• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Makahaba Nairobi walia wenzao kutoka Uganda na Tanzania wanawapokonya ‘wateja’

Makahaba Nairobi walia wenzao kutoka Uganda na Tanzania wanawapokonya ‘wateja’

Na MWANGI MUIRURI

MAKAHABA nchini wanaohudumu katika Kaunti ya Nairobi wameteta kwamba wenzao kutoka Uganda na Tanzania, wameteka soko lao.  

Makahaba hao wamelalamikia kupokonywa soko na wenzao, kutoka nchi jirani jambo wanalosemama limewaathiri kimapato.

Wameteta kuwa warembo motomoto wamekuwa wakivuka mipaka na kuingia jiji la Nairobi, ambapo wanavutia wateja wa mahaba kwa kiwango kikuu.

Kwa upande wao, wanaume wengi ambao tuliongea nao katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi walisema kwamba warembo wa mataifa hayo jirani huvutia kitabia na hata huduma.

Mshirikishi wa muungano wa makahaba Nairobi Mashariki, Bi Cecilia Wangari aliambia Taifa Dijitali kwamba wanawake hao kutoka mataifa jirani wanapendelewa na wateja.

“Wamekuja na kuingia mitaani ambapo wamezindua ushindani mkuu dhidi yetu. Sielewi ni kwa nini wateja wanawakimbilia huku sisi tukiachwa hoi katika soko la taifa letu,” akasema.

Mmoja wa Waganda hao Bi Joy Abbo aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “sisi hatuna mambo kwa kuwa tunasimama kando na hawa wenzetu Wakenya lakini tunashtukia tu wateja wakifurika kwetu na hata kutulipa pesa za ziada kuliko tunazowatoza”.

Bi Wangari aliteta kuwa “hata baada ya kupiga ripoti kwa maafisa wa kiusalama tukiteta kuwa wao ni maharamia wanaofaa kusakwa na kurejeshwa makwao, tunaambiwa kwamba wako nchini kihalali kufuatia mkataba wa maelewano ya Afrika Mashariki”.

Hata wakiteta wanawake hao wazimwe kushiriki biashara ya ngono, Wangari alisema “tunaambiwa kwamba sote tunafaa kukamatwa kwa kuwa sheria zinazima ukahaba nchini”.

Akielezea kulemewa na gharama ya juu ya maisha, alisema “sasa tumebakia kumenyana sokoni tukijaribu kila aina ya mbinu kubakia sokoni dhidi ya ushindani wao”.

Makahaba wakarimu kutoka Tanzania na Uganda Mwanamume aliyejitambulisha kama Symo alisema kuwa “warembo hao wa Tanzania na Uganda sio wezi, hawana ujeuri wa kuharakisha mteja na baada ya huduma hutushukuru na kutuombea baraka za pesa ndio turudi tena kununua huduma”.

Alisema kwamba hali hiyo ni kinyume na wengi wa hapa nchini ambao “hutupora, hutuzimia uhondo kabla ya mkataba wa pesa kuisha, na kando na kuongea kiuhuni, hata hutushambulia”.

Kamanda wa polisi Nairobi Bw Adamson Bungei aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “ikiwa wanataka sheria iwasaidie kusalia wakivunja sheria, huku tukiwafurusha wenzao basi wasahau”.

Bw Bungei alisema kwamba “kilichoko ni kwamba kazi ya kuwaandama walio katika biashara hiyo ni yetu sote kama vyombo vya usalama na hatuwezi kuwa na mapendeleo”.

Hata hivyo, alisema kuwa ni vigumu sana kudhibiti sekta hiyo ya ukahaba.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kindiki: Nguvu sawa na za kukabili Al-Shabaab kutumika...

Bajeti 2023/24: Biashara ndogo na za kadri zatengewa Sh300...

T L