Umu ni kifungua mimba wa Lunga Kiriri-Kangata.

Alikuwa amejiunga na kidato cha kwanza wakati walipohamishiwa Mlima wa Simba.

Lunga alifadhaishwa na kuhamishwa kwake. Kipato chake kilikatika ghafla. Angali anakumbuka mashamba na mali yake iliyomfanya tajiri na kuishi maisha mazuri huku wanawe wakisomea shule za kifahari.

Fidia aliyopewa na serikali haikutosha kuyagharimia mahitaji yake.

Mkewe Naomi alikataa kuishi katika nyumba waliyojengewa na serikali katika eneo la Mlima wa Simba; akirejelea kisa cha Billy alivyokataliwa na Sally.

Anatoroka baada ya kumuandikia ujumbe mfupi wa simu kwamba ameenda kutamba na ulimwengu.

Lunga alihuzunika kwa kuachwa na mkewe na kutwikwa jukumu la kuwalea wanawe hadi akashikwa na wahka uliomsababishia kihoro na uwele wa shinikizo la damu.

Anaaga dunia na kuwaacha wanawe mikononi mwa kijakazi Sauna anayewateka nyara Dick aliyekuwa Darasa la Saba na Mwaliko Darasa la Kwanza na kumpelekea Bi Kangara aliyekuwa akiwalangua watoto.

Umu alibaki pweke na kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

Umu anakumbwa na mawazo mengi, anashangaa sababu ya Sauna kuisaliti familia yake licha ya kuwa mchangamfu na mtiifu.

Anamlaumu pia mamake kwa kutoroka na kuwaacha. Alipozidiwa na mawazo, alihama huku akiapa kulinda utu wake. Aliondoka Mlima wa Simba hadi jiji la Karaha kwa garimoshi.

Alikuwa amezuru jiji hilo mara kadhaa akiwa na wazazi wake kwenye gari lao. Hakuwahi kupata fursa ya kutembea huko kwa miguu.

Aliamua kuanzisha maisha mapya jijini. Ana nia ya kuwatafuta wahisani wampe makao. Anatumai kuwapata ndugu zake jijini. Umu anapofika mjini anaona njia ya Church Road, anakumbuka ziara yake humo na mamake siku moja.

Alikumbuka ombaomba waliohitaji msaada kwao na jinsi mamake alivyokataa kuwasaidia akidai kuwa hawaaminiki lakini Umu aliamua kumpa mmoja wao shilingi mia mbili.

Mvulana huyo aliapa kumsaidia siku moja.Alitumai kumpata mvulana huyo ili ampe makao angalau ya usiku huo.

Anapofika mbele ya mkahawa mkubwa uliokuwa mkabala na kanisa, aliona kundi kubwa la vijana wa mitaani, kisha akasikia mtu akimwita ‘kipusa’.

Alipogeuka akamwona ni yule ombaomba aliyemtarajia,amekuwa nadhifu na meno yake ni meupe,anajitambulisha kuwa yeye ni Hazina.

Alimuelezea Umu jinsi serikali ilivyomuondoa mtaani na kumpeleka shuleni.

Aliacha kuvuta gundi.

Wana makao mapya ambapo yeye na wenzake waliookolewa wanaishi na kupewa msaada.

Baadhi yao ni: maseremala, waashi na mafundi wa juakali, Hazina alijifunza upishi na huduma za hoteli.

Alimkaribisha Umu hotelini alimofanya kazi.

Umu anamsimulia Hazina yaliyomsibu.

Hazina alimpeleka walikoishi na kumjulisha kwa Julida, msimamizi wao.

Mama huyo alimhakikishia Umu kuwa Wizara ya Elimu ingefadhili masomo yake na kuwa serikali ingefanya kila iwezalo kuwasaka ndugu zake.

Alijiunga na Shule ya Tangamano alikojihisi mgeni. Anashindwa kusahau masaibu yaliyomkumba licha ya juhudi za Bi Dhahabu za kumshauri asahau yaliyopita na kuikubali hali yake mpya.

Tathmini: Rejelea masaibu yaliyoikumba familia ya Lunga Kiriri-Kangata.

Joyce Nekesa

Shule ya Kitaifa ya Kapsabet Boys

You can share this post!

Cindy asimulia changamoto zinazowakumba waigizaji, mastaa

UCHAMBUZI WA FASIHI: Ploti ya Onyesho la Kwanza Tendo la...

T L