• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
VYAMA: Kongamano la sita la CHAUKIDU laanza rasmi katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi

VYAMA: Kongamano la sita la CHAUKIDU laanza rasmi katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi

Na CHRIS ADUNGO

KONGAMANO la sita la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) litaanza rasmi hii leo katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi.

Mada kuu ya kongamano hili la siku mbili ni ‘Kiswahili na Viswahili Kuelekea Karne Moja ya Usanifishaji’. Washiriki watapania pia kulinganisha mitazamo kuhusu matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali na kuweka wazi mikakati ya kuendeleza lugha hii inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 kote duniani.

Kwa mujibu wa Dkt Nancy Ngowa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Andalizi kutoka Chuo Kikuu cha Pwani, kongamano limevutia idadi kubwa ya wajumbe kutoka Amerika, Tanzania, Uingereza, Rwanda, Afrika Kusini, Ghana, DR Congo, Poland, Ujerumani, Sudan, Ethiopia, Zanzibar na Burundi.

“Kongamano litafunguliwa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Pwani, Prof Mohammed Rajab. Litafungwa kesho na Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Jeffah Amason Kingi na washiriki kupata fursa ya kuzuru Fort Jesus (Mombasa) na Jumba Ruins (Mtwapa) siku inayofuata,” akasema Ngowa.

Wajumbe wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika vyuo vikuu vya ughaibuni waliandaa jana warsha iliyowapa fursa ya kujadili nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa sasa na haja ya kuhakikisha kuwa hawawi nyuma katika safari ya kuijengea lugha hii majukwaa zaidi ya kukuzwa kimataifa.

“Upekee wa kongamano hili ni kwamba linaandaliwa katika mazingira yaliyo na wazungumzaji asilia wa Kiswahili. Washiriki watajifunza mengi kuhusu utamaduni wa Waswahili kuanzia kwa vyakula, mavazi, mashairi na vifaa wanavyovitumia kufanyia shughuli mbalimbali,” akaongeza Dkt Ngowa.

Kongamano la CHAUKIDU linafanyika siku mbili baada ya Mkutano Mkuu wa 41 wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamadumi (UNESCO) kutenga Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Azimio hilo lilipitishwa na nchi zote wanachama wa UNESCO bila kupingwa mnamo Novemba 23 jijini Paris, Ufaransa. Kiswahili sasa ni lugha ya kwanza Afrika iliyo na siku maalumu ya kuadhimishwa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Makala kutokana na kongamano yatachapishwa katika Journal of Swahili Studies lililozinduliwa katika Chuo Kikuu cha Pwani mnamo 2020.

Mbali na Serikali ya Kaunti ya Kilifi, wadau wengine ambao wamefanikisha maandalizi ya kongamano la CHAUKIDU mwaka huu kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Pwani ni East African Educational Publishers (EAEP), Focus Publishers na Benki ya Equity.

You can share this post!

Haaland awabeba Dortmund dhidi ya Furth ligini

Refa anayeibukia na mwenye maono ya kupiga shughuli...

T L