• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Mikakati ya Gavana Wamatangi kuboresha sekta ya maziwa Kiambu

Mikakati ya Gavana Wamatangi kuboresha sekta ya maziwa Kiambu

NA SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Kaunti ya Kiambu imesambaza vifaa vya uongezaji maziwa thamani kwa vyama vya ushirika vya wafugaji, kama njia mojawapo kupiga jeki sekta ya maziwa.

Ufadhili wa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh25 milioni, ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya Kaunti ya Kiambu kupiga jeki sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Akivikabidhi viongozi wa vyama vya ushirika, Gavana Kimani Wamatangi aliainisha mipango aliyoweka kuangazia changamoto zinazozingira sekta ya maziwa Kiambu.

Mchango huo ulijumuisha mashine tano za kudondoa maziwa (ATM) za kiwango cha lita 3, 000 kila moja, za kuchemsha (lita 1, 000 kila moja) na ratili za kupima maziwa.

Vifaa hivyo, Gavana Wamatangi alisema vinalenga kuongeza maziwa thamani ili kuboresha mianya ya soko.

“Kupitia mikakati niliyoweka, serikali ya kaunti yangu inashirikiana na wadauhusika kuboresha sekta ya maziwa nchini,” Bw Wamatangi akasema.

Wakati wa utoaji vifaa hivyo, Muungano wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Kiambu, uliwakilishwa na Bw Peter Mwangi ambaye ni mwenyekiti wa Kireira Dairy Farmers Cooperative.

Hafla ya ufadhili huo ilifanyika katika Makao Makuu ya Serikali ya Kaunti ya Kiambu, Kiambu Mjini, na Gavana Wamatangi alidokeza mikakati kama vile mbinu za kukabiliana na magonjwa, vimelea, ujamiishaji mifugo, soko, mifumo ya kiteknolojia, na ubora endelevu, aliyoweka kufanikisha ufugaji ng’ombe wa maziwa.

“Serikali ya Kaunti imeweka mipango faafu kuboresha sekta ya ufugaji ng’ombe wa maziwa, inayojumuisha ununuzi wa chanjo kudhibiti kero ya magonjwa, utoaji wa mbegu za uhamilishaji (AI) bila malipo na pia zingine kupunguza bei,” akaelezea.

Kufuatia gharama ya juu ya chakula cha madukani cha mifugo, Gavana alisema serikali yake inaendeleza mikakati kujenga kiwanda cha kutengeza chakula ambacho kitakuwa cha ubora wa juu.

“Tunajadiliana na Kiambu County Dairy Farmers Association (KICODAFA) ili kufanikisha mpango huo.”

Serikali yangu imejitolea kufanya mafunzo ya kilimo kwa njia ya utaalamu, tukilenga mifumo ya kisasa na teknolojia na bunifu kukabiliana na athari za tabianchi, Gavana Wamatangi akasema.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya ushirika, Bw Peter Mwangi, mwenyekiti wa Kireira Dairy Farmers Cooperative, alisema licha ya Kaunti ya Kiambu kuwa kati ya maeneo yanayoongoza katika uzalishaji wa maziwa nchini, imekuwa ikisahaulika na serikali.

Mwangi, hata hivyo, alipongeza jitihada za Gavana Wamatangi akisema zinaashiria kiongozi anayeelewa changamoto za wakulima.

Alisisitiza haja ya wadauhusika; kutoka sekta ya kibinafsi na umma kushirikiana.

“Tuna changamoto nyingi zinazotuzingira, ila tunashukuru Gavana Kimani Wamatangi kwa sababu anaunga mkono mipango yetu katika kuongeza maziwa thamani,” Bw Mwangi alisema.

Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Kiambu (CEC), Wilfred Mwenda alisema idara yake inaendeleza oparesheni ya utoaji chanjo kwa mifugo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundomsingi ya barabara.

“Tunafanya kazi kwa karibu na vyama vya ushirika kuboresha soko la maziwa,” Bw Mwenda akasema.

Kiambu inaongoza katika uzalishaji wa maziwa nchini, ila wakulima wamekuwa wakilalamikia bei duni.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Harambee Starlets yashindwa kufuzu WAFCOB baada ya...

Wahuni wa utekaji nyara Kiambu wanaswa   

T L