• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MALEZI KIDIJITALI: Daima kinga yashinda tiba!

MALEZI KIDIJITALI: Daima kinga yashinda tiba!

NA BENSON MATHEKA

JUKUMU kubwa la mzazi enzi hizi za dijitali ni kudhibiti matumizi ya vifaabebe vya watoto wake.

Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kwamba mzazi hana budi kudhibiti jinsi mtoto wake anavyotumia vifaa hivi ili kumwepusha na hatari zinazozidi kuongezeka.

“Hatari kwa mtoto zinazotokana na matumizi ya vifaabebe na teknolojia kwa jumla hasa mtandaoni zinaweza kumsababishia mzazi hasara kubwa mtoto anapoathirika. Hivyo basi, ili kuzuia hali hii, mzazi anafaa kutekeleza jukumu lake la kufuatilia na kudhibiti matumizi ya vifaabebe ya watoto wake kuanzia wakiwa na umri mdogo,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Ian Doras kwenye makala aliyochapisha mtandaoni.

Doras anasema kwamba wazazi wanaofuatilia kwa karibu matumizi ya vifaabebe ya watoto wao huwa wanaepuka gharama ya kupuuza jukumu hilo.

“Kutodhibiti matumizi ya mtandao ya mtoto wako au muda anaotumia akizama kwenye simu na kompyuta kunamaanisha mzazi atabeba mzigo mkubwa wa gharama ya matibabu,” asema.

Kulingana na mtafiti wa masuala ya malezi Damaris Phillips, kufuatilia na kudhibiti matumizi ya vifaabebe ni sawa na mzazi kukinga mtoto na maradhi.

“Daima kinga yashinda tiba. Hii ndio sababu wazazi wanaoachilia watoto wao kuzama katika matumizi ya mtandao bila kujali wanachofanya na muda wanaotumia huwa wanalia baadaye wakipata matatizo ya kiafya, kisaikolojia au kupotoshwa na wahalifu wa mtandao,” asema Damaris.

Mtaalamu huyu anasema kwamba wazazi wanafaa kukumbatia jukumu la kusaidia, kufuatilia, kutekeleza na kudhibiti matumizi ya vifaabebe vya watoto wao.

“Enzi hizi za dijitali, hatari ya mtoto inaanzia kwa kile anachofanya na kifaa cha teknolojia ya kisasa unachomnunulia kama mzazi. Hivyo basi, wa kwanza kulaumiwa mambo yakienda mrama ni mzazi,” asema.

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Kuhifadhi chakula bila friji

SOKOMOKO WIKI HII: Wajackoyah na mdogowe walivyopigwa na...

T L