• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mishie analenga kufikia Zoe Saldana 

Mishie analenga kufikia Zoe Saldana 

Na JOHN KIMWERE 

MWANZO kila mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. 

Ni katika hali ya kutumainia na kuvumilia maana anaamini kuwa wakati upo atafanikiwa kutinga upeo wa msanii wa kimataifa.

Anashikilia kuwa ingawa hajapata mashiko, katika tasnia hii amepania kuendelea kujifunza zaidi masuala ya uigizaji ili kutimiza azma yake miaka ijayo.

Binti huyu anasema kuwa tangia akiwa mtoto alidhamiria kuhitimu kuwa daktari wa moyo.

Huyu sio mwingine ila Michelle Wambui Kimani ambaye kisanaa anafahamika kama Mishie.

Kando na uigizaji, chipukizi huyu ni mnenguaji viuno (dancer), mwanamitindo na msanii wa sauti ya matangazo (voice over artist).

”Katika mpango mzima ninajivunia kuwa mwana maigizo ambapo nimepania kushiriki filamu za Hollywood,” amesema.

Mwigizaji Michelle Wambui Kimani ambaye kisanaa anafahamika kama Mishie. Picha / JOHN KIMWERE

Anaongeza kuwa msanii Mkenya aliyezaliwa nchini Mexico, Lupita Nyong’o ndiye humtia moyo zaidi kuwa anastahili kupambana bila kupumua.

Lupita ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Wakanda’ bila kuweka katika kaburi la sahau filamu iitwayo  ’12 Years a slave’ iliyomshindia tuzo ya Oscar Awards mwaka 2012.

Hata hivyo anasema mapenzi ya filamu yalimsukuma pakubwa kuanza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2019 chini ya kundi la Vuma Productions.

Kwa jumla anajivunia kufanya kazi na makundi kama Zamaradi Production, Kikwetu Production, Zebra Production na Multan Production.

Anajivunia kushiriki filamu kama ‘Kina,’ ‘Sky Girls,’ ‘Paa’ ‘Salem,’ Adiel TV,’ ‘Mino,’ na ‘Selina.’

Anadokeza kuwa kati ya filamu hizo ‘Mino,’ na ‘Paa’ huwa zinamvutia zaidi kuliko zingine.

Anashikilia kuwa katika uigizaji wake analenga kufuata nyayo za kati ya waigizaji mahiri duniani akiwamo Zoe Saldana mzawa wa Marekani.

Mwigizaji Michelle Wambui Kimani ambaye kisanaa anafahamika kama Mishie. Picha / JOHN KIMWERE

Zoe ameshiriki filamu kibao ikiwamo ‘I kill Giants,’ ‘Colombiana,’ ‘Takers,’ na ‘The Losers,’ kati ya zingine.

Hapa nchini anasema angependa kujikuta jukwaa moja na wasanii kama Brenda Wairimu ‘Subira,’ na Kate Actress ‘Nafsi.’

Kimataifa angependa kushirikiana na wenzake kama Thuso Mbedu ambaye ni mzawa wa Afrika Kusini aliyeshiriki filamu kama ‘Woman King.’

Mwingine akiwa Mercy Johnson mzawa wa Nigeria aliyeshiriki filamu kama ‘Heart of a fighter,’ ‘The Maid,’ na ‘Weeping soul,’ kati ya zingine.

”Sina shaka kutaja kuwa wapo waigizaji ambao huvuna vinono zaidi pia ni taaluma inayosaidia baadhi yetu lakini ukweli wa mambo ina changamoto kibao,” akasema.

Chipukizi huyu aliyetua duniani mwaka 2000, sio mchoyo wa mawaidha anashauri wenzie wa kike wanaokuja kuwa lazima wajitahidi pia wafahamu hakuna mteremko bali ni sekta yenye ushindani mkali.

Anawahimiza wawe wabunifu pia wajitokeze kupigania nafasi adimu zinazopatikana bila kuhofia waliowatangulia.

Aidha anawashauri wasiwe na pupa ya kupata umaarufu pia nyakati zote wajiheshimu na kumweka Mungu mbele kwa chochote wanachofanya.

Hata hivyo, anatoa wito kwa wenzao waliowatangulia  kuwashika mkono na kuwapa mawaidha jinsi ya kazi ya uigizaji ili kufanikisha azma yao maishani.

  • Tags

You can share this post!

Madereva 2 watozwa faini jumla Sh170, 000 kwa kusababisha...

June anavyowika tasnia ya uigizaji

T L