• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 1:20 PM
NGUVU ZA HOJA: Sababu ya Mswahili kuhusishwa na ulaghai

NGUVU ZA HOJA: Sababu ya Mswahili kuhusishwa na ulaghai

Na PROF IRIBE MWANGI

JUMAMOSI iliyopita nilikuwa natembea na rafiki yangu Prof Obuchi mtaani.

Tuliingia mahali kununua bidhaa fulani. Mteja mmoja alikuwa amesimama akiongea na muuzaji.

Mteja alikuwa ameshika hundi. Wote walikuwa katika mazungumzo ya dhati ambayo hatukuweza kuyasikia.

Tulichokisikia ni hitimisho la mwenye duka, “Wee bwana, usiniletee uswahili wako hapa!”

Katika muktadha (mwandani wangu fulani hulitaja neno hili kama maktaba) huu, uswahili unanasibishwa na ujanja, upwagu na ulaghai. Kwa nini hali hii hutokea?

Hili ni jambo la kihistoria. Wageni wa mwanzo walifika katika eneo la Pwani na wenyeji wao wa kwanza walikuwa Waswahili.

Waswahili basi walijifunza mengi mapya kabla ya jamii nyingi za bara. Walikuwa kwenye misafara mingi ya biashara na walitumia hila na ujanja kufaulisha biashara zao. Jambo hili lilifanya mtu yeyote aliyetumia ujanja na ulaghai kuitwa Mswahili.

Hiki kimekuwa kikwazo kikubwa dhidi ya matumizi ya Kiswahili kwa kuwa wengi wasingetaka kunasibishwa na ulaghai. Maana inayotokea hapa kuhusu Uswahili na Mswahili basi ni hasi.

Lakini hiyo maana hasi ni ya kuhusishwa tu, ni maana ambayo huitwa ya kimatilaba.

Ukweli ni kwamba Mswahili ni Mwafrika, Mbantu ambaye asili yake ni eneo la pwani ya Afrika Mashariki.

Mswahili si mtu anayetokana na mseto wa damu ya Mwarabu na Mwafrika kama ilivyoelezwa katika baadhi ya vitabu.

Mswahili si Mwarabu na wala Kiswahili si mojawapo ya lahaja ya KiArabu. Kiswahili ni KiBantu. Bila shaka Mswahili si mtu mjanja au mlaghai, ni hali tu iliyomfanya kupata maarifa na ujuzi fulani kabla ya wengine.

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya...

VALENTINE OBARA: Mashambulio yazimwe kabla kuenea kwingine

T L