• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:55 PM
Refa anayeibukia na mwenye maono ya kupiga shughuli kimataifa

Refa anayeibukia na mwenye maono ya kupiga shughuli kimataifa

Na PATRICK KILAVUKA

Kwa kweli jitihada haiondoi kudura. Ref Chipukizi Ivonne Wayua, 21, ni muamuzi mchanga ambaye amejifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba amefikia ndoto yake ya kufikia refa wa hadhi wa kimataifa mithili ya Mike Dean.

Kabla kiu ya kuwa mpuliza kipenga kumsakama, refa huyu aliyezaliwa Mitaboni, Kaunti ya Machakos alikuwa mchezaji wa kabumbu akicheza kama mchana nyavu. Alisomea shule ya Msingi ya Kalikya kisha sekondari za Upendo, Kangemi na Top Mark, Kawangware.

Aliwahi kuwa mchezaji bora akiwa Shule ya Msingi Kalikya mwaka 2014 katika michezo ya Shule za Msingi Kaunti ya Machakos. Alipokuja Jijini, alijiunga na ulingo wa kandanda kwa kusajiliwa katika timu ya Zion Winners halafu kuguria Waruku Sportiff ambapo alicheza ngarambe ya Westlands Soccer Association na dimba la Tim Wanyonyi Super Cup, 2020.

Hata hivyo, alichukua mikoba ya timu ya mabinti wa Waruku Sportiff. Mwaka jana, kulitokea fursa ya kujifunza urefa na aliuona kama mwanya wa upenyo katika kuhakikisha anaziba pengo la akina dada katika jukwaa hili la kuangazia uwezo wa utajiri wao katika kuwa waamuzi wa soka.

Alipata mafunzo ya wiki moja na kupata cheti cha ngazi ya tatu. Aliweza kupata nafasi ya kufanya zoezi la urefa katika ngarambe Ligi ya Kanda ya Shirikisho la Kandanda Kenya (FKF).Mbali na ligi hiyo, ligi ya Kaunti ya Nairobi ya Chama cha Soka (NCFA) ilipoasisiwa, alipata fursa ya kuchezesha mchuano wa Zion Winners dhidi ya Utalii.

Refa Ivonne Wayua akizungumza na kocha wakati mchuano wa Ligi ya NCFA (Nairobi County football Association) ya wasiozidi miaka 13 uwanjani Kihumbuni…Picha/PATRICK KILAVUKA

Pia, alinogesha uamuzi wake katika mechi ya ligi hiyo Daraja ya Kwanza kama refa wa kwanza msaidizi ambapo alipigisha mechi kati ya Westlands Soccer na Kapsambo. Isitoshe, alichezesha mchuano wa ligi ya Primia ya NCFA kati Zion Winners na Kinyago .

Mbali na kuchezesha mechi ya Daraja ya Kwanza kati ya Golden Stars dhidi ya Kinyago. Hata hivyo, anasema kwamba kiu ya kuwafunza chipukizi kandanda kupitia maamuzi, alizamia kuwa muamuzi wa mechi za chipukizi hao kama njia ya kuwapelekea kuzingatia sheria za kabumbu.

Mbali na marefa wengine kutovutiwa na kuwa wapuliza kipenga kwa kizazi hiki cha soka ambacho ndicho shina la kandanda. Yeye anaridhika kukikuza. Anapuliza firimbi katika michuano ya Ligi ya NCFA ya wasiozidi miaka 13 na 15.

Kupitia kibarua hiki cha kuleta nidhamu katika wachezaji makinda, ameona wanasoka chipukizi wakizingatia sheria za soka. “Nilitaka kuwapatia wanadimba chipukizi laini ya kutambua umuhimu wa kusakata boli wakifuata sheria za soka.

Marefa wengi huwa hawataki kufanya maamuzi ya michezo ya vijana hao. Lakini ninayo matumaini kuwasuka vyema wakiwa bado wachanga kwa kuzizijua sheria, kutawawezesha kunidhamika, kufanya kazi ya urefa kuwa rahisi na kutambua umaana wa kuwa wachezaji wa soka,” aelezea Wayua.

Changamoto ambayo ameipata katika kusukuma gurudumu la urefa ni kwamba, kuna kasumba ya taasubi ya kiume miongoni mwa wanasoka, mashabiki na makocha hali ambayo hupelekea kushuku uamuzi unayofanywa uwanjani na marefa ya jinsia ya kike.

Angependa kuwashukuru wazazi wake, wadau NCFA na Westlands soccer, Waruku Sportiff na kocha Daniel Mutiso kwa himizo zao na jukwaa waliompa kujikuza katika uwanja wa kandanda na sasa anavuna matunda yake.

Manufaa ambayo amechota katika shughuli mzima ni kwamba, sasa anaweza kujikimu na hata kusaidia mzazi kadri ya uwezo alionao. Aghalabu, urefa wa soka umemtenga na maovu ya kijamii na anakumbuka wosia wa mwalimu wake Bw Kioko kwamba akizingatia boli, huenda akarithi talanta ya mamake aliyesomea alikosomea Shule ya Msingi ya Kalikya kwa sababu alikuwa anasakata kabumbu mpaka kiwango cha kitaifa zama zake.

Anasema mwa miaka tano ijayo ni ombi lake kwamba, atakuwa anapuliza kipenga kama refa wa kati katika Ligi za hadhi za Shirikisho la Kandanda Nchini. Ushauri wake kwa makocha, wanasoka na makocha ni kwamba, wawe wakizipitia kanuni za utaratibu wa kuchezesha soka ambazo unabadilika kila kuchao ili wawe na uwezo wa kujua na kuwa na upevu wa mabadiliko katika sheria hizo.

Wathamini maamuzi yafao kutoka kwa wapuliza kipenga wa kila jinsia.

You can share this post!

VYAMA: Kongamano la sita la CHAUKIDU laanza rasmi katika...

Serikali kutathmini VAT inayotozwa mbegu za mboga

T L