• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Vipaji wa soka Murang’a wageuza mashamba kuwa uwanja El Nino ikiwahangaisha

Vipaji wa soka Murang’a wageuza mashamba kuwa uwanja El Nino ikiwahangaisha

NA MWANGI MUIRURI
MVUA ya El Nino ambayo imekuwa ikishuhudiwa hapa nchini imeanika hali duni ya viwanja vya michezo katika Kaunti ya Murang’a, hali ambayo inaathiri ukuzaji vipaji vya vijana.

Viwanja kulowa maji, kuwa na matope na miundombinu duni kumetajwa kama kero kuu ambapo vijana wanaojaribu kujiendeleza katika kukuza vipaji vyao inabidi wasubiri mvua ikatike.

Hali hii imetatiza ligi za soka katika kaunti hiyo kwa timu za vijiji hivyo basi hata kuathiri vipaji kwa sababu ya ukosefu wa mazoezi.

“Tumekuwa tukitumia viwanja vya shule za msingi kuendeleza ligi zetu za soka mashinani. Lakini wakati Covid-19 iliingia 2020 na mikusanyiko ya watu ikafungwa, ligi nyingi zilisambaratika,” asema Bw Julius Mwangi ambaye ni mshirikishi wa talanta na ubunifu mashinani Murang’a.

Mwangi aliongeza kwamba “wakati hatari ya Covid iliisha na tukarejelea michezo mashinani, kuliingia hatari ya wizi shuleni hali ambayo tena ilifanya wengi wa walimu wakuu na bodi simamizi kufunga viwanja vyao kwa wanavijiji”.

Hali hiyo iliwatuma vijana na ligi zao kutafuta viwanja vya kuendelezea vipaji vyao, kwingine ikiwabidi kufyeka vichaka katika mashamba yasiyotumika ili kupata nafasi za mazoezi na ushindani.

“Bila kupigwa jeki na yeyote, vijana wamekuwa wakihangaika si haba kupata mazingara muafaka kuendeleza michezo na kwa sasa mvua ya El Nino imetuhangaisha ya kutosha baada ya maji na matope kuvamia viwanja hivyo ambavyo tumejitafutia kwa ubunifu,” akasema Bw Mwangi.

Aliongeza kwamba hali pia si hali katika viwanja vya kaunti ambavyo vimetengewa ushindani kwa kuwa havijatunzwa kwa vyovyote vile hivyo basi kuvifanya viwe sawa na madimbwi ya maji taka na matope.

Katika siku za hivi karibuni, picha zimekuwa zikisambazwa mitandaoni kwa ucheshi na kejeli kuhusu hali ilivyo, wachezaji soka wakiulizwa ni kwa nini waliingia ugani kulima au kutengeneza matofali ya ujenzi kutokana na hali ya matope.

Katika stakabadhi za matumizi ya kaunti, kwa miaka 10 kuanzia 2014 sekta ya michezo ilitengewa Sh2 bilioni huku kila mbunge katika maeneobunge yote saba Murang’a akipata Sh1 milioni kila mwaka kuendeleza michezo mashinani.

Wachezaji wa mpira katika uwanja wa Kandara kwa Waziri wa Mashamba Bi Alice Wahome na mwenzake wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u. PICHA|MWANGI MUIRURI

Mwaka wa 2019, Gavana Mwangi wa Iria (japo kwa sasa ni mstaafu) alitangaza kwamba alikuwa ametenga Sh100 milioni za kukarabati viwanja vinane vya michezo, licha ya kwamba alipoapishwa mwaka wa 2013, alikuwa ametangaza kwamba angekarabati viwanja 35.

Hii ilimaanisha uwanja kwa kila wadi zote 35 za Kaunti ya Murang’a.

Viwanja vya kaunti hiyo ni pamoja na Ihura, Kago, Matenjagwo, Gakoigo, Mumbi, Kahuro, Rurii na Kimorori, licha ya ahadi, hakuna kilichofanywa cha kufanya nyuga hizo kuwa na viwango vya kuorodheshwa kama faafu kimichezo.

Hata licha ya kujivunia kuwa na timu iliyopewa jina la Kaunti—Murang’a Seal na ambayo ilianzishwa na walinzi wa kampuni ya G4s na kwa sasa inawika katika ligi kuu ya kitaifa ya soka, ilibidi mwekezaji binafsi ajengee Kaunti uwanja.

Wakili Robert Macharia alijenga uwanja wake wa kibinafsi kwa kima cha Sh350 milioni na kwa malipo, Murang’a Seal na mashabiki huutumia kuandaa gozi.

Oktoba 11, 2023 Waziri wa Michezo Bw Ababu Namwamba alitembelea Murang’a na kutangaza kwamba serikali itajenga uwanja mkubwa wa kimichezo.

“Kaunti hii inasifika sana kwa maendeleo ya nchi na ni lazima tuituze uwanja mkubwa wa hadhi ili vijana hapa wajiendeleze kispoti,” akasema.

Hali hii duni ya viwanja imezidisha presha kwa viongozi wa kaunti kuchukulia spoti kwa uzito zaidi na liwe suala la dharura kwamba kuwe na mvua au kiangazi, kutakuwa na nyuga za kutosha kuandaa mazoezi na ushindani katika fani mbalimbali za kispoti.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MAKALA YA KIPEKEE: Kanisa linalohusishwa na kidosho...

Kinara wa Benki ya Equity na familia ya Moi wakabana koo...

T L