• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
AKILIMALI: Mfumo bora kufanikisha kilimo cha matikitimaji

AKILIMALI: Mfumo bora kufanikisha kilimo cha matikitimaji

Na SAMMY WAWERU

MATIKITIMAJI ni kati ya mazao ya shambani yenye soko la haraka kwa sababu ya ladha yake ya kipekee na utamu.

Ni matunda yanayopendwa kwa sababu ya kusheheni virutubisho, hasa madini muhimu ya Vitamini.

Isitoshe, yana maji yake ya ndani kwa ndani na ambayo ni hai na yenye sukari.

Kutokana na manufaa yake kiafya na yenye ushindani mkubwa sokoni, Joshua Musyoki na David Mbula waliamua kuingilia kilimo chake.

Walichukua hatua hiyo baada ya kuchoshwa na kilimo cha nyanya na mahindi, wakitaja nyanya kama mazao yenye kikwazo kisichomithilika cha soko.

Nyoyo zao sasa zimeridhishwa na matikitimaji na wanasema ikiwa kuna shughuli za kilimo wasizojutia kuingilia, ziite ukuzaji wa matunda hayo.

Wameweza kufanikisha kilimo cha matikitimaji eneo ambalo ni nusu-jangwa, Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu.

Kwa sababu ya uhaba wa maji, wenyeji wengi hukuza mahindi na nyanya kwa waliojipanga kupitia mfumo wa uvunaji maji.

Musyoki na Mbula ni kati ya wachache wanaolima matikitimaji.

Wanayasifia kuwa miongoni mwa mimea rahisi kupanda, kutunza na ambayo gharama yake ni ya chini mno.

Wakulima hao hulima shamba kwa kutumia trekta. Mashine hiyo vilevile huwaandalia mitaro.

“Nafasi kati ya laini za mitaro huipa mita 3 – 4, kisha kutoka mmea mmoja hadi mwingine mita 4,” Musyoki anaelezea, akidokeza kwamba wamekumbatia mfumo wa besini.

Joshua Musyoki, mkulima wa matikitimaji eneo la Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu akielezea kuhusu mfumo bora kuzalisha matunda hayo. Picha/ Sammy Waweru

Mitaro huandaliwa kuunda mfano wa ‘milima’, ambayo kulingana na maelezo ya Musyoki ndiyo laini.

“Beshini ni mitaro iliyo kati ya laini, tunayoiziba kila baada ya mita 4,” anasema.

Hutumia mbolea ya mifugo na fatalaiza katika shughuli za upanzi.

“Tukishaandaa jukwaa la upanzi, humwagilia mitaro maji na yanapofika kuanzia juu, ndipo hupanda mbegu ya matikitimaji,” Musyoki anafafanua.

Mbinu nyingine ni ya ‘Master pit’, iliyovumbuliwa na Zacharia Onchuru, mtafiti na mkulima hodari wa matikitimaji eneo la Pwani.

Ni mfumo wa utengenezaji beshini, yenye kina cha urefu wa sentimita 30, kuenda chini, na upana wa sentimita 45.

Beshini zinapaswa kuwa umbali wa mita 2 kwenye laini, nafasi kati ya laini hadi nyingine Onchuru akipendekeza iwe mita 2 pia.

“Katika kila beshini, panda mbegu nne za matikitimaji,” mtaalamu huyo anashauri.

Kulingana na Onchuru, ekari moja inasitiri jumla ya beshini 1, 200, akisifia mfumo huo kupunguza matumizi ya maji kwani mkulima pia anaweza kutumia nyasi za boji (mulching) ili kuzuia uvukizi.

Joshua Musyoki anasema baada ya wiki tatu, huweka kwenye mashina ya mitikitimaji fatalaiza ili kuboresha mazao.

“Inapoanza kutunda, endelea kuitunza kwa mbolea ya mifugo na fatalaiza,” Musyoki anahimiza, akisisitiza haja ya unyunyiziaji maji.

Mkulima huyo anasema kwa wiki, hunyunyizia maji mara tatu.

“Nimegundua matikitimaji yanastawi na kufanya bora maeneo yenye joto, mazao ya maeneo kame yakiwa na ushindani mkuu sokoni,” anasema mkulima huyo.

Vidukari, vithiripi, viwavi, spider mites na melon flies, ni kati ya wadudu wanaoshambulia matunda hayo.

Magonjwa yanayoshuhudiwa ni pamoja na early na late blight, Anthracnose, Bacterial fruit blotch, downy mildew, miongoni mwa mengine.

Matikitimaji yanakomaa kati ya siku 65 – 75, baada ya upanzi.

Mbali na kuliwa yakiwa yameiva, pia yanaweza kuongezwa thamani kwa kuyaunda sharubati au juisi.

You can share this post!

TAHARIRI: Stars ianze kusaka vipaji mashinani

Liverpool wakabwa koo na Newcastle United katika EPL ugani...