• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
MAKALA YA KIPEKEE: Kanisa linalohusishwa na kidosho aliyesitisha ghafla harusi lazungumza   

MAKALA YA KIPEKEE: Kanisa linalohusishwa na kidosho aliyesitisha ghafla harusi lazungumza   

NA FRIDAH OKACHI 

KANISA ambalo msichana alitarajiwa kufunga pingu za maisha na mchumba wake japo akasitisha ghafla harusi limezungumza, likisema litaangazia suala hilo ndani kwa ndani.   

Africa Gospel, kanisa lililoko Kapsoiyo, Kaunti ya Bomet limesema limeanzisha uchunguzi kubaini sababu zilizofanya bibi harusi kubadilisha nia dakika za mwisho.

Bi harusi na mchumba wake, walitarajiwa kuwa ‘kitu kimoja’ mnamo Jumamosi, Desemba 9, 2023 japo akageuza Mawazo usiku wa kuamkia siku ya siku.

Kanisa la Africa Gospel lilitarajiwa kuunganisha wanandoa hao watarajiwa.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, limesema suala hilo lipo chini yake katika harakati kubaini kilichochochea mtibuko wa hafla hiyo.

Mmoja wa washirika ambaye aliomba kubana majina yake, alikiri uchunguzi umeanzishwa.

Hata hivyo, alisusia kuzungumza mengi akisema wahubiri na wazee wa kanisa tayari wametwaa suala hilo.

“Sitaki kuongelea jambo hilo ambalo lipo chini ya kanisa kufanya uchunguzi…Mwanandoa aliomba muda zaidi,” alisema.

Kutibuka kwa mpango wa harusi hiyo, kulifichuka kupitia mitandao ya kijamii.

Katika ujumbe uliosambazwa kupitia WhatsApp na mmoja wa wanachama wa kamati andalizi ya harusi aliyetambulika kama Kiprotich Edwin, wanandoa hao; Nelly na Amos walionelea ni heri kujipa muda zaidi.

Aidha, duru zinaarifu kwamba wazazi wa pande zote mbili walikubaliana na pendekezo hilo, japo liliibuliwa na bi harusi.

“Habari za asubuhi marafiki, wengi wa marafiki wa Nelly na Amos wanataka kujua sababu ni ipi harusi hiyo imeahirishwa…Sababu kuu ni kuwa Nelly ameomba muda zaidi. Kanisa na wazazi wa pande zote mbili wamekubali ombi lake. Asante kwa kuelewa,” unasema ujumbe uliochapishwa Kiprotich.

Kulingana na mchungaji wa kanisa hilo, alipokea barua ya iliyomuarifu kwamba harusi hiyo haitaendelea jinsi ilivyopangwa baada ya kutoelewana kati ya familia hizo mbili.

Tukio la aina hiyo la sarakasi kwa wanandoa si la kwanza kuwahi kufanyika, kwani mwaka 2016 mwanamuziki wa nyimbo za injili Eunice Njeri alimpa talaka mume wake Isaac Bukasa muda mfupi baada ya kufunga pingu za maisha.

Mwimbaji, hata hivyo, alioleka baadaye kwa mume mwingine.

  • Tags

You can share this post!

Krismasi: Vijana wanavyopiga sherehe wakigeuza makazi yao...

Vipaji wa soka Murang’a wageuza mashamba kuwa uwanja El...

T L