• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Kenya Kwanza yatishia kuzima Winnie Odinga

MIKIMBIO YA SIASA: Kenya Kwanza yatishia kuzima Winnie Odinga

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto sasa anapania kuwapa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Azimio Raila Odinga, kichapo kingine kwa kuzima juhudi za wandani wao kujishindia nafasi kwenye orodha ya wawakilishi tisa wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Duru katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA) zimeiambia safu hii kwamba uchaguzi wa wawakilishi wa Kenya katika bunge la EALA ni mojawapo ya ajenda kuu za mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza (PG) utakaoongozwa na Rais Ruto, Jumanne.

“Ndiyo, mkutano wetu wa PG utafanyika Jumanne ambapo tutajadili suala hili la EALA na miswada mingine ambayo tunatarajia kuwasilisha bungeni kufanikisha yaliyomo katika manifesto ya Kenya Kwanza (KKA).
Tutahakikisha kuwa watu tisa watakaochaguliwa kuwakilisha Kenya katika EALA ni wale ambao wako tayari kupigia debe sera za serikali ya sasa katika bunge hilo la Afrika Mashariki,” akasema mbunge mmoja wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambaye aliomba tulibane jina lake.

“Aidha, tutakuwa na usemi kuhusu ni kina nani watakaochaguliwa katika nafasi tatu zilizotengewa Azimio kwenye orodha ya watu tisa watakaowakilisha Kenya katika EALA. Hii ni kwa sababu wote walioorodheshwa na mirengo hii miwili watapigiwa kura, mmoja baada ya mwingine, bungeni,” akaongeza.

Inasemekana mrengo wa KKA unapania kuzima uchaguzi wa wawakilishi wa Azimio wanaodhaniwa kupendelewa na Bw Kenyatta na Odinga. Hao ni Bi Winnie Odinga, ambaye ni bintiye Raila na Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni (aliyekuwa Mbunge wa Ndaragua) na mkurugenzi wa uchaguzi katika chama hicho Kanini Kega (aliyekuwa Mbunge wa Kieni).

Chama cha ODM kimewasilisha majina ya watu sita ambao watapigania nafasi mbili zilizotengewa chama hicho. Wao ni; Winnie, mfanyabiashara wa Mombasa Suleiman Shahbal, wabunge wa zamani; Justus Kizito (Shinyalu), Mohamed Diriye (Wajir Kusini), Timothy Bosire (Kitutu Masaba) na aliyekuwa Waziri katika serikali ya kaunti ya Turkana, Beatrice Askul.

Hata hivyo, inasemekana kuwa Bw Odinga anapendelea bintiye Winnie, na Bw Shahbal wapewe nafasi hizo mbili.

Kwa upande mwingine nafasi moja ya Jubilee inashindaniwa na Bw Kioni na Kega, pamoja na aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Wajir Fatuma Gedi. Lakini inasemekana uongozi wa Jubilee unataka Bw Kega apewe nafasi hiyo moja iliyotengewa Jubilee.

Nafasi moja ya chama cha Wiper nayo imetengewa mwanawe kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka, Kennedy Kalonzo, aliyewakilisha Kenya katika EALA kati ya 2017 na mwaka huu.

Lakini wabunge wa muungano wa KKA, hasa wale UDA wameapa kuhakikisha kuwa wanawaangusha Bi Winnie, Bw Kega na Kioni katika uchaguzi utakaofanyika bungeni Alhamisi Novemba 17.

“Ndiyo, tutawaangusha wale wandani wa karibu wa Raila na Uhuru waliotuponda zaidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu,” anasema Mbunge wa Kimili, Didmus Barasa.

“Isitoshe, sisi kama wabunge kutoka Magharibi tunamshabikia Bw Justus Kizito kwa sababu ODM haijawatendea haki wabunge kutoka eneo hilo licha ya wao kumsaidia Raila kupata kura nyingi,” anaongeza mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya UDA.

Kulingana na kanuni ya uchaguzi wa wawakilishi wa Kenya katika EALA, wale wote walioorodheshwa kushindania nafasi tisa za Kenya, hupigiwa kura bungeni mmoja baada ya mwingine.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Dau la Azimio laelekea kuzama

KIGODA CHA PWANI: Uteuzi wa Omar, Shahbal katika EALA...

T L